MWALIMU KIELELEZO: Elizabeth Kadzo Ziro wa Shule ya Utange, Mombasa
Na CHRIS ADUNGO
WATOTO wote wana haki ya kulindwa.
Kila mtoto ana haki ya kuishi, kuwa na wazazi au walezi, kusikilizwa, kupata huduma muhimu na kulelewa katika mazingira salama.
Familia ndicho chanzo cha ulinzi wa mtoto. Wazazi au walezi wengine wana jukumu la msingi la kutengeneza mazingira ya nyumbani ambayo ni salama na yenye upendo. Shule na jamii ina jukumu la kutengeneza mazingira ya nje ya nyumbani ambayo ni salama na faafu kwa mtoto.
Kwa bahati mbaya, mamilioni ya watoto hawana ulinzi – baadhi wananajisiwa na kulawitiwa. Kila siku watoto wengi wanakabiliwa na ukatili. Wananyanyaswa, kutelekezwa, kudhulumiwa, kutengwa na kubaguliwa. Aina hizi za ukiukwaji wa haki za watoto hupunguza uwezekano wao wa kuishi, kukua vizuri na kufikia ndoto zao.
Idadi kubwa ya watoto hutumikishwa badala ya kufurahia utoto wao. Mbali na idadi kubwa ya watoto wa umri mdogo kutumikishwa katika ajira, kuna wengi ambao pia huozwa kwa ulazima na kutiwa katika ndoa za mapema.
Haya ndiyo maovu ambayo Bi Elizabeth Kadzo Ziro amepania kukomesha kabisa katika eneo la Shanzu, Kaunti ya Mombasa.
Katika maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani mwaka huu, Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilitambua juhudi za Bi Kadzo katika kupigania haki za wasichana wanaodhulumiwa kimapenzi na kuozwa kwa lazima katika eneo la Utange, Mombasa.
“Mbali na majukumu ya kawaida ya kufundisha, yapo mambo mengi ambayo watoto wanastahili kufanyiwa. Ni wajibu wa mwalimu kutambua na kukuza vipaji vya wanafunzi wake na kuwa tayari kuwasaidia wanapopitia changamoto za aina mbalimbali. Msaada kwa wanafunzi wa sampuli hii ndio hunipa tija katika kazi yangu,” anasema Bi Kadzo ambaye kwa sasa ni mwalimu katika Shule ya Msingi ya Utange, Mombasa.
Kadzo alizaliwa jijini Nairobi mnamo 1973. Ndiye mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto wanne wa Bi Constance Ziro na marehemu Bw Joseph Ziro ambaye hadi kufariki kwake, alikuwa mfanyakazi wa kampuni ya umeme ya Kenya Power & Lighting, Kaunti ya Lamu.
Mbali na Bi Mary Kahonzi Ziro ambaye kwa sasa ni Naibu Mwalimu Mkuu katika Shule ya Upili ya Mwijo, Kaunti ya Kilifi, ndugu wengine wa Kadzo ni Moses Ziro (Nairobi) na John Safari Ziro (Kwale).
Baada ya kusomea katika chekechea ya Kibaki, Lamu mnamo 1980, Kadzo alijiunga na Shule ya Msingi ya Mkomani Girls, Lamu. Alisomea huko kwa mwaka mmoja pekee mnamo 1981 kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Kinarani, eneo la Kaloleni, Giriama, Kaunti ya Kilifi. Alisomea huko kuanzia 1982 hadi alipofanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwishoni mwa 1988.
Alama nzuri alizozipata zilimpa nafasi katika Shule ya Upili ya St John’s Girls Kaloleni alikosomea kati ya 1989 na 1992.
Kadzo alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Shanzu, Mombasa mnamo 1993. Alifuzu mnamo 1995 na akaajiriwa na TSC iliyomtuma kufundisha katika Shule ya Msingi ya Kizurini, Kaloleni. Alihudumu huko hadi 1998 kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Kinarani (1999-2001). Kati ya shule nyinginezo ambazo Bi Kadzo amewahi kufundisha ni Navy Primary Mtongwe, Likoni (2002-2005), Mlaleo Primary Kisauni (2005-2015) na Frere Town Kisauni (2015-2018).
Wakfu wa Aga Khan umekuwa mstari wa mbele kupiga jeki juhudi za Bi Kadzo katika kuchangia maendeleo ya jamii tangu 2014. Zaidi ya mafunzo ya kumwezesha kuwapokeza wanafunzi malezi bora ya kiakademia katika eneo la Shanzu, Mombasa, Wakfu wa Aga Khan umemnufaisha pia kidijitali na kumpa jukwaa la kutalii mbinu tofauti za kufundisha idadi kubwa wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi la sita.
Kwa mtazamo wa Bi Kadzo, uzuri wa kufundisha watoto wa umri mdogo ni kwamba wanaelewa mambo upesi, wana hamu ya kujifunza vitu vipya na ni rahisi kuwadhibiti.
“Kudumisha urafiki na watoto humfanya mwalimu kujihisi mkamilifu. Kilele cha urafiki huo ni pale wanafunzi wanapokuwa radhi kukupa hadithi za kila sampuli kuhusu maisha yao binafsi,” anasema kwa kukiri kwamba ualimu ni kazi inayompa mtu jukwaa la kubadilisha maisha ya watu wengi katika jamii.
Japo maazimio yake yalikuwa ni kusomea udaktari, Bi Kadzo alivutiwa na ualimu baada ya kuona kuwa waliokuwa wakiifanya kazi hiyo walikuwa watu wa kuheshimika zaidi katika jamii, walikuwa wamepiga hatua kubwa kimaendeleo, walitegemewa sana kwa ushauri wa kila aina na ilikuwa tija kujihusisha nao.
Kati ya watu waliomhimiza sana Bi Kadzo kujitosa katika taaluma ya ualimu ni Bw Jacob Ziro wa Shule ya Msingi ya Kinarani na Bw Mlewa aliyemfundisha katika Shule ya Upili ya St John’s Girls Kaloleni.