Makala

MUTUA: Iweje sasa Rais Trump anawatetea Waafrika?

May 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

WANENAO Kimombo husema kuwa hata saa iliyoharibika huonyesha saa sahihi angaa mara mbili kwa siku.

Ni msemo unaokusudiwa kuonyesha kuwa mtu na ubaya wake hakosi wema japo mdogo sana. Unashabihiana hulka ya Rais wa Amerika, Donald Trump, ambaye amewahi kuwadharau Waafrika kiasi cha kuyaita mataifa yao ‘mashimo ya choo’.

Nchini mwake analaumiwa kwa ubaguzi wa rangi dhidi ya wasio weupe, hasa wenye asili ya Afrika na Asia.

Wakati huu anasutana na mtangulizi wake, Barack Obama, mtu mweusi wa kwanza kuwa Rais wa Amerika.

Kisa na maana Trump amekuwa akimpiga vijembe Bw Obama, akidai kwamba mtangulizi wake huyo alimchunguza kinyemela kwa kuhusiana na Urusi.

Kumbuka inadaiwa Trump alisaidiwa na Urusi kushinda uchaguzi wa urais dhidi ya Bi Hillary Clinton mnamo 2016.

Kwa kuudhika kwamba Trump anamchokonoa kila anaposhindwa kuiongoza Amerika au akilemewa na kampeni za uchaguzi wa Novemba mwaka huu, Obama amemvaa hivi majuzi!

Obama amesema kuwa Amerika haikulishughulikia janga la korona ifaavyo; ilichelewa mno kuchukua hatua madhubuti kuwakinga raia na virusi hivyo hatari.

Kwa kawaida Bw Trump hapendi kukosolewa na yeyote, lakini hasira zake huongezeka maradufu kila Obama anaposema chochote kuuhusu utawala wake.

Juzi nusra amwite Obama, Rais wa 44 wa Amerika, mhalifu! Alidai Obama alitenda uhalifu kwa kumchunguza, madai yaliyokanushwa na hata mwanasheria mkuu wa Amerika.

Kumbuka Trump amemchimba Obama kwa muda mrefu sana, hata kabla ya Obama mwenyewe kuwa rais, hasa akidai Obama si mzawa wa Amerika, hivyo hafakufaa kuwa rais. Ijapokuwa Trump aliomba msamaha na kukubali hadharani kwamba Obama ni mzawa wa Amerika madai hayo dhidi ya kiongozi huyo mwenye asili ya Kenya huchukuliwa kuwa ubaguzi wa rangi.

Wiki chache tu zilizopita, Trump alimfokea mwanahabari Mwamerika, ila wa asili ya China – Bi Weijia Jiang – alipomuuliza kwa nini alijigamba mara kadhaa kwamba Amerika imepiku kila nchi duniani kwa vipimo vya korona.

Rais huyo alimwambia mwanahabari wa watu: “Kaiulize Uchina swali hilo! Ukiuliza swali la kijinga utapata jibu usilotarajia!” Huo pia ulichukuliwa kuwa ubaguzi wa rangi.

Hata hivyo, juzi Trump amewashangaza wengi duniani alipolaumu shirika la afya duniani (WHO) kwa kutopinga ubaguzi wa rangi unaofanyiwa Waafrika.

Huku akitishia kuondoa Amerika kwenye uanachama wa WHO, Trump alisuta shirika hilo kwa kutoishutumu Uchina, ambako Waafrika wanabaguliwa kwa misingi ya rangi yao.

Na alitishia kuinyima WHO ufadhili kabisa iwapo haitasema chochote kuhusu dhuluma hizo zilizo kinyume na kanuni za Umoja wa Mataifa.

Katika hili, naungana na Trump kwa asilimia 100 kuzilaani WHO na Uchina kwa maovu waliyofanyiwa Waafrika kana kwamba huko hakuna serikali.

Nimeona video nyingi ambapo Waafrika, hususan kwenye miji ya Guangzhou na Wuhan, wamefukuzwa kutoka vyumba wanavyopanga huku wakipigwa mno.

Video nyingine inaonyesha wazazi watarajiwa wakinyimwa huduma hospitalini kwa sababu ni weusi hali ujauzito kafika kinywani! Wanaambiwa peupe hawatibu Waafrika.

Video iliyoniatua moyo ni ya mama na mtoto wake mgongoni ambao walitoka kwenda kwenye shughuli za kutwa, wakirejea wakaambiwa hawawezi kuingia nyumbani kwao. Mtoto analilia mgongoni kwa uchovu na njaa, mama anazunguka huko na kule asipate kwa kwenda, kufumba na kufumbua Waafrika wanapigwa kwa mijeledi, mayowe yanahanikiza hewani!

Huo ni unyama unaopaswa kulaaniwa na mtu yeyote aliye na akili razini – hata Trump. Hata hivyo, inaaminika Trump aliingilia kati suala hilo kwa sababu za kisiasa.

Kwake Amerika amebanwa vilivyo na mpinzani Joe Biden, atakayezichapa naye hapo Novemba, hivyo Trump anatafuta kituko chochote ili Waamerika wasahau hajawatumikia vyema.

Iwe kweli au vingine, nimeamua mnyonge nimnyongee na haki yake nimpe.

 

[email protected]