Makala

Mshukiwa wa mauaji alivyotia wakazi hofu kwa kutoa ‘orodha’ ya anaotaka kuchinja

April 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UPDATE: Kamanda wa polisi Murang’a Kainga Mathiu amethibitisha kukamatwa kwake

Na MWANGI MUIRURI

WENYEJI wa kijiji cha Chui kilichoko eneo bunge la Mathioya, Kaunti ya Murang’a wamelalamikia kuzembea kwa maafisa wa polisi kumtia mbaroni mwanamume ambaye tayari ameua watu wanne na kutangaza kwamba analenga wengine wanane.

Kati ya walio katika orodha hiyo ya kulengwa kwa mauti ni pamoja na naibu wa chifu na kamanda wa polisi wa eneo hilo.

Mshukiwa wa mauaji hayo yuko mafichoni licha ya kudaiwa kuonekana mara kwa mara katika eneo hilo.

Anasemekana kwamba mwaka wa 2015 aliwaua Bw Joseph Geita na mkewe Bi Keziah Muthoni katika kijiji hicho, akaenda rumande kwa miaka saba na mwaka wa 2022 akaachiliwa.

Baada ya kuishi katika kijiji hicho kwa miaka miwili akiwa huru, inadaiwa aliwavamia na kuwaua kwa upanga Bw Stanley Kamau na Bw Bernard Mahiu mnamo Machi 22, 2024. Miili ya wote wawili ilipatikana nje ya kambi ya polisi ya Chui mwendo wa saa nne usiku wakiwa na majeraha ya upanga vichwani.

Kambi hiyo licha ya kukamilishwa kujengwa mwaka wa 2016, haijawahi kupokezwa maafisa wa kuhudumu, wenyeji wakilaumu serikali kwa kuwaweka katika hatari za utovu wa usalama.

Wawili hao walizikwa Jumanne Aprili 2, 2024 katika kijiji hicho, waombolezaji wakiteta kwamba wanaishi kwa taharuki kwa kuwa mshukiwa alidai kwamba kuna wengine wanane ambao hajatimizia hukumu ya mauti.

Lakini wale walio katika orodha hiyo na ambao tayari wameshauawa ni wanaume wawili huku ikibakia wengine wanane—wanawake sita na wanaume wawili.

Mshukiwa huyo licha ya kusemekana kwamba huonekana akirandaranda katika barabara za eneo hilo, hajatiwa mbaroni wenyeji wakisema taharuki waliyo nayo haina kifani.

“Sisi tunaishi kama watahiniwa wa mauti ambapo ni dakika yoyote ujipate umekatwakatwa kama mutura sokoni. Licha ya kwamba tunajua majina ya walio katika orodha ya mshukiwa, hatujui kama atabadilisha nia na aisanifishe ili iwe na majina mapya,” akasema Bi Lucy Marara.

Kamanda wa polisi wa Kaunti ndogo ya Mathioya Bw Antony Muriuki aliambia Taifa leo Dijitali kwamba maafisa wake wanatia bidii kumsaka mwanamume huyo huku akiomba usaidizi zaidi kumnasa.

“Hatujui jinsi mahakama ilimwachilia mwanamume huyo na akarejea kijijini humo na ambapo sasa anashukiwa kutekeleza mauaji hayo mawili.”

Bw Muriuki alifichua kwamba mshukiwa huyo alikuwa aue watu wanne usiku huo wa Machi 22 “lakini wawili wakafanikiwa kuhepa na wakajifungia ndani ya nyumba zao”.