Mtambo maalum kupima ubora wa chakula cha mifugo
LICHA ya wakulima kulemewa na gharama ya juu ya chakula cha mifugo kuendeleza ufugaji, ubora wake pia umekuwa wa kutiliwa shaka.
Hii ni kutokana na utapeli unaosakatwa na baadhi ya kampuni na viwanda vya kuunda chakula cha mifugo.
Kero hii imekita kambi kote; kuanzia ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, mbuzi, kondoo, nguruwe, na hata kuku, suala ambapo huchangia wafugaji kukadiria hasara bin hasara.
Hali hiyo ni sawa na kutia chumvi kwenye kidonda kinachouguza.
Kukabiliana na changamoto hii ya chakula duni kisicho na ubora, Agrifirm, kampuni ya ushirika wa wakulima kutoka Uholanzi, inahamasisha wakulima kukumbatia kifaa cha kupima ubora wa chakula cha mifugo na malighafi kinachojulikana kama Evaluemate.

Mtambo huu wa kisasa utasaidia wafugaji kutathmini ubora wa lishe katika chakula cha mifugo.
Dkt Charles Kigen, Meneja wa Mauzo Agrifirm, anaeleza kuwa kifaa hiki kinafanya kazi kwa kutumia mifumo ya upangaji wa kalibrasheni (calibration lines) iliyohifadhiwa kwenye wingu (cloud).
Aidha, kinafanya uchambuzi wa vipengele vya kemikali katika chakula cha mifugo na malighafi kwa kupima mwangaza unaoakisiwa.
“Teknolojia hii hutumia mwangaza kuangazia malighafi na kuchambua mwangaza unaoakisiwa. Kwa kulinganisha mwangaza huu na mifumo ya awali iliyopangwa kulingana na virutunisho maalum, hutoa matokeo kuhusu uwepo wa kemikali.

“Kwa mfano, kiwango cha protini hutambuliwa kwa kupima viwango vya nitrojeni kwa kuzingatia kiasi cha mwangaza ulioakisiwa,” Dkt Kigen anafanua.
Teknolojia hii hutumia algorithimu ya hesabu kupima ubora wa protini, nishati, wanga, mafuta, na fiber katika chakula cha mifugo, ambavyo ni vigezo muhimu katika uundaji wa lishe bora ya mifugo.

Evaluemate, ni kifaa ambacho kinaweza kuunganishwa na simu ya mkono yaani rununu, na kina skana ya ndani inayotoa matokeo papo hapo wakati wa kupima chakula cha mifugo na malighafi.
Kinatengenezwa na kampuni nyingine, Agrifirm ikihusika na kuunda kalibrasheni inayotumika kwenye kifaa hiki.
Ni ununifu utakaowawezesha wafugaji kupima ubora wa bidhaa zao, kufanya uchambuzi wa awali, na kutambua sampuli zinazohitaji uchunguzi wa kina zaidi.

“Sampuli zinazotumika kuunda mifumo ya kalibrasheni hukusanywa kutoka maeneo ya ndani na kuchunguzwa katika maabara yaliyothibitishwa na kupitishwa na ISO (International Organization for Standardization). Data yake huunda mifumo ya kalibrasheni inayoifanya teknolojia hii kuwa sahihi na ya kuaminika,” Dkt Kigen anafafanua, akibainisha kuwa kiwango cha mafanikio ya kifaa hiki ni zaidi ya asilimia 80.
Hata ingawa teknolojia hii ni mpya katika sekta ya chakula cha mifugo, imekuwa ikitumika katika uchimbaji madini na upimaji wa udongo.
