Makala

MSIFIKIRI NI MTEREMKO: Vijana wakusanya sahihi kupiga chini uteuzi wa mawaziri 14

Na FRIDAH OKACHI July 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VIJANA nchini bado wanaendelea na kupambana na uongozi mbovu, baada ya kundi la Bunge of Mayut-Kenya kuanza mchakato wa kukusanya sahihi za vijana kutoka kaunti ya Nairobi na Kiambu kupinga uteuzi wa mawaziri 14.

Mwanzilishi wa mchakato huo Bi Nerima Were alisema uteuzi uliofanywa na Rais William Ruto ni kinyume na Katiba ya Kenya Kifungu cha Sita.

“Kuna hati iliyowekwa kwenye mtandao. Tunaomba vijana wajitokeza kwa kuleta ombi hilo kwa kutia sahihi, kuweka jina na mahali wanapoishi ili kuwaondoa mawaziri hao,” alisema Bi Were.

Kwa wale ambao wangependa kuhusika kwenye zoezi hilo, mwazilishi huyo alisema wahusika wanahitaji kuandika jina na mahali wanapoishi na kupeleka ombi hilo kwenye maeneo yaliyotengwa ya kukusanya sahihi hizo. Hata hivyo, zoezi lina mawakili wa kujitolea ambao wanahusika kuweka muhuri.

“Ni zoezi la siku tatu ambalo lilianza Ijumaa. Litaendelea Jumatatu na Jumanne. Wale mawakili wa kujitolea wanapatikana katika jumba la Equity Plaza, Kaunti ya Thika kwa wakazi wa Juja, Kimbo na maeneo mengine, Dullo advocates kwenye barabara ya Ngong, Jumba la Bazaar na la Kimataifa- ghorofa ya tisa kwenye barabara ya Mama Ngina jijini,” alisisitiza.

Mawakili hao, pia wana jukumu la kuelekeza vijana jinsi ya kufanya zoezi. Pia Bi Were alisema kutokana na muda kuwa mchache na kukosa kufika kwenye kaunti 45 bado vijana wanaweza kushiriki.

“Tunahitaji sahihi zaidi ya milioni na ili kufikisha, vijana walio kwenye kaunti zingine wanaweza kuma jina na eneo la kuishi, wakiambatanisha na sababu kwa nini waziri mteule hafai,” aliongeza.

Mwazilishi huyo alisema mawaziri 14 ambao ni Opiyo Wandayi, John Mbadi, Hassan Joho, Wycliffe Oparanya, Prof Kithure Kindiki, Alice Wahome, Soipan Tuya, Aden Duale, Divis Chirchir, Rebecca Miano, Alfred Mutua, Onesmus Kipchumba Murkomen na Justin Bedan Njoka wanaweza kupitishwa kwenye Bunge na kuidhinishwa kwa siku za hivi karibuni kinyume na katiba.

Aliongeza kuwa Rais alifanya kinyume na ahadi aliyokuwa ametoa wakati wa maandamano ya Gen Z yalikuwa yameshika kasi. Pia, mchakato huo unalenga sheria ya thuluthi mbili ya jinsia kukosa kufuatwa ipasavyo.

“Inasikitisha sana, rais kuteua waziri aliye na umri wa miaka 60. Wakati wa hotuba alisema wafanyakazi wa serikali walio na zaidi ya miaka hiyo wataenda nyumbani. Angalia kwenye uteuzi huo, nafasi ya kijana ni mmoja, nafasi ya wanawake kati ya 14 ni wawili.”

Ijumaa jioni (Julai 26,2024) Taifa Leo ilitembelea jumba la Bazaar na jumba la Kitaifa ambapo shughuli ya ukusanyaji sahihi kutathimini hali ilivyokuwa inaendelea. Wakili Nyokabi Njogu (Bazaar) alisema idadi ya vijana waliojitokeza ilikuwa wachache muno. Wengi walikifika bila ombi hilo.

“Wengi wanaofika hapa wana ari ya kushiriki zoezi hili lakini inabidi niwaelekeze jinsi ya kufanya,” Alisema Bi Njogu.