Makala

Mtandao wa ufyonzaji mafuta watia doa mji wa Makutano

May 16th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

MTANDAO wa wizi wa mafuta ya magari katika mji wa Makutano ulioko katika mpaka wa kaunti za Kirinyaga na Embu umeharibu mazingira kando na kutwika uchumi wa kitaifa hasara ya kukosa ushuru.

Magenge ya vijana wanaodaiwa kufadhiliwa na mtandao wa mabwanyenye, madalali na maafisa wa polisi, hutegea madereva wa malori ya serikali na wawekezaji wa kibinafsi na kuwashurutisha wawauzie mafuta.

Aidha, raia wa kawaida akiacha gari lake nje ya majengo ya mji huo, huwa linavamiwa na mafuta yake kukamuliwa.

Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini mtandao huo wa magendo huumiza miradi ya serikali ambapo wanakandarasi kama wa kujenga barabara na kuchimba mabwawa walikiri kuwepo kwa mtindo wa wafanyakazi wao kuiba mafuta ya magari na ya matingatinga na kuyauza kwa mawakala ambao huyasafirisha hadi mji wa Makutano kuyauza kwa soko kubwa la magendo.

Wadau sasa wameungama kwamba mtandao huo unafaa kuzimwa huku kukichipuka habari kwamba baadhi ya makamanda wa polisi na maafisa wa utawala huchukua hongo kuulinda.
Ripoti ya ujasusi ya Mei 13, 2024, yenye nambari rasmi EMB2259778 ilisema kuna baadhi ya maafisa wa vitengo vya usalama walio katika makao makuu ya eneo la Mlima Kenya Mashariki na pia katika Kaunti ya Embu ambao hupewa hongo, kulinda mtandao huo.

Ripoti nyingine ambayo rekodi yake rasmi ni EMB2259778 ilisema kwamba kituo cha polisi cha Makutano ambacho kinafaa kuwajibikia suala hilo, huwa inafumbia macho uovu huo.

“Baadhi ya maafisa wa kituo hicho cha Makutano huchukua hongo kwa niaba ya baadhi ya wakubwa wao kiasi kwamba biashara hiyo haramu hata hushirikishwa katika lango la stesheni hiyo,” ripoti hiyo ikasema.

Mshirikishi wa kundi la uhifadhi wa mazingira katika ukanda wa Mlima Kenya (CRECAG) Bw James Musila, aliambia Taifa Leo kwamba biashara hiyo haramu husababisha umwagikaji wa mafuta katika maeneo mengi ya mji huo.

“Kunaponyesha, mafuta hayo ambayo yamemwagika katika mchanga husafirishwa hadi katika Mto Tana ulioko karibu na kuishia kuua samaki, mamba na wanyama wengine ambao huishi ndani ya maji hayo,” akasema Bw Musila.

Aliongeza kwamba mafuta hayo pia huufanya udongo wa mashamba ya eneo hilo kukosa rotuba kwa kuwa hupoteza uwezo wa mchanga kuingiwa na hewa safi.

Bw Musila aliongeza kwamba “hiyo ni kero kubwa na halisi na ambayo inafaa kuingiliwa na Mamlaka ya Kutunza Mazingira Nchini (Nema)”.

Hata hivyo, ukora huo husemwa kwamba hauwezi ukazimwa kwa urahisi kwa kuwa licha ya kutekelezwa hadharani, maafisa wa serikali hufungwa macho na mikono na hongo ambazo hutandazwa, biashara kwa siku ikisemwa kuwa ya takriban Sh1.5 milioni.

“Mimi nilijaribu kupambana na mtandao huo lakini ukanilemea kwa kuwa mamlaka husika ya kuthibiti biashara ya mafuta na gesi (Epra) ilikataa kutuunga mkono,” akadai aliyekuwa Naibu Kamishna wa Kaunti ndogo ya Mwea Bi Jane Manene.

Bi Manene alisema “yale ambayo huendelea katika mji huo kuhusu mafuta ni biashara kubwa, hatari na haramu”.
Aliongeza kwamba makateli hao huficha mafuta hayo katika nyumba zilizo karibu na za wapangaji na kwa bahati mbaya ikiwa kutazuka ajali ya moto kuna zaidi ya watu 200 wataathirika.

Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini Bw Gitonga Murungi alisema hasara kubwa ni kwa wamiliki wa magari na pia mitambo ya jenereta.

“Mafuta hayo huwa chafu na hata uhifadhi wayo katika madanguro hauzingatii usalama na ubora. Wanaoishia kuuziwa mafuta hayo hujipata wamehadaiwa ambapo wakati mwingine huwa yamechanganyishwa na maji au kemikali nyingine,” akasema Bw Murungi.

Bw Murungi alisema watu wa Murang’a Kusini ambao ni majirani wa mji huo huathirika sana kupitia magari yao kuharibika.

“Kando na uchumi wetu kupoteza pesa kupitia biashara hiyo haramu, ubora wa miradi ya serikali hudhoofika kwa kuwa mwanakandarasi anapokumbwa na wizi wa mafuta wa malori na matingatinga yake, huwa anafuta hasara hiyo kupitia kupunguza ubora wa miradi,” akasema.
Aidha, Bw Murungi alisema kwamba hakuna mtu aliye na ruhusa ya kushiriki biashara ya mafuta bila kuwa na leseni rasmi ili serikali idhibiti usalama wa maeneo ya biashara hizo kwa majirani wake.

Magenge hayo ya wizi wa mafuta husemwa kuwa kiini cha kuzorota kwa usalama katika baadhi ya vishoroba vya mji huo wa Makutano.

Aidha, kwa kuwa magenge hayo hujipa pesa za haraka na ambazo hutumiwa katika kuponda raha, ukahaba katika mji huo huwa wa juu.

“Inasikitisha kuona wasichana wadogo wakiingia kwa mtego wa kuvutiwa na pesa hizo na kuishia kutungwa mimba na wahalifu hao,” akasema mwenyeji ambaye aliogopa kufichua jina lake.
Alisema uhalifu wa ubakaji na ulawiti katika mji huo huathiri watoto, walemavu na wake kwa waume wazima.

“Kisa cha ajabu ni kwamba tumekaa kwa muda bila kuwa na chifu baada ya aliyekuweko kufutwa kazi kutokana na ufisadi huku maafisa wengine kadha walio katika huduma wakikosa uwezo wa kukabiliana na genge hilo,” akasema mwenyeji huyo.

[email protected]