Makala

Mshtuko kijijini msichana aliyefaa kuanza chuo Septemba kuuliwa na mpenziwe

Na WYCLIFFE NYABERI September 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

FAITH Kemunto Obino, 20, alitoweka nyumbani kwa wazazi wake kijijini Nyamonuri, eneobunge la Mugirango Kaskazini, Kaunti ya Nyamira takriban mwezi mmoja uliopita.

Familia yake ilianza kumtafuta lakini juhudi zao zote ziliishia patupu.

Kwa kuwa alipaswa kujiunga na Chuo Kikuu cha Machakos mwezi huu wa Septemba, familia yake ilitafuta usaidizi wa polisi ili kujua aliko.

Waliripoti kutoweka kwake katika Kituo cha Polisi cha Nyamusi, Nyamira Kaskazini.

Kwa muda wote aliokosekana, simu yake ilibaki imezimwa.

Lakini ilipofika Jumapili iliyopita, wakati msako ulipokuwa unaendelea, familia yake ilipokea ujumbe mfupi kutoka kwa nambari ya simu ya Faith.

Mwili wa Faith Kemunto (uliomo katika begi) baada ya kufukuliwa mnamo Septemba 4, 2025 katika kijiji cha Maosi, Nyamira. Marehemu inasemekana aliuawa na mpenzi wake kabla ya kuzikwa kwa siri kwenye kaburi lenye kina kifupi kwenye chimbo lililo kando ya barabara. Picha|Wycliffe Nyaberi

Ujumbe huo ulitumwa kwa simu ya kakake na mtu aliyeuandika alidai kuwa alikuwa rafiki ya Faith ambaye alikuwa na uhusiano wa kimapenzi naye.

SOMA PIA: Polisi wasaka mwili wa binti anayesemekana kuuawa na mpenziwe na kuzikwa pangoni

Jamaa huyo ambaye ametambuliwa kama Gideon Makori, inasemekana alimwomba kakake Faith amtumie Sh500 lakini ombi lake lilikataliwa.

Siku moja baadaye, kakake Faith alipokea ujumbe mwingine kutoka kwa nambari ile ile aliyokuwa akiitumia dadake.

Ujumbe huo safari hii ulikuwa na habari za kuvunja moyo kulingana na mjomba wa Faith, Maroko Maina.

Ujumbe huo wa arafa ulisema hivi, kulingana na Bw Maina: “Fay tulimuua na tukamzika!”

Jamaa huyo aidha alitoa maelezo ya mahali walikomzika binti huyo katika kaburi lisilo na kina kirefu kwenye machimbo ambayo yako kando ya barabara moja ya humo kijijini.

Alipopokea habari hii ya kushtua, kakake Kemunto alikimbia nyumbani kuwaarifu wazazi wake.

Wakaelekea Ekerenyo kuripoti suala hilo tena kwa polisi. Polisi waliandamana na wazazi wa Kemunto hadi pahali ambapo walikuwa wameambiwa mwili wa mpendwa wao ulikuwa umezikwa kisiri.

Walipofika katika machimbo hayo, walianza kufukua pahali walikodhani kulikuwa kunaonekana kuchimbwa.

Baada ya kuondoa mchanga kiasi, walikutana na kitu kilichofanana na mwili wa binadamu.

Walisitisha shughuli hiyo kwa ushauri wa polisi hadi wapate kibali cha mahakama kuhusu kumfukua maiti kama inavyohitajika kisheria.

Tangu siku hiyo, familia hiyo imekuwa ikikesha katika machimbo hayo hadi siku ya Alhamisi ambapo mwili wa binti huyo ulifukuliwa na kikosi cha maafisa wa serikali kutoka vitengo mbali mbali vya kiusalama na idara ya afya.

Mwili huo ulipoondolewa katika chimbo hilo, wazazi wa Faith waliutambua kuwa alikuwa wake. Hali ya huzuni ilitandaka kijiji hicho siku nzima wakati shughuli hiyo ya ufukuzi ilipokuwa ikifanywa.

Wakizungumza na wanahabari hapo mbeleni baada ya habari kuhusu alikokuwa amezikwa mwanao kuwafikia, wazazi wa Kemunto walisema kwamba binti yao aliondoka nyumbani zaidi ya mwezi mmoja uliopita baada ya mwanamume huyo kutoroka naye.

Wananchi wa kijiji cha Maosi, Nyamaiya, Kaunti ya Nyamira waangalia kwa mshangao shughuli ya ufukuzi wa maiti ya Faith Kemunto mnamo Septemba 4,2025. Picha|Wycliffe Nyaberi

Mamake marehemu, Grace Nyaitondi alisema alijua bintiye alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani ambaye hata hivyo hakuwa amemleta nyumbani kwa utambulisho.

Bi Nyaitondi alisema kuwa wakati fulani, alimwambia bintiye azingatie masomo yake kwanza lakini akaazimia kuwa katika uhusiano na mwanamume huyo.

Babake Kemunto, Charles Obino hakuamini kilichompata kitindamimba wake na alimtaja kama mtu mchapa kazi.

Aliwataka polisi kuwasaidia kutegua kitendawili cha kifo cha mwanawe.

“Binti yangu alikuwa msichana mchapakazi. Sina la kusema zaidi ya kuomba mamlaka watusaidie kujua ukweli,” Bw Obino alisema.

Jamaa huyo anayedaiwa kumuua binti huyo anasemekana kukamatwa Alhamisi asubuhi.

Tukio hili la ajabu limewaacha wengi na mshangao.