Makala

MUTANU: Serikali idhibiti bei ili kupunguzia Mkenya mzigo wa maisha

August 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na BERNARDINE MUTANU

TANGU mwaka wa 2017, hali ya uchumi nchini imekuwa mbaya kiasi kwamba gharama ya maisha imepanda sana.

Huku bei ya mafuta ikitarajiwa kupanda zaidi, itakuwa vigumu kumudu gharama ya maisha nchini.

Wakati huo, ikiwa Kenya itatia sahihi mkataba wa mkopo kutoka kwa Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) wananchi wanafaa kutarajia kupanda juu zaidi kwa ushuru.

Ni matumaini ya kila Mkenya kwamba gharama ya maisha itapungua. Lakini ilivyo ni kwamba huenda hali ya uchumi ikawa mbaya kutokana na ongezeko la bei ya mafuta na ongezeko la mikopo.

Kwa miezi kadhaa, bei ya mafuta imekuwa ikiongezeka kila mwezi na kiwango cha kupungua kwa bei ya dizeli na mafuta taa ni cha chini kiasi kwamba hakuna tofauti na mwezi jana.

Kutokana na ongezeko hilo, gharama ya kutengeneza bidhaa itazidi kuongezeka, hivyo kuathiri zaidi gharama ya maisha.

Inaamaanisha pia kuwa huenda kampuni nyingi zinazotumia mafuta ya dizeli kutengeneza bidhaa yakaathirika, hali inayoweza kupelekea kupunguzwa kwa operesheni, hivyo kupunguzwa kwa wafanyakazi.

Tayari, kampuni nyingi zimewapunguza wafanyakazi wake na zingine zimefunga au kuhamisha operesheni zao nchini.

Pia, wamiliki wa matatu wametangaza kuwa wataongeza nauli. Hatua ya serikali kuongeza ushuru pia kwa baadhi ya huduma kama vile umeme pia imeathiri wananchi.

Pendekezo la wafanyakazi kutozwa ushuru wa nyumba huenda likawa mwimba kwa wafanyakazi wengi ambao tayari maisha ni magumu.

Ilivyo ni kuwa, kutakuwa na idadi kubwa ya wananchi ambao hawatakuwa na kazi au na nyenzo za kujipa pato. Kutokana na hilo, vijana wengi wataingia mitaani ‘kujitafutia’ na hivyo ongezeko la uhalifu nchini.

Ninachosema ni kwamba, ni vyema serikali kuchukua hatua madhubuti kudhibiti kuyeyuka kwa uchumi kwa sababu ikiwa hilo litafanyika, basi athari zitakuwa mbaya zaidi.

Huku kampeni ikizidi kuhusu matumizi ya kawi mbadala, ni wakati pia wa wananchi kufunzwa jinsi ya kujitegemea, kuliko kutegemea ajira.

Ingawa ni jukumu la kila mwananchi kuchangia katika kujenga uchumi, inafaa serikali kuzingatia maslahi ya kila mmoja hasa wananchi walio na mapato ya chini.

Uchumi utakua ikiwa wananchi wote wataimarika kimapato na ikiwa nafasi zaidi za ajira zimeundwa pamoja na kudhibitiwa kwa mfumko wa bei ya bidhaa.

Hatua hizo pia zikichukuliwa zinatarajiwa kupunguza viwango vya uhalifu nchini, hasa maeneo ya mijini.