Jamvi La SiasaMakala

Mungu ni Mungu hata asipotuokoa kutoka motoni, familia ya Gachagua yasema

Na WINNIE ONYANDO November 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

FAMILIA ya Rigathi Gachagua, naibu Rais aliyebanduliwa, imesema kuwa haitashtuliwa na changamoto zinazoiandama.

Bw Gachagua kupitia chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X (Twitter) na Facebook alisema kuwa anafurahia kurejea nyumbani alikozaliwa.

“Namshukuru Mungu kwa kunipa familia inayonijali. Nitaendelea kutoa shukrani zangu kwa Mwenyezi Mungu kwa kunipa familia kama hii. Mungu Bariki Kenya,” aliandika Bw Gachagua.

Vile vile Mhubiri Dorcas Gachagua kupitia chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, alisema kuwa familia hiyo itaendelea kutoa sala za shukurani katika kila jambo.

Akinukuu kitabu kitakatifu cha Danieli 3:16-18, pasta Dorcas alisema kuwa haijalishi wanapitia changamoto gani kwani hata kwenye moto mkali, Mungu atabakia kuwa Mungu.

“Ni rahisi kuangazia changamoto na mazingira yanayokuzunguka na kusahau kanuni za wokovu. Leo, mimi na familia yangu tumeamua kutoa sala ya shukrani, tukielewa kwamba, Mungu anabaki kuwa mwenye enzi, iwe anatuokoa kutoka katika moto au la, Danieli 3:16-18,’

“Tunamshukuru Mungu kwa uaminifu wake wa ajabu. Tunamwita, Ebeneza, kwa umbali huu tunamsherehekea. Tumeona rehema zake na wema wake. Utukufu na heshima zimrudie,” Pasta Dorcas aliandika katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram.

Kando na hayo, kama Ayubu, Pasta Dorcas amesema kuwa wataendelea kumtumainia Mungu.

Ujumbe huo uliambatanishwa na picha ya Bi Dorcas, Bw Gachagua na wanao wawili, Keith Ikinu na Kelvin Gachagua, wakiwa wamekaa kiwanjani kwenye nyasi nyumbani kwao.

Ujumbe huo ulijiri muda mchache tu baada ya Profesa Kithure Kindiki kuapishwa kuwa naibu rais.

Gachagua alipata pigo kortini

Japo Bw Gachagua amejaribu sana kuzuia kuapishwa kwa Profesa Kindiki kupitia rufaa kortini, hatimaye Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi, Alhamisi ilitupilia mbali kesi iliyozuia kuapishwa kwa profesa huyo.

Kuondolewa kwa agizo la kusitisha kuapishwa kwa Profesa Kindiki ni pigo kwa Bw Gachagua ambaye amekuwa akitegemea mahakama kumnusuru.

Awali, Mahakama ya Rufaa ilidinda kuzuia Mahakama Kuu kutoa uamuzi kuhusu agizo la kuzimwa kwa hafla ya kumwapisha Naibu Rais mpya.

Akikula kiapo Ijumaa Novemba 01, 2024, Profesa Kindiki aliahidi kuwa mwaminifu kwa Rais William Ruto akitekeleza majukumu yake.

Katika hotuba yake baada ya kuapishwa, Profesa Kindiki alisema amekuwa mwanafunzi mwema wa Rais Ruto na kwamba hatamwangusha katika majukumu mapya aliyompa ya kuwa msaidizi wake rasmi.

“Nimekuwa mwanafunzi wako mwema kwa miaka 20. Nimejifunza kuwa mnyenyekevu na mwaminifu, sitakuangusha katika majukumu mapya uliyonitwika,” akasema.

Prof Kindiki, aliapishwa Ijumaa katika hafla ya kufana iliyofanyika  nje ya Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC) iliyoshuhudiwa na Rais William Ruto, Jaji Mkuu Martha Koome, maafisa wengine wa serikali na wageni mashuhuri.