Murang’a yapata bustani wazi kuepuka drama za ufuska
NA MWANGI MUIRURI
KAUNTI ya Murang’a imejipa bustani yake ya kwanza ya umma ambayo ina ukubwa wa takriban futi 40 kwa 100 na viti vinne pekee.
Bustani hiyo ya wazi inazuia tabia chwara za wapenda ufuska, lakini la muhimu zaidi ni kwamba pembeni, wazee wametengewa sehemu ya kuchezea drafti.
Bustani hiyo ambayo iko karibu na steji kuu ya Mukurwe-ini ilitembelewa na ujumbe wa taifa la Eswatini kama kielelezo bora cha maendeleo, Gavana Irungu Kang’ata akisema ni mradi mmoja wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Mnamo Mei 16, 2024, Gavana Kang’ata akiandamana na Mwakilishi wa Wadi ya Township Bw Machigo Karina, aliwaongoza wageni hao wa kutoka Eswatini ambao walifika wakiwa wamevalia nguo kama shuka za jamii ya Maasai hapa nchini.
Kiongozi wa ujumbe huo wa Eswatini Bw Apolo Mapalala alisema alifurahishwa sana na bustani hiyo na kwamba akirejea kwao atazindua midahalo ya kuiga maendeleo sawa na hayo.
Lakini kile kimezua gumzo mjini Murang’a ni kuhusu udogo wa bustani yenyewe ambayo iko katika kipimo cha ploti moja ya ujenzi, ikizingatiwa kwamba mji wa Murang’a hutaniwa kama mwenyeji wa mzunguko mdogo zaidi nchini.
“Sio mradi mbaya lakini upana wake ni mchache sana. Kumefinyana. Hapa hakuna usiri unaofaa kuwa na bustani ya umma ambapo hata wapendanao wanafaa kuja hapa kuchumbiana na kupokezana maua kukoleza penzi,” akasema Bw Martin Mwaniki, ambaye ni mwenyeji.
Bw Mwaniki alisema kwamba kuna bustani sifika nchini ambapo hata huwa tunasikia harusi zikiandaliwa ndani yazo.
“Hii yetu ni ndogo mno,” akasema.
Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu alisema kwamba bustani za umma huwa na maana yake ya kuwapa watu mahali pa kupumzika “na pia huorodheshwa miongoni mwa miradi ya kurejesha mazingira ya kijani kutufaa katika suala la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi”.
“Wakati wa gavana wa kwanza Bw Mwangi wa Iria, hakukuwekwa mikakati ya kujenga bustani ya umma hivyo basi kuwafanya wengi katika miji ya eneo hili kuhangaika wakisaka pa kustarehe bila malipo,” akadai seneta Nyutu.
Bw Nyutu alisema ukosefu wa viwanja muafaka vya kuwekeza rasilimali katika utengenezaji wa bustani ni kikwazo kikuu.
“Kuna mapendekezo kadha ambayo yalikuwa yamewekwa na utawala wa Bw wa Iria ikiwa ni pamoja na kuzinduliwa kwa mbuga ya wanyamapori katika viunga vya mji wa Murang’a na pia kuzindua bustani ya umma ndani ya uwanja wa Ihura,” akasema.
Bi Susan Kamau, ambaye ni mchuuzi katika mji wa Murang’a, alisema kwamba bustani hiyo licha ya udogo wake, itawasaidia wachuuzi kupata mahali pa kupumzikia na pia kuuzia wale watakaofika kuitumia.
“Hili ni soko letu kwa kuwa mkusanyiko wa watu huja na uteja. Lakini serikali ichunge kwa kuwa wakazi wengi wa Murang’a wakiona mahali ambapo kuna nyasi huwa wanapageuza kuwa eneo la kujiachilia haja ndogo na kubwa,” akasema Bi Kamau.
Alisema kwamba wenyeji huchafua mazingira kwa kutabawali na kuenda haja kubwa ovyoovyo katika vichochoro vya mji huo “na hata hapa ambapo serikali imepanda nyasi na kuweka seng’eng’e, huenda tupate pamegeuzwa kuwa choo haramu cha umma”.
Katika bustani za aina hiyo katika kaunti nyingine , kumeripotiwa visa vya watu kuzigeuza maeneo ya starehe za wapenzi, baadhi wakizigeuza madanguro.