Makala

MSHAIRI WETU: Sophy Onura 'Johari Mwana Zawadi'

March 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MBALI na kupitisha ujumbe maalum kwa wanajamii, ushairi ni sanaa ambayo imeibukia kuwa kipengele mahususi cha burudani.

Ushairi ni fani pevu ya fasihi ambayo mbali na kutoa picha kamili ya jamii na kuwasilisha mawazo ya mtunzi, pia huinua kiwango cha umilisi wa lugha.

Katika kusoma, kukariri au kughani; mashairi huhimiza, huelimisha, huonya na kukemea maovu yanayofanywa na wanajamii kwa njia taratibu.

Hivyo, mashairi hulenga kupitisha ujumbe wa mafunzo mbalimbali na kuipa jamii mwelekeo.
Huu ni mtazamo wa mshairi Sophy Onura ‘Johari Mwana Zawadi’.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Nilizaliwa mnamo 1991 katika eneo la Nyanza Kusini nikiwa kitindamimba katika familia ya mama Peris na marehemu Bw W.O. Onura aliyekuwa meneja katika kampuni ya Londiani Timber na baadaye akawa chifu wa Lokesheni ya Getenga.

Ulisomea wapi?

Nilianza masomo ya chekechea katika Shule ya St Ann’s kisha nikahamia mjini Bungoma kusomea katika Shule ya Msingi ya Bungoma D.E.B.

Nilijiunga baadaye na Shule ya Upili ya Namachanja, Bungoma kabla ya kuelekea Itierio High, Kisii nilikofanyia mtihani wa KCSE.

Nilisomea ualimu katika Chuo cha Walimu cha Kericho, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kujiendeleza kitaaluma katika Kiswahili na somo la Jiografia.

Nini kilikuchochea kuupenda ushairi?

Mapenzi yangu kwa Kiswahili, uandishi na msukumo wa kutaka kuelimisha watu kuhusu mambo mbalimbali kwa njia isiyo ya kuleta mitafaruku.

Ulitunga lini shairi lako la kwanza?

Mnamo 2002, nikiwa mwanafunzi wa shule ya msingi.

Mashairi yako huegemea zaidi mada zipi?

Hupania kujadili masuala ibuka katika jamii kama vile ukabila, siasa, ufisadi, ubinafsi, njaa, mafuriko, maradhi na elimu.

Nini hukuongoza kuteua mada hizo?

Kinachonipa dira katika uteuzi wa mada ni mazingira ninamojipata wakati wa utunzi wa mashairi mbalimbali. Masuala ya kuangazia pia katika ushairi huchochewa na hali zinazowakabili wanajamii kadri wanavyojitahidi kujiendeleza kiuchumi, kisiasa, kitamaduni na kisayansi.

Hukuchukuwa muda kiasi gani kutunga shairi moja?

Nahitaji takriban dakika 45-60 kusarifu na kuhakiki ipasavyo shairi moja aina ya tasdisa la kati ya beti sita na nane.

Mbona mashairi ya arudhi?

Kwa sababu ni rahisi kuyaghani na urari wa vina huwanata zaidi wasomaji na wasikilizaji. Mbali na kuleta ujumi huo kwa sikio la mpokeaji, mashairi haya ndicho kipimo halisi cha ukomavu wa mtunzi.

Ushairi umekuvunia tija gani?

Baadhi ya mashairi yangu yamefana pakubwa katika mashindano ya kiwango cha shule za msingi kwenye tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Nimewahi pia kutambuliwa na kutuzwa nikiwa mwanafunzi katika Chuo cha Walimu cha Kericho kwa kuibuka bora katika mashindano mbalimbali ya kutunga na kughani mashairi.

Ushairi umenipa marafiki wengi ambao kwa sasa hufuatilia tungo zangu katika gazeti hili kila wikendi.

Una mipango ipi ya baadaye kuhusiana na ushairi?

Ninapania kuandika diwani kadhaa ingawa tayari nimejumuisha mashairi machache katika vitabu vyangu vya hadithi kama vile ‘Dua ya Faraja’.

Mbali na kutunga na (au) kughani mashairi, unafanya nini kingine?

Mimi ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Juja Preparatory, Kaunti ya Kiambu.

Unawashauri nini chipukizi na watangulizi wako katika taaluma?

Chipukizi wazidi kupiga hatua bila ya kufa moyo. Wajitahidi kujitofautisha na watu wengine ili wajikuze kitaaluma. Washairi wa zamani wazidi kuwashika limbukeni mkono.