Makala

Mutula Kilonzo Junior alazimika kuomba radhi kwa matamshi yake kuhusu HIV Homa Bay

Na GEORGE ODIWUOR April 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Makueni Mutula Kilonzo Junior, alijiaibisha hadharani kwa kauli yake kuhusu mienendo ya wagonjwa wa Ukimwi katika kaunti ya Homa Bay.

Gavana huyo alilazimika kuomba msamaha kutoka kwa wakazi wa Homa Bay kwa kuonya vijana kutoka Makueni kuwa waangalifu wanapozuru kaunti hiyo inayopakana na ziwa Victoria wasije wakafanya kosa na “kuambukizwa Ukimwi.”

Vijana kutoka Makueni ni miongoni mwa wale wanaoshiriki katika Makala ya 10 Mashindo ya Michezo ya Vijana kutoka Kaunti zote nchini (KYISA).

Michezo hiyo itafanyika kwa kipindi cha siku sita kuanzia Aprili 13 na inashirikisha fani za kandanda, voliboli, mpira wa vikapu na voliboli ya ufukweni.

Michezo hiyo itaandaliwa katika Asumbi Complex kwenye eneo bunge la Rangwe na washiriki ni vijana kati ya umri wa miaka 18 na 23.

Ndiposa Gavana Kilonzo Junior akawashauri vijana kutoka Makueni kujihadhari wasishiriki mienendo inayoweza kuchangia wao kuambukizwa virusi vya HIV.

Kaunti ya Homa Bay ni mojawapo ya zile zenye viwango vya juu vya maambukizi ya Ukimwi ikiandikisha kima cha asilimia 10.6, kulingana na Baraza la Kitaifa la Kupambana na Magonjwa ya Kuambukiza (NSDCC).

Gavana Kilonzo Junior, akirejelea wimbo “Vuta Pumzi” unaoangazia masuala ya kijamii kama ugonjwa wa Ukimwi, aliwashauri vijana kutoka Makueni wasishiriki mienendo mibaya wakiwa Homa Bay.

“Kama mzazi, sharti niseme hili kwa sababu sitaonyesha uwajibikaji nisipofanya hivyo. Homa Bay ni kaunti nzuri lakini wakazi wanapenda anasa, tofauti na wakazi wa Makueni,” akasema.

Alionekana kuashiria kuwa mienendo hiyo inachangia ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya HIV miongoni mwa wakazi.

Kulingana na Bw Kilonzo Junior, wagonjwa wa Ukimwi katika kaunti ya Homa Bay wamefanya ugonjwa huo kuonekana wa kawaida.

Alidai amesikia kuhusu visa ambapo wagonjwa hawaathiriwi na unyanyapaa kiasi kwamba baadhi yao huwaomba watu wengine kuwasaidia kupata dawa za kupunguza makali ya Ukimwi kutoka hospitali mbalimbali.

“Hawaogopi virusi vya HIV. Hawana unyanyapaa, ni sehemu ya maisha,” akasema.

Gavana Kilonzo Junior pia alisema kuwa kaunti ya Homa Bay inayo viwango vya juu vya maambukizi ya Malaria na magonjwa mengine yanayosambazwa kupitia maji chafu.

Hata hivyo, kiongozi huyo aliisifu kaunti hiyo kwa kuwa na mandhari mazuri, mikahawa mizuri na visiwa.

Lakini kauli za Bw Kilonzo Junior hazikuwafurahisha wakazi wa Homa Bay waliomtaka gavana huyo wa Makueni kuomba msahama.

Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang alisema hakutarajia kuwa gavana huyo kutoa kauli kama hiyo.

“Inasikitisha kuwa anadai kuwa Homa Bay ni ngome ya maradhi na mienendo mingine mibaya bila sababu zozote. Sisi pia tuko na dhana potovu kuhusu Makueni lakini hatuwezi kusambaza mambo yasiyo na msingi,” akaeleza.