• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Mti wa kitamaduni ulioanguka unavyozua hofu   

Mti wa kitamaduni ulioanguka unavyozua hofu  

NA OSCAR KAKAI

KWA  karne nyingi, mti  mtakatifu  wa kiasili wa jamii ya Pokot kwa jina Mnagei ama Simotwo(Fig Tree) uliheshimika na jamii hiyo ambayo inaishi katika eneo la Kaskazini mwa Kenya kama wa kuleta baraka.

Mti huo mkubwa na mzito ambao hutoa mizizi yake juu, katika mtaa wa Bendera, eneo la Karas mjini Kapenguria barabara kuu ya  Kitale –Lodwar, ulianguka karibu miaka miwili iliyopita na kuleta hofu miongoni mwa wakazi.

Tangu uanguke, hakuna mtu ameuharibu kwa njia ya kuushika ama kukata sehemu ya mti huo au kuutumia kama kuni, mbao.

Jamii ya Pokot bado haijakubali hali hiyo kutokana na kuanguka kwa mti huo maarufu kama Mugumo katika jamii ya Agikuyu, ikisema kuanguka kwake kunaashiria kitu fiche ambacho wazee bado hawajatabiri.

Mti huo ambao una mandhari mazuri ya kuvutia ulikuwa ukitumika kama eneo la wazee la kuabudu.

Bado unachukuliwa kama ishara ya baraka na mafanikio.

Kulingana na wazee, mti huo hauna tu historia ya kipekee bali unaiendeleza.

Wazee wanataka tambiko kufanyika, huku viongozi wa kidini wakipuuzilia mbali suala hilo ambalo wanasema kuwa hauna maana yoyote na haufai kuwapa hofu wakazi.

Ni chini ya mti huo ambao mfalme wa Uhabeshi Menelik 11 alifanyia maombi mwaka wa 1895.

Malkia wa mfalme huyo, Ras, alikuwa anaishi eneo la Karas mjini Kapenguria baada ya jamii ya Pokoto kuita eneo hilo Ka (wa) Ras.

Mti huo wa Mnagei ndio ulizaa wadi na Lokesheni ya Mnagei, Pokot Magharibi ambayo ndiyo makao makuu ya kaunti hiyo mjini Kapenguria.

Mwenyekiti wa baraza la jamii ya Pokot Mzee John Muok anasema kuwa wazee wanapanga kufanya tambiko kuhusu mti huo.

“Gavana wetu Simon Kachapin na mbunge wa Kapenguria Samuel Moroto wanafaa kuwapanga wazee kufanya shehere hiyo. Hatujui tutaenda wapi. Tunaomba Mungu atupe mti mwingine. Tunataka viongozi waje pamoja na kufanya tambiko la kusafisha mti huo,” alisema.

Hata hivyo, wakazi wametoa hisia zao kutokana na mti huo ambao wanasema ulihusika pakubwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti, 2022 ambapo baadhi ya viongozi kwenye kaunti hiyo walipoteza viti, wengine wakisema kuwa hakuna haja wakazi kuwa na hofu kwa sababu mti huo ulianguka kutokana na uzee wake.

Wengine wanasema kuwa wakati mti wa Mnagei unapoanguka, unaashiria mambo mazuri ama mabaya na tambiko la kusafisha hufanywa ili kufurahisha miungu.

Mti huo ambao huchukuliwa kama ngome ya roho una zaidi ya miaka 100.

“Jibu liko na wazee kwa sababu wanawasiliana na miungu kuwapa jibu,”alisema mzee Harrison Loyatum.

Bw Loyatum anasema kuwa mti huo ulianguka kwa amani bila kuharibu chochote na wakazi hawafai kuwa na wasiwasi kwani mambo mazuri yapo njiani.

“Mti huo uliangukia upande wa kulia na kwa jamii yetu wakati mwanamume anafariki na kuzikwa anaangalia mlima Mtelo. Nyuki wako ndani lakini hawajasumbua yeyote. Paipu za maji, barabara na stima hazikuharibiwa,” anasema.

Alisema kuwa mti huo ulifeli kuangalia Mashariki, hilo likiashiria ufanisi.

Wengine husema kuwa mwisho wa mti huo haumaanishi chochote, bali ni uzee tu.

Mwana utamaduni wa jamii ya Pokot, Mzee William Lopetakou alisema kuwa mti huo uliangukia upande wa Mashariki ishara ya baraka kwa jamii.

“Ingekuwa mti huo uliangukia upande wa Magharibi, ingekuwa laana na bahati mbaya kwa jamii,” anasema.

Mzee huyo anasema kuwa kuanguka kwa mti huo kunaonyesha kuisha kwa msimu fulani na mambo mazuri yatafanyika katika eneo hilo.

“Mti huo ulikuwa umezeeka na ukaanguka kama jinsi binadamu hufariki,” anasema.

Alisema kuwa umekuwa eneo hilo kabla hata jamii ya Pokot kuhamia eneo hilo.

“Jamii yetu ilikuwa ikifanyia tambiko chini ya mti huo na kuleta baraka na kuzuia mambo mabaya yasiikumbe jamii,” anasema.

Anasema kuwa tambiko lazima lifanywe ili ukatwe vipande vipande na kuondolewa kwa matumizi ya jamii.

Hata hivyo, Pasta James Akazile anasema kuwa nguvu ya mti huo umepitwa na wakati na watu hawafai kuwa mateka wa ushirikina ambao hauna maana wakati huu.

“Awali wakazi waliamini kuwa mti huo kama Mungu wao. Kuna wakati watu walitaka kuung’oa. Tuliambia wale ambao walikuwa wakijenga barabara ya Kitale –Lodwar kutouharibu na wakauacha,” anasema.

Anashauri watu kutoabudu miti, akisema waweke Imani yao kwa Mwenyezi Mungu

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

MAKALA MAALUM – Prof Oniang’o: Wanaume Gen Z...

Kang’ata aiga Gachagua akiahidi kutuza wakulima wa maembe...

T L