Makala

MWANAMKE MWELEDI: Msomi, mtafiti na mtaalamu katika masuala ya kijamii

March 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KEYB

KAZI yake inazidi kuwa na mchango mkubwa humu nchini na kimataifa.

Jina lake ni Judith Mbula Bahemuka, profesa katika Chuo Kikuu cha Nairobi, vilevile mwanasoshiolojia aliye na utaalamu katika masuala ya ustawi wa maeneo ya mashambani.

Hasa kazi yake imeangazia jinsi ya kupunguza umaskini kupitia mifumo ya kilimo ili kuimarisha maisha katika maeneo ya mashambani.

Aidha, amejiundia jina kutokana na mchango wake katika kuangazia mchango wa wanawake katika ustawi wa kilimo.

Judith anatambulika kama mojawapo ya watu waliotaalumika sana nchini. Mwaka wa 1970, alihitimu na shahada ya sanaa kutoka Marygrove College nchini Amerika. Baadaye, alihitimu na shahada ya uzamili, kisha ya uzamifu katika sanaa na soshiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Mbali na hayo, Judith pia ana hati katika masuala ya kilimo cha kimataifa na ustawi wa maeneo ya mashambani kutoka Chuo Kikuu cha Cornell, nchini Amerika.

Pia, ana hati ya mahusiano ya kimataifa kutoka taasisi ya Humphrey Institute, Chuo Kikuu cha Minnesota, Amerika. Aidha, alipewa shahada ya utambuzi kutoka chuo cha Kalamazoo, vilevile chuo cha Trinity College, nchini Amerika.

Mbali na hayo, Judith pia amehudhuria hafla mbali mbali za mafunzo kama vile Hubert Humphrey Fellowship, kutoka mwaka wa 1982 na 1984, University of Nairobi Graduate Teaching Fellowship, kati ya mwaka wa 1974 na 1977.

Taaluma yake ndefu imemwezesha kuhudumu katika viwango mbalimbali na kupata uzoefu katika sehemu tofauti. Amefanya kazi na afisi ya kitaifa ya kukabili virusi vya HIV tokea kuanzishwa kwake ambapo alihusika pakubwa katika harakati za kutathmini maradhi ya Ukimwi nchini kati ya mwaka wa 1992 na 1993.

Kati ya mwaka wa 1994 na 1998, alihudumu kama profesa wa Chuo Kikuu cha Nairobi, na pia akafanya kazi kama mwenyekiti wa Idara ya Soshiolojia ya chuo hicho.

Katika kipindi hiki, kati ya mwaka wa 1995 na 1997, alishiriki katika maandalizi ya stakabadhi kuhusu virusi vya HIV, ambapo alisimamia kamati kuhusu wanawake, watoto na maradhi ya Ukimwi.

Mwaka wa1997, alikuwa mwenyekiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Sanaa (UNESCO) katika masuala ya Elimu, Afya na Ustawi wa Wanawake ambapo alihudumu hadi mwaka wa 2003 alipotawazwa kama mwakilishi wa kudumu wa Kenya, na Balozi wa Umoja wa Mataifa jijini New York. Alihudumu katika nafasi hii hadi mwaka wa 2006.

Mwaka wa 2000 alianzisha kituo cha International Learning Centre katika Chuo Kikuu cha Nairobi na kuhudumu kama mkurugenzi wake wa kwanza.

Kufikia sasa, kituo hiki kimeunda makala ya hali ya juu ya kitaalamu chini ya mwamvuli wa East Africa in Transition. Judith pia alikuwa mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya sayansi ya kijamii na ubinadamu katika tume ya kitaifa ya UNESCO, na kuiwakilisha Kenya katika bodi ya utendaji ya shirika hili hili.

Judith ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Upili ya Loreto Convent Msongari, pia amehudumu katika bodi kadhaa za kitaifa kama vile mwanachama wa bodi ya mpango wa kitaifa wa biashara katika maeneo ya mashambani (KREP).

Pia amewahi kuwa naibu mwenyekiti wa tume ya elimu ya juu, ambayo kwa sasa inafahamika kama Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu. Mwaka wa 2013, aliteuliwa kama chansela wa Chuo Kikuu cha Eldoret.

Kimataifa, amefanya kazi kwa karibu na shirika la Global Partners Project nchini Amerika.

Mbali na hayo, amewahi kushikilia nafasi kama Balozi wa Kenya nchini Canada na Cuba kati ya mwaka wa 2006 na 2009.