MUTUA: Watakaotungua Trump wafuate sheria si siasa
Na DOUGLAS MUTUA
NINAFAHAMU fika kwamba kuondolewa, au vinginevyo, madarakani kwa Rais Donald Trump wa Amerika hakuna athari za moja kwa moja kwa Mkenya wa kawaida.
Hata hivyo, kwa maana wajuaji wa kusema hudai kila Amerika inapochemua, dunia nzima hupata mafua, sina budi kukumegea mawili matatu kuhusu mchakato huo.
Na bila shaka tumejua kwamba, baadhi ya sera za Amerika zinaweza kuwaathiri Wakenya wengi, hasa tukitilia maanani afya ya uzazi na mapambano dhidi ya Ukimwi.
Trump alitutikisa kidogo alipoingia madarakani na ghafla akazinyima fedha zahanati fulani nchini Kenya zilizojulikana kwa uavyaji mimba.
Ufadhili wa miradi ya kupambana na Ukimwi pia ulipungua pakubwa kwa maana sera za serikali yake ni kuangalia maslahi ya Waamerika kwanza, si kugawa fedha kote kote. Kuhusu juhudi za kumchunguza na hatimaye kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye zinazoendeshwa na chama cha upinzani cha Democrat, Trump yuko imara mpaka sasa. Bunge la wawakilishi, Congress, ambalo ni la ngazi ya chini, linadhibitiwa na chama cha Democrat. Lile la juu, yaani Seneti, linadhibitiwa na chama chake cha Republican.
Mambo yanavyokwenda huku, haswa kuhusu harakati za kumwondoa rais madarakani, Bunge la chini hupiga kura kimtindo tu, ila jukumu la kumhukumu na kumtungua ni la Seneti.
Ili Seneti ifanikiwe kumpata na hatia na kumwondoa, sharti maseneta 67 – kati ya wote 100 – wapige kura kuunga hoja ya kumwondoa. Hilo kwa sasa, hata kwa dawa, haliwezekani! Labda baadaye, kashfa hizi zisizoisha zikiendelea kuibuka na kuwashawishi maseneta wengi wa chama cha Republican kwamba, fedheha anayowapa kiongozi wao huyo haivumiliki tena.
Kwa ufupi, Congress inaweza kupitisha hoja ya kutokuwa na imani na Trump, hata kila siku kuanzia leo hadi uchaguzi mkuu wa mwakani, ila shughuli hiyo haizidishi haipunguzi.
Kumbuka, Bunge hilo lilipitisha hoja mia ngapi sijui za kuifuta ile sheria ya afya kwa wote iliyoletwa na Rais wa 44, Barrack Obama, ila juhudi hizo hazikulifaidi kitu.
Je, ni kitu kizuri kwa wabunge wa Democrat kujaribu kumwondoa Trump madarakani mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu utakaomng’oa au kumpa kipindi cha pili?
Hilo ni swali ambalo limezua mgawanyiko mkubwa ndani ya chama cha Democrat: Wapo wanaosema juhudi hizo hazifai wakati huu kwani akiponea, ataibuka imara zaidi na kushinda uchaguzi ujao. Huo ni mtazamo wa kisiasa.
Wapo pia wafuasi wa Democrat wanaosema jaribio la kumwondoa linafaa kwani linaweza kufaulu, hivyo basi wasilazimike kukutania naye kwenye debe la kura mwakani. Huo pia ni mtizamo wa kisiasa.
Mitizamo yote miwili ina matatizo kwa sababu haijikiti kwenye Katiba ya nchi. Unaosema ataibuka imara si wa hakika, anaweza kuwa hafifu, hivyo matokeo hayajulikani kabisa. Kwa maoni yangu, uamuzi wa kumwondoa Trump haupaswi kutegemea uwezekano wake kuponea au la, bali unafaa kujikita kwenye Katiba ya Amerika.
Katiba yenyewe inaorodhesha makosa ambayo yanaweza kumsababisha rais ang’olewe madarakani, na kwa hakika Trump ameyafanya mengi tu!