MUTUA: Amos Wako amegusa vipi masilahi ya Wamarekani?
Na DOUGLAS MUTUA
SIKU moja nilijipata pabaya nilipowaambia watani wangu nchini Kenya Wakenya wana mazoea ya kujibeba kana kwamba nchi yetu ndiyo jimbo la 51 la Marekani.
Hilo lilitokea miaka kadhaa iliyopita wakati ambapo Marekani ilikuwa chini ya utawala wa Rais Barrack Obama, ambaye ana asili ya Kenya.
Kila Mkenya hangetaka kupokonywa fahari ya kunasibishwa na kiongozi wa taifa lenye nguvu zaidi duniani, ndiposa nusra pachimbike tukizienda na watani wangu.
Wakati huo ningewaelewa Wakenya wote waliowana kwa meno na kucha kuthibitisha kwamba palikuwepo na ukuruba kati ya Kenya na Marekani.
Lakini siwezi kamwe kuwaelewa wakishikilia mtizamo kama huo wakati huu ambapo Marekani inaongozwa na mtu anayejali tu kuhusu masilahi ya nchi yake pekee.
Kumbuka Rais Donald Trump amewahi kuyaita mataifa yetu ‘mashimo ya kinyesi’, tusi ambalo liliudhi wengi wakati huo ila leo Waafrika wenyewe hulitema wakisinywa na kwao.
Iwe ni wakati wa utawala wa Obama, Trump au rais mwinginewe atakayechukua usukani Marekani, ni sharti kila mtu duniani aelewe kwamba taifa hilo hujihusisha tu na mambo yanayogusa masilahi yake.
Ni kwa saababu hii ambapo ninawacheka Wakenya nusra mbavu ziniteguke wanaposhangilia kwamba Marekani imeanza kuwasaidia kupambana na ufisadi.
Kisa na maana? Mwanasheria mkuu wa zamani, Bw Amos Wako, ambaye pia ni seneta wa Busia, amepigwa marufuku kukanyaga Marekani. Kwa makosa gani? Ufisadi. Maelezo? Hayapo.
Hii ina maana kwamba hakuna anayejua undani wa kilichoisababisha Marekani kumwagiza Bw Wako, tena kwa mara ya pili katika muda wa miaka 10, ajikalie Kenya.
Wakenya wanaoota mchana wanasema kwamba Marekani imejitolea kwelikweli kutusaidia, eti taasisi zetu zimelala usingizi wa pono usiojua wakati wa kuamka.
Taasisi zilizojipata matatani na Wakenya kwa kile kinachotwa kuzembea kazini ni pamoja na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Tume ya Maadili ya Kupambana na Ufisadi (EACC).
Hata Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ililaumiwa kwa kuyafumbia macho maovu ya wakuu hivi kwamba serikali ya kigeni imetuonea huruma na kuja kutuokoa.
Hiyo ni ndoto ya mchana ambayo Wakenya wanaota na kujisadikisha kwamba mambo yatatengenea hivi karibuni kwa sababu Mmarekani amekuja juu.
Nimeiita ndoto ya mchana kwa sababu wanaoota wako macho; wanajipa matumaini yasiyokuwepo. Labda ni huko kutotamauka kunakowapa nguvu za kuishi.
Ndoto ziwepo zisiwepo, ukweli nao ni mkaidi mno, haupotei njia; na ukweli ni kwamba Marekani haina nia wala wajibu wa kupambana na ufisadi nchini Kenya.
Ukiona taifa hilo likiingilia suala fulani, chunguza utathibitisha kuwa linahusu masilahi yake ya kiuchumi au usalama wa kitaifa. Yanayolihusu taifa lolote la Afrika, potelea mbali!
Ikiwa Bw Wako kwa kweli aliingiza madole yake kwenye kapu la peremende za watu, ole wake kwa kuwa miongoni mwa watu hao ni Mmarekani na hapendi masihara.
Hebu angalia: walanguzi wa dawa za kulevya wa familia ya Akasha waliendesha shughuli zao kwa miaka mingi wakipokezana biashara hiyo haramu kutoka vizazi hadi vizazi.
Sote pamoja na serikali yetu tulijua maovu ya familia hiyo ya Mombasa, lakini hatukujasiria kufanya chochote ama kwa woga au tamaa ya kula haramu.
Lakini Ibrahim Akasha na Baktash Akasha walipojiona kaiva kikweli, wakajaribu kuuza dawa zao haramu Marekani, hawakuruhusiwa kufikisha hata gramu moja huko.
Walichotwa kama kupepesa jicho, wakasafirishwa hadi Marekani na sasa wanatumikia vifungo virefu huko. Kumbuka hawakuuza hata vumbi la dawa hizo Marekani, iliyowafunga ni nia tu.
Marafiki wa Bw Wako, maafisa wa serikali na wafanyabiashara nchini Kenya wanaopapatika wakihofia kuzuiwa kwenda Marekani kwa kutuibia watulie na kujiuliza wameikosea Marekani vipi.