Mvulana shujaa asimulia alivyomzidia mamba nguvu na kunusurika mtoni
MVULANA kutoka Kaunti ya Kitui amesimulia jinsi alivyoibuka shujaa kwa kukabili kiboko na mamba walipomvamia kwenye Mto Athi mpaka akanusurika kinywani mwa mamba.
Dennis Mutunga, 13 ambaye ni mwanafunzi wa gredi ya sita katika Shule ya Katilini alikuwa akiteka maji alipovamiwa na mamba kutoka upande wa nyuma mwezi uliopita.
“Alinivuta hadi mtoni, nikavuta pua yake na kupambana nisiingie majini. Mpango ulikuwa nimkoseshe hewa ili nihepe makali ya meno yake na mpango huo ulifanya kazi,” akasema Dennis.
Bado amelazwa katika hospitali ya Makindu, Kaunti ya Makueni.
Pambano na mamba huyo lilimuacha Dennis akitokwa na damu kwenye mapaja yake lakini ametibiwa na sasa hayuko katika hatari yoyote kiafya.
“Tumefaulu kumtibu na sasa yuko hali thabiti kiafya. Mwishoni mwa wiki hii tutamruhusu aende nyumbani ili aendelee na shughuli na masomo yake,” akasema Supritendi Mkuu wa Hospitali ya Makindu Emmanuel Laiposha.
Babake Dennis Munyao Kombo naye alitaja kunusurika kwa mwanawe kama muujiza.
“Kumnyima mamba hewa ni sehemu ya kupigana naye na humlazimisha aachilie windo lake kwa sababu lazima apanue mdogo ndipo apumue. Ni muujuza jinsi Dennis alivyonusurika,” akasema Bw Kombo.
Tukio hilo lilifanyika wakati ambapo maji ya Mto Athi yamepungua na kuna visa vingi vya uvamizi wa mamba na viboko.
Naibu Chifu wa Kathumbi, John Nyamai alisema kuwa uvamizi huo hushuhudiwa kwa sababu wakazi na wanyama hao wote wanayatumia maji ya mto huo wakati wa msimu wa kiangazi.
Kwa mujibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu, kaunti za Kitui na Makueni zimekuwa zikishuhudia uvamizi mwingi wa mamba, visa vinavyotokea kila baada ya miezi miwili kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.
“Uvamizi wa mamba umeongezeka na kufikia 28 ambapo mauti ya watu 14 yameripotiwa,” akasema Solomon Musia, mshirikishi wa kupambana na majanga ya kidharura eneo hilo.
Jana, mwanamke mmoja alikuwa bado anapokea matibabu kwenye Hospitali ya Makindu baada ya kunusurika kuvamiwa na mamba mnamo Jumapili.
Siku iliyotangulia (Jumamosi) watu wawili walivamiwa na mamba na mwingine kiboko walipojaribu kuvuka sehemu ya Mto Athi inayopakana na Kaunti ya Makueni.
Miili yao ilipatikana japo juhudi za kupatikana kwa mwili wa mvulana aliyevamiwa katika kijiji cha Kanyonga, Kaunti ya Makueni bado zinaendelea kwa wiki ya tatu sasa.