Mvutano wazuka kati ya kampuni za kusaga miwa ukanda wa Magharibi
MVUTANO umezuka kati ya kampuni za kusaga miwa eneo la Magharibi baada ya shughuli hiyo iliyosimamishwa miezi miwili na Bodi ya Sukari nchini (KSB) kurejea.
KSB ilisimamisha mchakato wa kusaga miwa kutokana na uhaba wa miwa ambao ulisababisha wakulima kung’ang’ania miwa ambayo haijakomaa jambo lililoathiri ubora wa sukari.
Madai ya uvamizi, wizi wa miwa na uvunaji wa miwa kabla ya wakati yanazua mgogoro kati ya wakulima katika eneo hilo.
Ukanda wa Magharibi una viwanda sita vya sukari vikiwemo Kampuni ya Sukari ya Mumias, Nzoia, Butali, West Kenya, Ole Pito na Naitiri.
Malumbano mapya na madai ya hujuma yametikisa sekta hiyo baada ya Kampuni ya Sukari ya Mumias (Msc) kuishutumu Kampuni ya Sukari ya West Kenya, kwa kuajiri mtu wa ndani kuhujumu mashindano hayo.
Mumias inadai West Kenya inavamia na kuiba miwa katika shamba lake kabla ya kukomaa hata baada ya KSB kugawa kaunti ya Kakamega katika kanda mbili na kuipa kila kampuni eneo lake la kufanya kazi.
‘Tunadai kwamba KSB ibaki imara na kutekeleza agizo la kugawa maeneo ili kurahisisha utendakazi katika sekta hii,’ alilalamika Meneja wa Kampuni ya Sukari ya Mumias, Stephen Kihumba.
Alisema Mumias imetengeneza miwa katika hekari 3,428 za shamba lake na inajishughulisha na mpango wa kukarabati na kuboresha mashamba ya wakulima wa nje.
‘Tulipochukua madaraka mwaka 2021, shamba letu lilikuwa shamba la malisho na sehemu nyingine ilikuwa imenyakuliwa kwa ajili ya kilimo cha mahindi. Lakini leo, tumefunga hekari zote 3,428 na 2,128 za ziada kwa wakulima wa nje,’ aliongeza akisisitiza kwamba wakulima wanaosambaza miwa wanalipwa ndani ya siku saba.
Mnamo Oktoba 16, 2025, trekta ya West Kenya ilizuiliwa katika eneo la Makokha katika kaunti ndogo ya Matungu ikiwa imesheheni miwa ambayo ilikuwa imevunwa kutoka kwa mkulima aliyepewa kandarasi na Mumias.
Bw Kihumba alidai kuwa Mumias iliwasiliana na mkulima huyo na kuelekeza shughuli zote za shambani ikiwa ni pamoja na kulima shambani na usambazaji wa mbegu na mbolea.
“Kwa kuvuna miwa katika shamba ambalo hawajawekeza inaashiria kwamba hakuna nidhamu katika sekta hiyo hata kidogo,” akadokeza Bw Kihumba.
Aidha ilishutumu kampuni ya Kenya West kwa kuvuna miwa kabla ya muda wa miezi 13.