• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Mtoto aliyebakwa na kunyongwa huenda asipate haki baada ya mshukiwa mkuu kutoweka

Mtoto aliyebakwa na kunyongwa huenda asipate haki baada ya mshukiwa mkuu kutoweka

NA MWANGI MUIRURI

HAKI ya malaika Purity Njeri aliyeuawa kinyama Julai 18, 2020 akiwa na miaka saba pekee imekwama baada ya mshukiwa wa umri wa miaka 14 aliyekamatwa kudaiwa kutoroka kutoka jela la watoto la Murang’a.

Mtoto Njeri alipatikana ameuawa kwa kugongwa kwa kifaa butu kichwani na kisha mwili wake kupakiwa kwa gunia na kuzikwa katika Kaburi ndogo karibu na nyumbani kwao.

Unyama huo ulitekelezwa katika kijiji cha Ihiga-ini kilichoko katika wadi ya Nginda ndani ya eneo bunge la Maragua na uchunguzi uliozinduliwa ulimnasa Patrick Kombo wa miaka 14 kama mshukiwa mkuu.

Katika kituo cha polisi cha Maragua, Kombo alidai kwamba marehemu aliangukiwa na parachichi kwa kichwa na akaaga dunia.

Hata hivyo, ripoti ya upasuaji iliyofanyika katika mochari ya Murang’a na Dkt Abraham Njoroge ilibaini kwamba marehemu aliuawa kwa kugongwa kichwani kwa kifaa butu na pia akanyongwa baada ya kubakwa.

Polisi walimshtaki kijana huyo wakilenga kuthibitisha kwamba alitekeleza mauaji hayo na kisha akazika mwili kama njia ya kuficha ushahidi.

Polisi walisema katika taarifa yao kwamba baada ya kutishiwa kipigo cha kitutu na raia, alikiri kutekeleza unyama huo na ndipo raia wenyewe wakamtia mbaroni na kumwasilisha hadi kituo cha polisi.

Sasa, kesi dhidi ya mshukiwa imekwama katika mahakama kuu ya Murang’a.

Bw John Chege ambaye ni babake marehemu aliambia Taifa Leo kwamba kesi hiyo iliyorekodiwa kama ya mauaji chini ya nambari 18/2020 imekwama huku makachero wakimfahamisha kuhusu kutoweka kwa mshukiwa.

“Waliniambia kwamba mshukiwa alihepa kutoka jela la Murang’a linalozuilia watoto. Mimi nimebakia kusononeka si haba na hata nikaanza kunywa pombe kiholela ndio nisahau msiba wangu,” akasema.

Mshukiwa alikuwa amekanusha mashtaka hayo na wakati siku ya kutajwa kwa kesi hiyo mnamo Novemba 5, 2020 mbele ya Jaji Kanyi Kimondo, upande wa mashtaka ulikosa kumwasilisha mshukiwa kortini.

Jaji Kimondo alitoa makataa ya siku 14 mshukiwa awasilishwe mahakamani lakini haikutimia.

Iliibuka kwamba mshukiwa hata hakukaa katika rumande ya jela hilo la watoto kwa wiki moja kabla ya kutoweka.

Kwa sasa, mahakama imetoa ilani ya kukamatwa kwa mshukiwa huyo lakini hajapatikana.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa makachero ambao ripoti yake Taifa Leo imeona, mshukiwa huyo ambaye kwa sasa amefikisha miaka 18 amekuwa mgumu kumnasa kwa kuwa hakuna rekodi zake za usajili.

“Hakuwa na kitambulisho cha kitaifa, hakuwa na nambari ya simu au rekodi zozote isipokuwa za kuzaliwa ambazo zinaweza zikatumika kumnasa kijasusi,” ripoti ya Desemba 21, 2023 yasema.

Ripoti hiyo inasema kwamba “kuna fununu kwamba mshukiwa huyo yuko mafichoni katika Kaunti ya Lamu au ya Nyandarua”.

Hata hivyo, babake marehemu anasema kwamba “kuna uwezekano mkubwa ufisadi mkuu ulitumika kumtorosha mshukiwa huyo”.

Amehoji jinsi kijana ambaye alitoroka jela angepata mbinu na rasilimali ya kukwepa serikali yote ya Kenya kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Sasa msiongee na fisi, KWS inakuja kuwaondoa, wakazi wa...

Mechi isiyotabirika ‘Sauzi’ na Cape Verde zikikabana...

T L