MUTUA: Majasusi, wanajeshi wasalie katika kambi
Na DOUGLAS MUTUA
INGAWA pamekuwepo minong’ono dhidi ya hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kutwaa majukumu muhimu ya serikali ya Kaunti ya Nairobi, kiongozi huyo bado anaendelea na mabadiliko hayo.
Juzi, alimteua afisa wa kijeshi, Meja-Jenerali Mohamed Abdala Badi, mkurugenzi mkuu wa shirika jipya la usimamizi wa jiji hilo – Nairobi Metropolitan Services (NMS).
Si siri kwamba Gavana Mike Mbuvi Sonko, ambaye alichaguliwa na wananchi mnamo 2017, ameshindwa na kazi ya usimamizi, sikwambii kuzongwa na kesi mahakamani.
Hoja ya iwapo kisheria, Serikali Kuu ina mamlaka ya kutwaa majukumu ya ile ya kaunti, ingali inajadiliwa na wataalamu wa masuala ya sheria. Hawajakubaliana.
Suala ambalo nimekubali kupitwa nalo ni mazoea ya Rais Kenyatta kuwateua maafisa wa kijeshi na kijasusi kusimamia mashirika ya umma kana kwamba hakuna raia wa kawaida wenye uwezo.
Kwa mfano, amemtoa Meja-Jenerali kwenye shughuli muhimu za kusimamia mafunzo ya maafisa wa jeshi la wanahewa na kumtwika majukumu ya kusafisha mji mchafu nje-ndani.
Kumbuka, alimtoa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Haji kutoka Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) ambako alikuwa naibu mkurugenzi.
Usisahau Inspekta Mkuu wa Polisi, Hillary Mutyambai alitolewa kwenye NIS kwenda kusimamia vikosi vyote vya polisi ambavyo vimekuwa lawamani kwa mambo tele.
Hata mtangulizi wa Bw Mutyambai, Bw Joseph Boinnet, alikuwa ametolewa hukohuko NIS, akawapita maafisa wengi wa polisi walionuia kuteuliwa kuwaongoza wenzao waliokuwa wamefanya kazi nao kwa muda mrefu. Itakumbukwa kuwa, mnamo Desemba mwaka jana, tu Rais Kenyatta alimteua Bw Nicodemus Musyoki Ndalana Kamishna wa eneo la Kaskazini Mashariki.
Kabla ya uteuzi huo, Bw Ndalana alikuwa mkurugenzi msaidizi kwenye shirika la NIS ambako alisimamia kitengo kinacholinda mipaka ya nchi.
Maafisa wengine ambao Rais Kenyatta aliwatoa kwenye shirika la NIS ni mkuu wa shirika la maadili na na kupambana na ufisadi (EACC) Bw Twalib Mbarak na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji, Bw Alexander Muteshi.
Kwa Mkenya wa kawaida, ambaye bila shaka amechoshwa na uzembe wa raia wasio na uzoefu wa kijeshi wala kijasusi, mapendeleo haya ya rais yanaweza kuonekana mazuri.
Kenya, nchi ambayo kamwe haijawahi kutawaliwa na majeshi ikaona utundu na dhuluma zinazoendeshwa kwa mtutu wa bunduki, inaweza kusisimkia uchapakazi wa kijeshi ambao mara nyingi huwa wa kufikirika tu.
Hata hivyo, sharti tujiulize, kwa nini Rais Kenyatta, mtu ambaye hajawahi kutumika kwenye vikosi vya usalama, anawapendelea maafisa wenye uzoefu huo.
Ikiwa hawaamini wakuu wa mashirika ya umma na binafsi ambao hawana uzoefu wa kijeshi au kijasusi, ina maana kwamba mwenyewe hajiamini?
Ni hulka gani hasa, ambayo ametambua kwenye watu hao, ikampendeza kiasi kwamba amewateua wengi tu kuchukua kazi za raia au polisi wa kawaida?
Mtu yeyote ambaye amewahi kutumika kwenye vikosi vya usalama atakwambia kwamba, hapingi wala kuhakiki amri ya amiri jeshi mkuu, kazi yake ni kuitekeleza tu.
Huenda ni uzalendo wa aina hiyo ambao Rais Kenyatta amekosa kwenye raia wa Kenya ambao wana mazoea ya kuulizauliza maswali au kukimbia mahakamani kila amri inapotolewa?
Fikra kama hizo zimesababisha Rais wa Amerika, Donald Trump, kuwabadilisha maafisa wakuu wa serikali yake akitafuta uzalendo na kuabidiwa: ndiye bwana mkuu.
Athari za tabia hii – na Mungu atuepushane nazo – zikitokea Afrika, aghalabu huwa dalili za kiongozi kujiandaa kunata madarakani
Rais Uhuru Kenyatta anapaswa kujiepusha na vishawishi vyovyote vya kuwadharau wataalamu wa kiraia na, kuruhusu majasusi, wanajeshi kusalia kambini.