Makala

Murkomen: Mkenya alichokoza Ethiopia ikasababisha Turkana kuvamiwa

Na LABAAN SHABAAN February 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Usalama Kipchumba Murkomen amesema mhalifu mmoja aliyevuka mpaka kutoka Kenya hadi Ethiopia ndiye alisababisha mashambulio ya kushtukiza ya wanamgambo wa Daasanach Kaunti ya Turkana Jumapili iliyopita.

Zaidi ya wavuvi 20 wa Kenya walivamiwa na kufikia sasa hawajulikani walipo.

“Jumamosi iliyopita kwa bahati mbaya kuna mkora mmoja alienda kuleta shida upande wa Ethiopia kutoka Kenya na habari ambazo tunazo ni kwamba aliwaua watu watatu wa Ethiopia,” akasema Bw Murkomen.

“Kupitia mashambulizi ya kulipiza kisasi, inasemekana Wakenya walivamiwa kutoka upande wa Ethiopia wakiwa eneo la Ziwa Turkana. Hatujajua katika uvamizi huo ni Wakenya wangapi waliumia lakini kutokana na idadi ambayo familia inasema haijawaona, ni zaidi ya watu 20,” akaongeza.

Alikuwa akiongea jana wakati wa ziara ya kikazi katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Kiambu Road.

Mnamo Jumatano Waziri Murkomen alikuwa katika eneo la uhalifu, Lopeimukat na Natira huko Todonyang’ katika harakati ya uopoaji na uokoji wa walioathiriwa na mashambulizi kutoka kwa wapiganaji wa Daasanach.

Kulingana na Bw Murkomen, mchakato wa kidiplomasia kati ya Kenya na Ethipoia unaendelea tangu Jumanne ili kusaidia katika msako unaotazamiwa utazima hali ya taharuki inayoshuhudiwa.

Bw Murkomen alionyesha wasiwasi kuwa mamlaka za Ethiopia hazijajitolea kwa kiwango ambacho kinatarajiwa kimawasiliano, ili kukomesha mzozo na kusaidia katika upatikanaji wa mili ama watu waliopotea.

“Huku upande wa Ethiopia ukitepetea katika mawasiliano kiasi cha kufanya uokoaji kuwa mgumu, ninawapa heko maafisa kutoka nchi hizi mbili kwa kujitolea kwenye oparesheni ya uokoaji,” akasema Bw Murkomen katika taarifa aliyotoa Jumatano.

Kufikia sasa miili miwili imepatikana na kukabidhiwa kwa familia baada ya upasuaji kufanywa kupisha hafla ya mazishi.

Murkomen aliongeza kuwa juhudi za kukutanisha walioshambuliwa na familia zao zinapitia changamoto zikiwemo hali ya kijiografia ya mazingira ya Ziwa Turkana ambalo limeenea hadi upande wa Ethiopia.

“Serikali imeandaa rasilimali hitajika ikiwemo njia ya kidiplomasia kuangazia mgogoro ili kuhakikisha waliopotea wanarejea wakiwa salama,” akaeleza.

Wakati huo huo Waziri Murkomen alikashifu mzozo katika ya Kampuni ya Umeme (KPLC) na Serikali ya Kaunti ya Nairobi akiita hatua ya kaunti kumwaga uchafu katika afisi za kampuni hiyo kama tabia chwara.

“Pengine hatukutangaza hatua tuliyochukua kama ilivyohitajika. Lakini KPLC iliwasilisha ripoti ambayo ilisaidia kuwezesha maafisa wa kaunti kukamatwa. Isitoshe, malori kadhaa yamechukuliwa na kufungiwa katika kituo cha polisi,” akasema bila kutoa ithibati.

Bw Murkomen alidokeza kuwa kuchelewa kwao kuwasilisha taarifa kwa Bunge kulisababisha walaumiwe kwa utepetevu katika utendakazi wao.