Makala

MUTUA: Serikali iache masihara kuhusu virusi vya Corona

February 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

MAREKANI inapanga kutowapokea wasafiri kutoka mataifa rafiki – Italia na Korea Kusini – kutokana na kuweko visa vingi vya coronavirus.

Saudia imesitisha hija ndogo iitwayo Umrah, ambayo huendelea mwaka mzima, ikawaambia mahujaji wajikalie kwao ili wasieneze ugonjwa huo unaoua kwa kasi.

India haikupoteza wakati; imefutilia mbali vibali vyote vya kusafiria ambavyo iliwapa watu kutoka China na ikatangaza mikakati kabambe ya kuzuia maambukizi.

Nao waandalizi wa michezo ya Olimpiki, ambayo itafanyika jijini Tokyo, Japan, kuanzia mwishoni mwa Julai, wanakadiria gharama na huenda wakaamua kutoiandaa.

Kenya yetu imechukua hatua gani kuwalinda wananchi wake ambao wakiambukizwa tu wataanza kuandaa mazishi?

Imewakagua kimzaha wasafiri waliofika nchini kutoka China, ambayo ni chemchemi ya ugonjwa huo, kisha ikawaachia huru na kuwaambia wajizuie kutotangamana na watu.

Huku hayo yakiendelea, naibu waziri wa Afya wa Iran, Iraj Harirchi, ambaye wiki jana alificha habari za kusambaa kwa ugonjwa huo nchini mwake, ameambukizwa.

Bw Harirchi na mbunge wa nchi yake ni miongoni mwa watu wachache mashuhuri nchini humo ambao wamelazwa hospitali na kuzuiwa kutangamana na watu ili wasiwaambukize.

Inakisiwa kwamba watu karibu 3,000 wamefariki kutokana na homa hiyo. Wengi waliofariki ni raia wa China.

Ugonjwa wenyewe umetangazwa dharura na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kuwa umeenea kila bara duniani.

Tayari umeathiri chumi za mataifa makuu na tajiri duniani kama China, Marekani na yale ya bara Uropa kwani mazingira ya kufanya biashara hayatamanishi.

Barani Afrika, Algeria na Nigeria zimeripoti kuwepo kwa visa vya ugonjwa huo, hali ambayo inawatia wengi hofu kwani ugonjwa wenyewe unasemekana kuenea kwa kasi mno.

Changamoto kuu kwa wadau wa afya ya jamii kote duniani ni kwamba ugonwa wenyewe haudhibitiki rahisi na viini vinaweza kukaa mwilini kwa takriban siku 27 bila kugunduliwa.

Cha mno ni kwamba wanasayansi wamesema chanjo ya ugonjwa huo ingali inaandaliwa, eti labda itakuwa tayari baada ya wiki mbili au tatu kuanzia sasa.

Angalia: Marekani imetishia kuchukua hatua hizo kali baada ya raia wake 60 kuambukizwa, baadhi yao nje ya nchi. Wanasayansi wake wamo mbioni kutafuta chanjo.

Na kuna uwezekano wa kuanzisha mipango ya watu kufanyia kazi nyumbani kwa kompyuta na wanafunzi kujisomea makwao hali ya dharura ikitangazwa.

Marekani na uwezo wake wote wa kifedha na kimatibabu iko radhi kuchukua hatua hizo, lakini Kenya, ambayo hata vidonge vya kudhibiti maumivu kupata ni shida, haijali.

Ni makadirio gani ya haraka hivyo ambayo yalifanya kuamua kwamba wasafiri hao 239 waliotoka China hawakuhitaji udhibiti na uangalizi wa wataalamu kwa saa 24 hadi ithibitike kwamba hawana virusi?

Ni kupotoka kwa hali ya juu kwa serikali kuwaagiza watu hao eti wajidhibiti wenyewe kwa muda wa siku 14 ili wasiwaambukize watu.

Wewe unaweza kufanya hivyo ilhali umekuja nchi ya watu kwa sababu ulitaka kukamilisha shughuli fulani?

Ingawa tunazungumza kuhusu watu 239 ambao waliachiwa huru wajidhibiti, huenda tayari maelfu wameshaingia Kenya kutoka China.

Hao tunaowajadili walikuwa kwenye ndege moja tu, lakini mjo wao ulikuwa mwanzo wa kurejelewa kwa safari za kampuni ya ndege ya China Southern nchini Kenya.

Hiyo ni hatua ya kuatua moyo sana kwa maana dunia nzima inakabiliana na hatari ya maambukizi kwa kuwazuia Wachina kusafiri, nasi tunakwenda kinyume na kanuni.

Hatuhitaji wagonjwa 239 kutua nchini Kenya ndio tuanze kuanguka kama nzi!

Mmoja tu anatosha, maambukizi yakianzia kusini yafike kaskazini, mashariki na magharibi ghafla!

Serikali inapaswa kabatilisha uamuzi huo wa kurejelewa kwa safari za ndege na kampuni yoyote ya China na udhibiti zaidi ufanywe ili kuwaweka salama Wakenya.

 

[email protected]