Makala

MWALIMU KIELELEZO: Elizabeth Achieng Odongo

November 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

KUWAFUNDISHA wanafunzi wenye mahitaji maalumu ni wito!

Siri ya kuwa mwalimu bora hasa kwa wanafunzi wa sampuli hii ni kutawaliwa na upendo wa dhati kwa taaluma, kuchangamkia masuala yanayohusiana na mtaala na kuwa mwepesi wa kubuni mbinu mbalimbali za ufundishaji.

Kusoma kwingi, kufanya utafiti wa kina kuwahusu na kuwauliza wajuao pia kutakujenga. Ili kufikia kiwango cha uelewa kinachohitajika miongoni mwa watunga-sera na wakufunzi wa walimu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu, utetezi na jitihada za uelimishaji zinapaswa kutiliwa mkazo.

Haya ni kwa mujibu wa Bi Elizabeth Achieng Odongo ambaye kwa sasa ni mwalimu katika Shule ya Msingi ya Sacred Heart, eneo la Ganjoni, Kaunti ya Mombasa.

Elizabeth anashikilia kwamba ipo haja kwa watunga-sera na wakufunzi wa walimu kuelewa vyema elimu jumuishi ili waweze kukuza kiwango cha kushirikishwa kwao katika masuala mbalimbali.

“Mafunzo ya ualimu lazima yawe na uwiano wa nadharia na vitendo. Yanahitaji kuwa na uwiano wa kujifunza kuhusu dhana ya elimu jumuishi. Walimu wanapaswa kuangalia na kutekeleza nadharia hizi kivitendo huku wakisaidiwa na wenzao wenye uzoefu zaidi,” anasema Elizabeth kwa kusisitiza kuwa mafunzo yenyewe yanahitaji kuwiana na mazingira na tamaduni za watu mbalimbali.

Elizabeth alizaliwa mnamo 1967 katika kijiji cha Kanyaluo Owuor, Kaunti ya Homa Bay. Ndiye mtoto wa tano katika familia ya watoto wanane wa marehemu Bw Shem Odongo Omollo na marehemu Bi Priscillah Agolla.

Elizabeth alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Kowuor, eneo la Rachuonyo Kaskazini, Homa Bay mnamo 1974. Huko ndiko alikosomea hadi mwishoni mwa 1981 alipofanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Saba (CPE).

Alama nzuri alizojizolea katika mtihani huo zilimpa nafasi ya kusomea katika Shule ya Upili ya St Mary’s Lwak Girls, eneo la Rarieda, Kaunti ya Siaya kuanzia 1982 hadi 1985 alipofanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCE).

Kati ya walimu waliompokeza malezi bora ya kiakademia na kumhimiza ajitahidi zaidi masomoni ni Bw Ako wa Shule ya Msingi ya Kowuor na Bw Orina na Bi Audi waliomfundisha katika Shule ya Upili ya Lwak Girls.

Baada ya ndoto za kusomea masuala ya upishi kuzimika ghafla mwanzoni mwa 1986, Elizabeth alihamia jijini Mombasa kuishi na dadake Tryphose Odero ambaye hadi kustaafu kwake, alikuwa mwalimu katika Shule ya Msingi ya Jamvi La Wageni, Likoni.

Baada ya kuchochewa pakubwa na kazi ya dadake, Elizabeth alitafuta kibarua cha kufundisha katika Shule ya Msingi ya Mtongwe, Likoni. Alihudumu huko kati ya 1987 na 1990 kabla ya kuhamia Shule ya Msingi ya Shika Adabu, Likoni alikofundisha kwa miaka minne.

Akiwa Shika Adabu, Elizabeth alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Shanzu, Mombasa alikosomea kati ya 1991 na 1994.

Baada ya kuhitimu, Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma kufundisha katika Shule ya Msingi ya Likoni (1994-1996) kabla ya kupata uhamisho hadi Shule ya Msingi ya Ronald Ngala, Mvita, Mombasa alikofundisha kati ya 1997 na 2004. Ilikuwa hadi Januari 2005 ambapo Elizabeth alijiunga na Shule ya Msingi ya Sacred Heart anakofundisha sasa masomo ya Kiingereza, Dini na Sayansi.

Elizabeth amewahi pia kusomea Diploma ya Elimu ya Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalumu (Special Needs Education) katika Taasisi ya Kenya Institute of Special Education (KISE) kati ya 2002 na 2004. Baada ya kuhitimu, alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea shahada ya Elimu ya Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalumu kati ya 2005 na 2009.

Elizabeth aliolewa na mumewe mpendwa Bw Maurice Obogo mnamo 1988 na wamejaliwa watoto wanne – Patrick Wilson, 31, Bob Hillary, 29, Ian Omondi, 24, na Julie Akinyi, 23. Wanamlea pia Mark Wamalwa, 16, ambaye ni mtoto wa kakaye Bw Obogo.

Wakfu wa Aga Khan umekuwa mstari wa mbele kupiga jeki juhudi za Elizabeth katika kuchangia maendeleo ya jamii tangu 2019. Wakfu huo umemnufaisha kidijitali na kumpa jukwaa la kutalii mbinu tofauti za kufundisha wanafunzi.

Mwalimu Elizabeth Achieng Odongo wa Shule ya Msingi ya Sacred Heart, eneo la Ganjoni, Kaunti ya Mombasa. Picha/ Chris Adungo

Isitoshe, umemwezesha kufahamu maisha ya awali ya baadhi ya wanafunzi wake, kujifunza tamaduni mbalimbali na kuielekeza jamii kimaadili.

Katika kipindi cha zaidi ya miaka 30 iliyopita ya ualimu, Elizabeth amefundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali. Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wengi wa wanafunzi na walimu ambao wametangamana naye katika makongamano mbalimbali ya kupigia chapuo masuala ya elimu.

Mbali na kufundisha, Elizabeth pia ni Mkuu wa Kitengo cha Elimu katika Kanisa la Waadventista wa Sabato (Seventh Day Adventist Church) Ziwani, Mombasa.

Aliwahi pia kuwa kiongozi wa masuala ya kifamilia katika kanisa hilo mnamo 2011 na 2015 ambapo alikuwa akiwashauri wanandoa na kuwaelekeza vijana kuhusu jinsi ya kujitegemea na kukabili changamoto mbalimbali maishani. Aliwafundisha pia waumini wenzake kuhusu namna ya kuchangia maendeleo ya jamii kwa uzalendo, umoja na ukakamavu zaidi.

Ukulima wa mimea mbalimbali na ufugaji wa kuku ni kazi ambayo Elizabeth anapania kumakinikia zaidi baada ya kustaafu.