• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 5:59 PM
Mui huwa mwema: Waraibu wa zamani wapigana na pombe ‘ile mbaya’

Mui huwa mwema: Waraibu wa zamani wapigana na pombe ‘ile mbaya’

TITUS OMINDE Na GABRIEL KUDAKA

KUNDI linalowaleta pamoja waliokuwa watengenezaji wa pombe na wanywaji walioasi ulevi katika eneo la Burnt Forest, Kaunti ya Uasin Gishu, limezindua mpango unaolenga kukabiliana na uuzaji na vileo katika eneo hilo kwa kuhubiria walevi ili waokoke na kuachana na pombe.

Mnamo Jumamosi iliyopita, Taifa Leo ilifuatilia shughuli za kundi hilo ambapo wanachama wake chini ya mwavuli wa ‘Okoa Mlevi’ walisema nia yao ni kuokoa jamii.

Bi Regina Samoei, ambaye ni mwanachama wa kundi hilo, alisema zamani alikuwa mtengenezaji chang’aa lakini sasa anashirikiana na wenzake kueneza ‘injili’ ya kuwahimiza walevi kuachana na pombe.

Lakini wenzake humtembelea kujua namna anavyokabiliana na maisha baada ya kuachana na pombe haramu.

Tangu alipoacha kutengeneza pombe miezi michache iliyopita, anasema mambo yanalainika.

“Mmerudi tena?” akauliza Bi Regina huku akiwakaribisha nyumbani kwake.

Bi Regina, ambaye alikuwa akiuza pombe kwa zaidi ya miaka mitatu, anasema alijitosa katika biashara hiyo haramu ili kutunza familia yake.

“Nina mtoto ambaye anaishi na ulemavu. Pia nina watoto wengine wawili katika Shule ya Sekondari, mmoja katika Kidato cha Pili na mwingine Kidato cha Nne. Nimekuwa nikitegemea uuzaji wa pombe ili kuwasaidia,” akasema Bi Regina.

Sasa ametii wito wa serikali wa kuacha kuuza pombe lakini angependa kupata usaidizi wa kifedha ili kujitosa katika biashara mbadala ya kujikimu kimaisha.

Yeye ni mwanachama wa Berean Self Help Group, kundi linalojumuisha akina mama wajane ambao wengi wao walikuwa watengenezaji pombe haramu.

Ni kikundi ambacho kilisajiliwa mwaka 2023 na kinatafuta uungwaji mkono ili kuwatia moyo wanachama wengi zaidi kujitosa katika vyanzo mbadala vya kujikimu kimaisha badala ya pombe haramu.

Chini ya kilomita moja kutoka nyumbani kwa Bi Regina, nyimbo zinatanda hewani na kuvuruga mazungumzo kati ya Bi Regina na wageni wake.

Muziki huo una mada za kukemea uuzaji na unywaji wa pombe haramu.

“Hao ni baadhi ya wanachama wetu wamekusanyika hapo baada ya kuzunguka eneo hili ili kuendelea kuhamasisha jamii,” akasema Bi Nelly Machii, Mwenyekiti wa Operesheni Okoa Mlevi.

Baadhi ya wanachama hao walisimulia uchungu wa ajabu waliokumbana nao walipokuwa kwenye minyororo ya ulevi.

“Nilikuwa mraibu wa ulevi kwa zaidi ya miaka 15. Hivyo nilipoacha na kuokoka, nilisema lazima nitafute watu wengine ambao bado wanapambana na changamoto ya ulevi,” mwenyekiyti huyo akaongeza.

Kwa sasa ni mchungaji wa kanisa mojawapo la Kiadventista mjini Eldoret.

Mraibu mwingine aliyerekebisha tabia alisimulia kwa uchungu jinsi pombe ilivyotikisa ndoa yake, miezi michache baada ya arusi.

“Tulifanya arusi ya kufana sana. Lakini pombe haiheshimu ndoa. Mke wangu aliniacha,” akakiri mraibu aliyerekebisha tabia.

Naye Evans Kimutai, kasisi wa Kanisa la SDA eneo la Kapkioi alichukua fursa hiyo kuhubiri injili ya wokovu na kuacha ulevi.

Baadhi ya waumini wapya walisherehekea maendeleo yao hata kutoa ushuhuda kuelezea namna walivyokabiliana na safari yao ya kuacha kinywaji hicho.

“Si rahisi. Nilikuwa nikinywa chupa sita za pombe kwa siku, lakini sasa nimepunguza hadi tatu. Nimedhamiria kuacha,” alisema mmoja wao ambaye bado anaendelea kupata nafuu.

Uasin Gishu ni mojawapo ya kaunti ambazo zimekuwa zikikabiliana na changamoto ya ulevi.

Maafisa wa kutekeleza sheria wamekuwa wakiendesha shughuli za kukabiliana na pombe haramu. Baadhi ya maafisa wa polisi walishambuliwa katika eneo la Ziwa walipokuwa wakiendesha msako dhidi ya pombe haramu.

Serikali iliimarisha vita kote nchini dhidi ya dawa za kulevya na ulevi kufuatia vifo vya watu 17 mwezi Februari katika Kaunti ya Kirinyaga baada ya kunywa pombe haramu.

  • Tags

You can share this post!

Maafisa wakuu wa serikali kuzimwa kutumia Tiktok –...

KRA yaagiza ushuru wa nyumba kutekelezwa kuanzia Machi 19

T L