Makala

MUTANU: Visa vya mauaji miongoni mwa vijana vichunguzwe kwa kina

May 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BERNARDINE MUTANU

Kumekuwa na visa vingi vya mauaji nchini. Ingawa baadhi yake ni uhalifu peupe, hatuwezi kufumba macho kwamba visa vingi ni vya kinyumbani au kimapenzi.

Jinsi mambo yalivyo, ni rahisi kusema kuwa suala la mauaji halishtui watu tena. Wanaotekeleza mauaji ya kimapenzi au kinyumbani wameonekana kuwa watu wasiojali.

Mauaji yamekuwa taarifa ya kila siku. Ni jambo la kushangaza ni kuwa wengi wanaouawa au kuuana ni vijana.

Huku mijadala ikizidi kuhusiana na kinachoendelea nchini, ni lazima kutilia maanani kwamba hakuna siku moja ambapo mtu huamka na kuamua kuua mtu mwingine.

Huwa kuna masuala ya kmsingi ambayo humfanya mtu kutekeleza kitendo kama hicho, bila kujali ikiwa kuna sheria au la. Kwa kufanya hivyo, mtu huwa ameamua kuwa hata kifungo cha maisha jela au hukumu ya kuuawa ni sawa.

Ili kutatua suala hili, lazima liangaliwe kutoka pande zote ili suluhisho la kudumu liweze kupatikana. Kwanza kabisa, lazima tuelewe ya kwamba kuna shinikizo nyingi katika maisha ambazo hufanya watu kuchukua baadhi ya hatua ambazo za kushtua.

Kwa mfano, mambo ilivyo ni kwamba hali yya uchumi ni ngumu sana nchini. Gharama ya maisha imepanda, watu wana msukumo wa kulisha familia zao, wapenzi kusomesha watoto na kutimiza majukumu katika jamii.

Ingawa hicho sio kiini cha kumfanya mtu kuua mwingine, ni kati ya sababu za kuchunguzwa au kutafitiwa ili kutatua suala la mauaji ya kiholela miongoni mwa raia.

Pia, suala la udanganyifu katika ndoa au usuhuba linaweza kuchangia katika visa vilivyoongezeka vya mauaji ya hasa miongoni mwa vijana. Ndoa zilizo na misukosuko husababisha mapigano ambayo yanaweza kuwa kiini cha mauaji.

Hata hivyo, jamii imegeuka, vijana wamekengeuka na wazazi nao wameshindwa na kutekeleza majukumu yao ya kulea.

Vijana wengi wamelelewa bila msingi wowote hasa kutokana na kuwa wazazi wamebanwa na kazi au hawajali kuhusiana na maslahi ya wana wao. Kulingana na utafiti, watoto huiga wanachowaona watu wazima wakifanya.

Ikiwa wazazi wanalewa pombe na kuzua rabsha nyumbani, watoto hukua wakijua kuwa hakuna ubaya wowote kushiriki ulevi na kupiga watu, hivyo hatukuwa vigumu kwa kijana kupiga na kuua mwenzake.

Ilivyo ni kwamba, watoto wengi hutunzwa na wasichana wa nyumba. Ukweli ni kwamba watoto hao hukua bila maadili zaidi ya kuwa ni vigumu sana kwa wazazi kujua kwa sababu huwa hawapo karibu nao kwa muda mrefu.

Sio kusema ya kwamba wasichana wa nyumba wanafaa kulaumiwa kwa utomvu wa nidhamu kwa baadhi ya vijana, ninachosema ni kwamba wazazi wanafaa kuwajibika na kuhakikisha watoto wao wamekua kwa msingi unaofaa.

Pia, baadhi ya wazazi huwa hawawapeleki watoto wao kanisani. Ukweli ni kwamba, dini husaidia sana kukabiliana na janga linaloshuhudiwa, zaidi ya kuwa wazazi wanafaa kuwapeleka watoto wao kwa ushauri wanapoona dalili za shinikizo.