Makala

MUTUA: Sekta ya afya nchini iige yafanywayo ughaibuni

December 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

JUZI nimezama kwenye lindi la mawazo nikitafakari kuhusu masilahi ya watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) barani Afrika.

Lililochochea tafakuri zangu ni tangazo la Wizara ya Afya ya Afrika Kusini kwamba wanasayansi wa taifa hilo wametengeza dawa mpya ya kupunguza makali ya HIV.

Taarifa hiyo ilinitanabahisha kwamba Siku ya Ukimwi Duniani iliadhimishwa Desemba Mosi. Si kwamba nina mapuumba ya mambo muhimu kama siku hiyo, la hasha!

Binafsi nimewapoteza jamaa wengi tu kutokana na ugonjwa huo, hivyo basi mapambano dhidi ya virusi vyenyewe ni vita ambavyo sisiti kushiriki pale fursa inapojitokeza.

Hata hivyo, nimeambatwa na uzembe wa kukumbuka baadhi ya tarehe ambazo miaka iliyopita zilikuwa muhimu mno kwangu.

Kisa na maana? Ninaishi katika nchi ya watu ambayo ina sekta ya afya madhubuti hivi kwamba maradhi yanayotuhangaisha nyumbani Afrika hayatajwi huku.

Ingawa takwimu zinaonyesha kwamba Marekani kungali na watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, kamwe huwezi kuona matangazo yoyote kuhusu suala hilo.

Hakuna zanahati zozote maalum za watu kuenda kupimwa, wala kampeni dhidi ya virusi vyenyewe.

Si kwamba wagonjwa wanafichwa; mapambano dhidi ya HIV si suala la dharura Marekani, limedhibitiwa.

Anayehitaji dawa huzipata, lishe bora nayo ipo, hivyo huwezi kumwona mtu aliyekondeana kwa kukosa chochote kati ya vitu muhimu vya kumwezesha kuishi vyema.

Ikiwa kuna kitu ambacho nimetamani serikali zetu Afrika ziige kutoka hizi nchi za watu, basi ni usimamizi wa sekta ya afya.

Mikakati ipo ya kupambana na dharura zozote za afya, nayo maradhi ambayo yana tiba yameshughulikiwa hivi kwamba hatari za maambukizi mapya zimebanwa kikamilifu.

Mathalan, huku hakuna malaria, ugonjwa dhalimu ambao ulinitwalia mdogo wangu yapata miaka 18 iliyopita.

Huo ni wakati ambapo ugonjwa wa malaria bado ulikuwa tishio kubwa kwa wakazi wa Nairobi na maeneo ya Mlima Kenya.

Leo hii naambiwa vituo vya afya vya serikali vilivyoko maeneo hayo haviwekwi dawa za ugonjwa huo kwa kuwa inaaminika umeangamizwa kabisa.

Ukifika huko ukiwa na dalili za malaria utaulizwa iwapo ulisafiri maeneo ya Magharibi mwa nchi, Nyanza au Pwani ambako bado kuna mbu hatari wanaoeneza ugonjwa huo.

Swali ambalo limekuwa likidunda kwenye kichwa changu kwa muda sasa ni: Kwa nini serikali ya kitaifa isitumie mbinu ilizotumia kudhibiti malaria kwenye maeneo ya Nairobi na Kati kuwafaa wakazi wa maeneo mengine?

Gharama

Inaigharimu serikali kiasi gani cha pesa kuzuia maambukizi ikilinganishwa na kuwatibu watu ambao tayari wameambukizwa? Je, watu wanastahili kufa kutokana na malaria katika Karne ya 21?

Ukishukiwa kuwa na malaria nchini Marekani, basi itabidi uzuiliwe pahali pako maalum, tiba itafutwe Afrika au kwingineko, utibiwe kisha uruhusiwe kuenda nyumbani.

Maradhi mengi kama homa kali huzuiwa kwa chanjo badala ya kusubiri hadi yawe janga la kitaifa, hatua ambayo huepusha mateso na hasara.

Yale sugu kama saratani yanakabiliwa kutoka pande zote kwani takriban kila hospitali ina kitengo maalum cha utafiti na matibabu ya ugonjwa huo.

Huduma ya kusafisha figo kwa mashine, ambayo huzifilisisha familia nyingi Afrika, hutolewa bila malipo, sikwambii ukihitaji na usafiri watakujia na kukurejesha nyumbani.

Laiti serikali zote Afrika zingezingatia na kuhakikisha umadhubuti wa sekta za afya, angalau kuyaondoa maradhi ambayo yanaweza kuangamizwa, zibaki kubaliana na HIV pekee.

Afrika Kusini ilipokuwa ikijiandaa kuzindua dawa mpya za kupunguza makali ya HIV juzi, taifa jirani la Zimbabwe lilikuwa na msukosuko wa watu kujifia ovyo!

Kwa nini? Sekta ya afya imeporomoka kabisa, madaktari waligoma wakachoka, wakaishia kukimbia kazi kabisa, dawa za kimsingi hata za kudhibiti maumivu hazipo pia.

Tunajua historia ya Zimbabwe; uzembe, wizi na ulaji rushwa ni maovu ambayo yamekuwa desturi. Afrika tutaacha kuuana kama nzi tukimaliza maovu haya.

 

[email protected]