Makala

MUTUA: Kenya isilale Kiswahili kinapoenea ulimwenguni

January 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

MABADILIKO ya baraza la mawaziri nchini Kenya yaliacha kunikosesha usingizi tangu enzi ya Rais Mstaafu Daniel Moi yalipogeuka mazoea.

Enzi hizo yakitumiwa ama kuwaadhibu au kuwazawidia wanasiasa waaminifu kwa kiongozi wa nchi bila kujali taaluma wala uzoefu wa mteuliwa kikazi.

Hizo ni nyakati ambapo Moi alipaswa kutambuliwa kuwa matawala bora, akiyaweka majalada yote kifuani na kuwakosesha kazi mawaziri, kazi yao ikawa kusoma magazeti.

Ingawa mambo yalibadilika kidogo miaka ya mwanzo ya utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, mzee wa watu huyo alimuiga Moi alipotishiwa kuzamishwa na sakata za kila aina.

Kwa mtu ambaye ameshuhudia mabadiliko mengi tu ya mabaraza ya mawaziri ya tawala zote tatu, haukupaswa kunipiga mshipa kutokana na yaliyofanywa hivi majuzi na Rais Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, nakiri hapa hadharani kwamba yalinikatisha tamaa kwa kiasi fulani.

Huenda hatua ya Rais ikayakwaza makuzi ya Kiswahili kwa namna fulani.

Kumwondoa Dkt Monica Juma kwenye Wizara ya Mambo ya Nje na kumpa nafasi hiyo Bi Raychelle Awour Omamo, huenda kutaathiri ushindani wa kukieneza Kiswahili.

Rais Kenyatta alipokuwa akifanya mabadiliko hayo, mwenzake wa Tanzania, John Magufuli, alikuwa akimpa balozi wake mpya wa Afrika Kusini majukumu ya kueneza Kiswahili.

Balozi huyo wa Tanzania, Bw Gaudence Milanzi, aliambiwa kuwa jukumu lake la kwanza akifika Afrika Kusini ni kuuliza ilikofika mipango ya nchi hiyo kuanza kufunza Kiswahili shuleni. Tuelewane hapa: Si kwamba Dkt Juma anajulikana kwa kuchangia makuzi ya lugha hii, lakini ni msomi aliye na sifa za kufanya na kufuatilia mambo ya kiusomi.

Mathalan, aliondolewa kwenye Wizara ya Mambo ya Nje akianzisha chuo maalumu cha kuwafunza maafisa wa kibalozi wa Kenya lugha za kokote watakakotumika.

Haikosi angempa maagizo balozi wetu aliye Afrika Kusini ahakikishe Wakenya hawaachwi nyuma katika juhudi za kueneza Kiswahili huko.

Sitilii shaka kujitolea kwa Bi Omamo katika uga huo, lakini sina taarifa kamili kuhusu uwajibikaji wake kwenye masuala ya kiusomi.

Na bila shaka hazungumzi Kiswahili, hivyo haikosi hakionei fahari. Hatakitetea, kukieneza wala kukipa kipaumbele kwa njia yoyote ile.

Hii ina maana kwamba huenda nafasi nyingi za kufundisha lugha hii Afrika Kusini, Sudan Kusini, Rwanda, Burundi na hata Uganda zitatwaliwa na Watanzania.

Wakati huu ambapo Kenya imejaa wataalamu ambao hawana kazi, na Serikali imeshindwa kubuni mamilioni ya nafasi za kazi ambazo iliwaahidi wapigakura, tunahitaji kila fursa ndani na nje ya nchi.

Nimeitaja Tanzania kuhusiana na kuenezwa kwa Kiswahili Afrika Kusini kwa sababu taifa hilo la marehemu Nelson Mandela lilipotangaza lingekifanyia majaribio, maafisa wa serikali ya Tanzania walitutaja.

Walisema wanajua ‘ndugu zao’ –wakirejelea Wakenya – wanakizungumza Kiswahili, hivyo walimu wao waliofuzu wawe tayari kutwaa fursa hizo kabla hatujafika huko.

Na wako katika nafasi bora zaidi kupata kazi hizo mpya kwa maana nchi yao ni mwanachama wa muungano wa mataifa ya kusini mwa Afrika (SADC) ambao unakitambua Kiswahili kama miongoni mwa lugha rasmi. Si siri kwamba Watanzania hutuonea gere kwa chochote tunachokifanya, kiasi cha kutukumbusha kwa kero kwamba wanakitumia Kiswahili kutuzidi, hivyo uhasama huo unaeleweka.

Lakini pia si siri kwamba idadi kubwa zaidi ya walimu wanaokifundisha Kiswahili ughaibuni, hasa Marekani na Uropa, ni Wakenya. Watanzania hawana lao hapo.

Mbali na kuzungumza Kiswahili sanifu kinachofundishwa shuleni, Wakenya tuna uwezo mkubwa zaidi kwa sababu tunakifahamu Kiingereza vyema, na tunaweza kuutumia utaalamu huo, hasa sarufi, kukifundisha Kiswahili.

Ukakamavu wetu na ukosefu wa woga tunapotangamana na watu kutoka pembe zote za dunia hutupa fursa ya kutamaniwa kote duniani. Natumai Kenya haitaachwa nyuma katika masuala muhimu ya kuiunganisha Afrika Bi Omamo akiwa mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje.

 

[email protected]