Makala

Mtunzaji viumbe asimulia jinsi anavyopenda kuwalisha kaa

June 9th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

KWA Athman Aswa, viumbe mbalimbali wa baharini wamekuwa kiburidisho chake kikubwa cha nafsi tangu alipokuwa mdogo kabisa hadi sasa ambapo ametinga umri wa miaka 45.

Bw Aswa, mzawa wa mji wa Mokowe, Lamu Magharibi, anasema mapenzi yake kwa viumbe hao wa baharini yamekuwa yakimsukuma kuamka kila asubuhi kukimbilia ufuoni kuwatazama ama wawe ni samaki wakirukaruka baharini au kaa wanaokimbia hapa na pale, iwe ni ufuoni au wakiwa wamejitokeza majini na kukwea juu ya ukuta maalum wa kukinga maji ya bahari yasifikie makazi ya binadamu almaarufu seawall.

Mara nyingi Bw Aswa amekuwa akijipata akishikilia vijidudu au minyoo ya ardhini, ambapo katika harakati zake za kutazama viumbe baharini, yeye amekuwa akiwarushia wadudu na kukaa akitazama kama watafuata na kula.

Hapo ndipo alipogundua siri kwamba baadhi ya viumbe fulani wa baharini hula aina fulani ya vyakula.

Kwa sasa Bw Aswa ni mwanachama na Naibu Mwenyekiti wa Kundi la kijamii la Mokowe Mainland Community Based Organisation.

Kundi hilo linajihusisha sana na masuala yanayofungamana na uhifadhi wa viumbe wa baharini na mazingira kwa ujumla.

Ndilo kundi la kwanza kabisa kuvuma kote katika Kaunti ya Lamu kwa kuanzisha mradi wa ufugaji wa kaa wa kuliwa.

Kaa ni mnyama mdogo wa majini mwenye miguu sita au zaidi na gamba mwilini.

Ni kutokana na mapenzi yake kwa viumbe na tajriba aliyonayo Bw Aswa ya tangu udogoni mwake katika kuwatunza viumbe wa baharini ambapo kundi hilo la Mokowe Mainland Community Based Organisation lilimteua kuwa afisa mshirikishi wa masuala ya kuwalisha kaa.

Kutokana na ujuzi wake, kundi hilo la kijamii limepiga hatua kubwa katika ufugaji wa kaa Lamu.

Ni kufuatia ufanisi huo ambapo viongozi mbalimbali, akiwemo Gavana wa Lamu Issa Timamy, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Lamu Muthoni Marubu, wabunge na hata mawaziri wa serikali ya kitaifa, waliamua kuzuru eneo hilo la ufugaji wa kaa kujionea maendeleo hayo.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili kwenye eneo la ufugaji kaa la Mokowe, Bw Aswa alieleza jinsi jukumu la kuwalisha kaa linavyohitaji mtu kujitolea kikamilifu.

Anasema kuwalisha kaa si kazi rahisi kwani lazima anayetekeleza jukumu hilo kufahamu tabia za viumbe hao.

“Wakati ukifuga kaa kwa azma ya kuwanenepesha, lazima uwe mjuzi wa ni nini viumbe hao wanataka kula, kwa wakati gani na kiasi gani kinachofaa. Hapa mimi ninajua hawa kaa wetu wanapenda kitu gani. Pia nimejua nyakati za kuwalisha na zile za kuwaacha walale,” anaeleza Bw Aswa.

Miongoni mwa vyakula ambavyo mtunzaji wa viumbe huyo anasema kaa hupendelea sana kutumia, ni madondo.

Madondo ni aina ya kaa wa baharini asiyeliwa.

Mbali na madondo, kaa pia hula samaki wadogowadogo, vipande vya nyama, minyoo ya ardhini, konokono na mboga kama vile kabichi iliyokatwa vipande vidogovidogo.

Bw Aswa anasema wakati mwafaka wa kuwalisha kaa ni pale maji ya baharini yanaporudi au kufuma kwani huo ndio wakati ambapo kaa huamka kutoka usingizini.

Bw Athman Aswa,45, ambaye ni mtunzaji viumbe anayependa sana kuwalisha kaa wa kuliwa baharini. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anasema yeye huwalisha kaa zaidi ya 20 kwenye eneo hilo lao la kijamii la Mokowe.

“Nilipopewa jukumu la kuwalisha kaa kwenye kundi letu, hapo kwanza nilianza kwa kuchunguza tabia za viumbe hao. Nilifahamu fika kwamba wao huamka wakitaka kula wakati maji yanapoongezeka au kufuma. Maji ya baharini yanayotoka na kwenda, hapo ndipo kaa hupata fursa kulala, hivyo huwezi kuwalisha,” akasema Bw Aswa.

Anasema yeye huwalisha kaa wao mara mbili kwa siku.

“Maji yenyewe ya bahari huingia na kutoka mara mbili kwa siku. Kwa hivyo wakati yameingia, mimi hufika eneo letu la kutunza na kunenepesha kaa nikiwa nimejihami kwa vyakula vya kuwapa. Majira ya kuwalisha kaa hubadilika kulingana na maji. Mara nyingine hata maji hurudi usiku kabisa. Hilo linamaanisha tunabeba tochi na kwenda eneo letu la kunenepesha kaa kuwalisha,” akasema Bw Aswa.

Mtunzaji huyo wa mazingira anasema lazima mja awe makini katika kuwalisha na kuwanenepesha kaa katika kiwango kinachostahili.

Anasema katika kuwalisha, lazima mtunzaji azingatie uzito wa chakula.

“Je, kaa unayemlisha yuko na uzito gani na unalenga afikie uzani upi? Ukijihami kwa ufahamu huo ndipo utaweza kujua Dhahiri ni kaa yupi utampa gramu ngapi za chakula na ni yupi anahitaji uzani upi wa chakula hicho hicho,” anaeleza Bw Aswa.

Anasema chakula kama vile madondo huhitaji muda wa kukitayarisha.

Anasema madondo huishi ndani ya vijungu (shell) ambavyo ni vigumu kuvunja.

“Kwanza natafuta vijungu hivyo na kuvikusanya. Huanza kuvivunja iwe ni kwa kutumia mawe kwa mawe au mawe kwa chuma. Nikivunja vijungu hivyo ndipo ninapata hayo madondo. Kisha ninapima gramu zangu, hasa kuanzia 75 kwendelea na kuwalisha kaa wetu. Wananenepa vizuri,” akasema Bw Aswa.

Bw Salim Bwana Mzee, mmojawapo wa wanachama wa kundi la kijamii la Mokowe Mainland Community Based Organisation, anamsifu Bw Aswa kwa jinsi alivyo na moyo wa kupenda kushughulikia viumbe wa baharini na kuwatunza.

Bw Athman Aswa (kulia) akiwa na Salim Bwana Mzee waonyesha kaa wanaowalisha na kuwanenepesha eneo la Mokowe, Lamu. Bw Aswa anasema kuwafuga na kuwanenepesha kaa si kazi rahisi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Mzee anasema ni kupitia juhudi za Bw Aswa ambapo kundi hilo limefaulu kukuza, kunenepesha na kuuza kaa kila mara, hivyo kujipatia mtaji.

“Namshukuru sana Bw Aswa. Nimekuwa nikiandamana naye na kutazama jinsi anavyowalisha kaa. Ameniwezesha hata mimi kujipatia ujuzi wa kutunza viumbe. Siku anapokosekana mimi ndiye ambaye huwa ninatekeleza jukumu la kuwalisha kaa wetu,” akasema Bw Mzee.

Watunzaji hao wa viumbe aidha wanawashauri wakazi kudumisha mapenzi kwa viumbe, hasa wale wa baharini kama vile kaa.

“Unapokuwa na mapenzi ya dhati kwa viumbe utakuwa na bidii ya kuwatunza na kuepuka kuwadhuru. Tukifanya hivyo mazingira yetu yatakuwa bora na ya kupendeza kuishi,” akasema Bw Mzee.