Mume jasiri araruliwa na simba akiokoa mkewe
MUME na mke waliopambana vikali na simba hadi wakamlemea kabla ya wao kukimbizwa hospitalini kwa matibabu, wamesimulia jinsi nusra wapoteze maisha yao mikononi mwa mnyama huyo hatari.
Alimwona simba huyo akimfuata mkewe aliyekuwa akitafuta kuni katika eneo la Maili Nane, viungani mwa mji wa Isiolo.
Bw Michael Apayo aliamua kumkabili simba huyo akifahamu fika kwamba angemuua.
Alikuwa tayari kukabiliana kumwokoa mama wa wanawe wawili, mdogo zaidi akiwa na umri wa miezi sita.
“Nilimwona mnyama huyo akimwandama mke wangu ambaye kwa hofu alianza kutoroka.
“Nisingekubali kutazama akiuawa kwa hivyo niliamua kumkabili Simba huyo,” alisema akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Isiolo ambako yeye na mkewe wamelazwa.
Bw Apayo alifaulu kumwangusha simba huyo ardhini huku juhudi zake za kumlemaza kabisa zikiambulia patupu.
“Simba huyo alinilemea, akanibana mwili wangu na kunikwaruza mgongoni,” akaeleza.
Mke wake, Susan Chebet, alitazama vita hivyo kwa umbali, akiomba kuwa mumewe atanusurika kifo.
Apayo alipambana na simba huyo kwa dakika 20.
Wakati akikaribia kukata tamaa, Bw Apiayu aliyekuwa mnyonge alimwomba mkewe kumpa panga ambayo alikuwa akitumia kukata kuni.
“Alifika haraka na kumkata mnyama huyo machoni mara mbili hadi akamdhoofisha. Hata hivyo, tuliathirika,” akakumbuka.
Akigaagaa kwa uchungu baada ya kukatwa jicho, kwa mara ya pili, simba huyo alianguka ardhini huku wanandoa hao wakitorokea usalama wao.
Bi Chebet, aliyepata majeraha ya kifua na miguu, alibubujikwa na machozi tulipomtembelea hospitalini.
“Nina furaha na huzuni kwa wakati mmoja. Ninashukuru Mungu tuliponea kifo lakini nina wasiwasi kuhusu hali ya watoto wetu. Nani atawatunza na sote tumelazwa hospitalini tukitibiwa?” akauliza.
Haijulikani kama simba huyo, ambaye alikuwa na kifaa cha kutambua aliko (tracker), aliko ila inashukiwa hayawani huyo aliyetoroka katika hifadhi ya Lewa, ama alikufa au alirejea kwenye hifadhi hiyo akiwa na majeraha.
Bw Apayo na Bi Chebet nao walisema hivi kumhusu: “Tulimwacha akiwa anagaagaa ardhini.”
Idadi ya simba nchini imekuwa ikipungua huku serikali ikiwaorodhesha kama viumbe walio hatarini kuangamia. Inakadiriwa kuwa kuna jumla ya simba 2,500 pekee nchini.
Bi Hellen Nakutun, ambaye ni jamaa waathiriwa hao alitoa wito kwa Shirika la Huduma ya Wanyamapori (KWS) kuwafidia wawili hao.
Alililaumu KWS kwa utepetevu kwa kutoweka ua wa umeme katika mbuga na hifadhi za wanyamapori, hali inayochangia wanyama hao kushambulia binadamu.
“KWS inafaa kuzuia wanyama kuponyoka kutoka kwa mbuga za wanyamapori ili wasiwashulie binadamu.
Inasikitisha kuwa maafisa wa shirika hili huwaruhusu wanyamapori kurandaranda vijijini,” Bw Nakutun akasema.
Aliwaomba viongozi wa eneo hilo na wasamaria wema kujitokeza na kusaidia familia hiyo.
Ua katika mbuga nyingi za wanyamapori una mianya mingi, hali inayochangia wanyama kupenya na kuondoka.