• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
MUTUA: Funzo kuu katika jekejeke la kusubiri matokeo ya kura US

MUTUA: Funzo kuu katika jekejeke la kusubiri matokeo ya kura US

Na DOUGLAS MUTUA

UCHAGUZI wa urais uliofanyika Marekani hivi majuzi ulinikumbusha matukio ya kukatisha tamaa yaliyowahi kuwatokea mashabiki wa timu ya kandanda ya Arsenal.

Mashabiki hao, nikiwa mmoja wao, watakwambia mioyo inavyowadunda kila timu yao inapochuana na nyingine kali. Itakuwa fedheha, au shangwe? Tunajiuliza kila mara.

Lakini pia tutakwambia hatujui stahamala na nguvu za kuupiga moyo konde hata baada ya kushindwa hutoka wapi. Tumetiwa mitihani tangu hapo na hatutamauki.

Ajabu akidi ni kwamba japo tumevunjwa mioyo mara zisizohesabika, hatupitikiwi akilini na fikra za kuacha kuiunga mkono timu hiyo na kuhamia, tuseme, Manchester United.

Ni kwa mintaarafu hiyo ambapo kuna mzaha kwamba ukitaka kumchumbia mtu, basi hakikisha ni shabiki wa Arsenal.

Hatawahi kukuacha hata ukichemsha uhusiano kiasi gani kwa kuwa sisi hatufi moyo. Utakuwa umepata eti. Nimesema ni mzaha; mimi si mshauri-nasaha wa mahusiano.

Hisia zangu zilijaribiwa si haba wakati wa ujumlishaji kura kwa maana nilidhani mwaniaji wangu angeshinda kwa urahisi, nikidhani mpinzani wake alikuwa hafifu.

Kama mhamiaji wa asili ya Kenya ninayeishi Marekani, namuunga mkono aliyekuwa Makamu wa Rais Barrack Obama, Bw Joe Biden, na wala si Rais Donald Trump.

Ni kawaida kwa wahamiaji wengi tu wakifika Marekani kukiunga mkono chama cha Democrat alichowania kwacho Bw Biden. Wanakubalika zaidi huko.

Ni kwa sababu hiyo ambapo nilipofika Marekani tu, kazi ya kwanza niliyofanya ni kumfanyia kampeni Rais Mstaafu Obama.

Nilibisha milango ya watu na kuwahamasisha Wamarekani wajitokeze kumchagua tena ili awatumikie kwa kipindi cha pili.

Siku yenyewe ya uchaguzi ilipofika, nilirejea tena kwa watu kuwahimiza watoke twende vituoni vya kupigia kura.

Tuliwaweka waliohitaji usafiri kwenye magari na kuwapeleka vituoni almuradi tu mwana wa asili ya Kenya asalie Ikulu ya White House.

Kando na itikadi za chama, ni heshima ambayo Bw Obama aliiletea Ikulu na Marekani kwa jumla ambayo ilinisadikisha kumuunga mkono Biden.

Nilizingatia kwamba Bw Biden na Bw Obama walikuwa washirika wazuri wakati wa utawala wao ndiposa nikaamua anafaa kumwondoa Trump na chuki yake Ikulu.

Nilidhani ni kazi rahisi kumshinda Trump hadi usiku wa baada ya uchaguzi alipoonekana kuwa mshindani imara, akatishia kusalia Ikulu kwa miaka mingine minne.

Nilishtuka hadi ya kushtuka, nikajikuna kichwa na kujiuliza mkuu wa chuki na kiburi akishinda wanangu watakulia wapi!

Tangu Trump aingie madarakani, maisha ya wahamiaji na watoto wao yamekuwa magumu sana.

Ubaguzi wa rangi umeongezeka hivi kwamba shuleni watoto watundu wa kizungu wamekuwa wakiwatishia wale wa wahamiaji kwamba ‘mtarejeshwa kwenu na Trump’.

Watundu hao, na hata wazazi wao kwa kiasi kikubwa, wanamuiga kiongozi wao ambaye amewahi kuwacheka walemavu na kuyatukana mataifa ya Afrika kuwa ni ‘mashimo choo’.

Amewadhalilisha na kuwatukana wanawake matusi yasiyoandikika kwenye gazeti la familia kama hili.

Hayo na mengine mengi ameyafanya akitumika kipindi chake cha kwanza, seuze akipata cha pili? Swali hili lilidunda kichwani mwangu mtawalia nikisubiri matokeo.

Nilipochungulia mitandaoni, nilikutana na Wakenya, baadhi yao marafiki zangu niliodhani ni wa dhati, wakimshangilia Trump na kutabiri akishinda wahamiaji tutakiona!

Wapo walionidhihaki moja kwa moja na kuniambia nikubali yaishe, eti Trump aliwekwa uongozini na Mungu, hakuna anayeweza kumwondoa. Sikutaka kuhubiriwa wakati huo.

Nilirejewa na matumaini pale matokeo ya awali yalipoashiria hali ya Bw Biden ikiimarika, huku Trump akikwama pamoja kwa muda mrefu.

Kwamba rais wa 46 wa Marekani atakuwa mtu mstaarabu na aliyekuwa makamu wa Obama ni kitu kinachonipa raha na matumaini.

Nikizingatia kwamba hakuna uchaguzi uliowahi kuwa muhimu kwangu kama huu, na sasa matamanio yangu yanaelekea kutimia, nakuhimiza usikate tamaa kwa lolote unalokabiliana nalo. [email protected]

  • Tags

You can share this post!

ONYANGO: BBI: Uhuru, Raila wasikilize rai za wakosoaji

CHOCHEO: Uhusiano unaozaa ndoa bora huanza kwa urafiki