Makala

MUTUA: Kobe angekuwa Mkenya hangeombolezwa sana

February 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

LABDA Wamarekani wangekuwa Waafrika hawangemlilia mchezaji hodari wa mpira wa vikapu, Kobe Bryant, ambaye aliaga dunia kwenye ajali ya ndege hivi majuzi.

Mchezaji huyo aliyestaafu yapata miaka minne iliyopita alifariki pamoja na binti yake, Gianna, na watu wengine saba helikopta yake ilipoanguka na kuwaka moto.

Walikuwa njiani kwenda kuhudhuria mechi ya mpira wa vikapu ambayo binti huyo alitarajiwa kucheza.

Wamarekani wanamlilia mpaka sasa kwa sababu, ingawa alikwisha kustaafu, wanamchukulia kama nyota wao aliyecheza kwa weledi na kuwaburudisha kikweli.

Machoni pao, huyo ni bingwa wa dunia. Labda msomaji una maoni tofauti kuhusu ubingwa huo wa dunia kwa sababu mchezo huo si maarufu mno Kenya.

Pengine hata humjui Bryant, umesikia tanzia yake redioni ukipita au ukaisoma magazetini. Inaeleweka kabisa. Alikuwa tajiri wa kutupwa; sikwambii ameacha dola za kimarekani zaidi ya milioni 600.

Nimejiuliza iwapo Bryant angekuwa Mkenya, au Mwafrika kwa jumla, angesheheni sifa ambazo anazo sasa hivi hata wakati wa kifo chake.

Kisa na maana ni kwamba sisi Waafrika tumezoea kuangazia zaidi mtu – hata akiwa tajiri namna gani – anavyohusiana na jamaa zake, hasa wazazi waliomzaa na kumlea.

Kawaida yetu, hasa ikiwa hatuna mazuri ya kusema kumhusu aliyefariki, ni kunyamaza kabisa kwa madai kwamba ni mwiko kumsema vibaya aliyetuaga.

Ikiwa kuna mambo ya aibu kumhusu mwendazake, kawaida yetu Waafrika ni kunong’onezeana wakati wa maombolezi.

Hadi kufikia kifo chake, Bryant alikuwa amekaa kwa miaka kadhaa bila kuwasiliana na wazazi wake, hata kujuliana hali tu.

Walikosania mambo mengi tu ya kifamilia kwa muda mrefu kiasi kwamba wazazi wake hawakuhudhuria harusi yake.

Si hayo tu! Aliwahi kumpandisha mama yake kizimbani kwa mashtaka ya kuuza vifaa vyake vya kimichezo ambavyo Bryant alikuwa amevihifadhi kwa ajili ya makumbusho.

Mama mtu alipoulizwa sababu za kuuza mali ya mwanawe bila idhini, alisema alitaka kununua nyumba!

Na kwa kweli alinunua jumba la kifahari.

Bryant aliteta kwamba mama yake alikuwa na tamaa, hakuridhika, na kwa jumla hakukuwa na jinsi ya kuwaridhisha wazazi wake.

Hiyo ingekuwa familia ya Kiafrika, lawama zingemwendea Bryant kwa kuthubutu kukabiliana na wazazi wake hadi kuwashtaki mahakamani.

Angelaumiwa pia kwa kuwatelekeza wazazi wake ‘waliomlea na kumsomesha’, akakimbilia kuoa akiwa na umri wa miaka 21, mara tu alipopata mafedha, badala ya kuwatunza walivyomtunza akiwa mdogo.

Lakini maisha ya Marekani ni tofauti: Ukitimiza umri wa miaka 18 unachukuliwa kuwa mtu mzima kisheria, hata mzazi wako akitaka anaweza kukwambia uondoke kwake ukajitafutie makao kwingine.

Watoto wengi wa Marekani huachania na wazazi wao hapo wakaendeleza maisha yao kwa njia huru.

Labda hicho ndicho kiini cha maisha yanayoonekana kuwa ya ubinafsi ambapo kila mtu hujali maslahi yake pekee.

Huenda ni kwa sababu hiyo ambapo kukosana kwa Bryant na wazazi wake hakuchukuliwi kuwa hoja kuu na Wamarekani; kwao mwanamume wa miaka 41 hana haja na wazazi.

Labda, lakini pia nimegundua Wamarekani wanajua kutunza sifa za mashujaa wao.

Zipo sifa mbaya za kuoza za Bryant ambazo hawataki zikumbukwe na yeyote.

Mchezaji huyo aliwahi kuchunguzwa na polisi kwa ubakaji, akakiri makosa yake, lakini kesi hiyo ikamalizwa kabla ya kufikishwa mahakamani.

Ilibidi Bryant amlipe mlalamishi kitita cha pesa ambacho hakijulikani. Na alinunua msamaha wa mkewe kwa pete ya almasi ya thamani ya dola 4 milioni za kimarekani!

Ajabu ni kwamba Wamarekani, ambao hukashifu vikali ubakaji, hawataki kusikia kuhusu tukio hilo la aibu.

Limemfutisha kazi ripota wa gazeti la Washington Post aliyejadili aibu yenyewe kwenye mitandao ya kijamii.

Nadhani kila jamii ina uwezo wa kupima uwiano kati ya sifa nzuri na mbaya, na hivyo basi kuamua ni zipi za kuvumishwa huko nje.

 

[email protected]