Makala

MWALIMU KIELELEZO: Millicent Loice Achieng

September 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

KUJIFUNZA kusoma na kuandika ni kazi ngumu!

Kwa sababu unataka wanafunzi wamakinikie masomo haya, ni muhimu ufanye darasa lako liwe la kusisimua kadri iwezekanavyo.

Wanafunzi wanahitaji kujua jinsi ya kuhusisha sauti na herufi, herufi na maneno, maneno na sentensi.

Michezo, michoro, picha za rangi, nyimbo na mashairi ambayo wanafunzi wanajua vizuri – na ambayo wanaweza kuimba na kughani kirahisi kwa vitendo – yatawasaidia kujenga mahusiano haya.

Njia nyingine ya kukuza uhusiano huo miongoni mwa wanafunzi wa madarasa ya chini ni kuwashirikisha katika usomaji na usimulizi wa hadithi.

Haya ni baadhi ya majukumu ambayo Bi Millicent Loice Achieng hujitahidi kufanikisha katika Shule ya Msingi ya Kenya Navy Mtongwe, Kaunti ya Mombasa.

Bi Achieng anavutiwa sana na ualimu kiasi kwamba hata wakati huu wa janga la corona, amekuwa akifundisha idadi kubwa ya wanafunzi wa chekechea katika eneo la Mtongwe mjini Likoni anakoishi.

“Unaposoma na watoto, usiwafafanulie kila kitu kwenye picha za vitabu au michoro ya chati. Waulize wanafikiri kitu gani kitatokea au kitafuata baadaye.

“Kumbuka kuwapa fursa nyingi ili wazungumzie kuhusu unachowafundisha – wahusika katika hadithi, kilichotokea, wanachohisi kuhusiana na hadithi n.k.”

Bi Achieng amegundua kwamba wanafunzi wanahitaji mazoezi mengi ili wajiamini katika usomaji. Yeye hutengeneza nakala nyingi za michoro, picha na chati za alfabeti na nambari kwa minajili ya ufundishaji.

Aidha, hutunga mashairi mepesi na nyimbo ambazo wanafunzi wanazijua vizuri na nyingine ambazo ni mahsusi kwa ajili ya kufundishia dhana mpya.

Wanafunzi huzitamka au huziimba kwa kuonyesha vitendo kuhusiana na tungo hizo wanapocheza.

“La muhimu zaidi ni kuwapa fursa ya kusoma herufi na maneno husika kisha wayaoneshe ubaoni au kwenye chati huku ukiwasaidia wanapotatizika,” anaeleza.

Ikilazimu, Bi Achieng huandaa kadi zenye picha, nambari, herufi na maneno katika masomo saba anayoyashughulikia ili kuzitumia kusomesha wanafunzi wake mmoja mmoja au katika vikundi vidogo.

Bi Achieng anafarijika kuona kuwa mazoezi ya sampuli hii yanasaidia mno kuwafanya wanafunzi wajiamini na kusonga mbele.

“Kusoma na kuandika kunaweza kusisimua na kuchangamsha sana. Lakini baadhi ya wanafunzi wanajenga mitazamo hasi kwamba kusoma na kuandika ni kugumu; labda kwa kuchoshwa na kazi za usomaji na uandishi ambazo zinafuata ruwaza zilezile daima, au pengine hawaoni thamani kubwa katika usomaji na uandishi.”

Mojawapo ya majukumu ya mwalimu ni kuamsha ari ya wanafunzi ya kusoma na kuandika, na kuwafanya wahamasike zaidi.

“Hakuna kinachonipa fahari zaidi katika taaluma ya ualimu kuliko kutangamana na watoto wachangamfu kupitia michezo, uimbaji na utambaji wa hadithi. Watoto wanaweza hata kukufanya usahau shida na changamoto za maisha,” anakiri Bi Achieng.

Kwa mtazamo wake, uzuri wa kufundisha watoto wachanga wa chekechea ni kwamba wanaelewa mambo upesi, wana hamu ya kujifunza vitu vipya na wanasahau haraka hata unapowaadhibu kwa utundu.

“Kudumisha urafiki na watoto humfanya mwalimu kuwa mkamilifu. Kilele cha urafiki huo ni pale wanafunzi wanapokukimbilia na kuwa radhi kukupa hadithi za kila sampuli kuhusu maisha yao binafsi.”

Bi Achieng alizaliwa katika eneo la Changamwe mjini Mombasa na kulelewa maeneo ya Majengo na Kongowea jijini humo, na pia eneo la Nyahera katika Kaunti ya Kisumu. Wazazi wake ni Bw Robert Ayieko Othano na marehemu Bi Helidah Were.

Alianza safari yake ya elimu mwishoni mwa miaka ya 1970 katika chekechea ya Majengo Social Hall, Mombasa, kabla kujiunga na Shule ya Msingi ya Achego, eneo la Songhor, Muhoroni. Alifanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) katika Shule ya Msingi ya Khadija mjini Mombasa mnamo 1988.

Alifaulu vyema na kupata nafasi ya kusomea katika shule maarufu ya Matuga Girls, Kaunti ya Kwale, kati ya 1989 na 1992.

Baada ya kukamilisha mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE), Bi Achieng alipata kibarua cha kufundisha katika Shule ya Msingi ya Curtis Kongowea Baptist mjini Mombasa, kati ya 1993 na 1996.

Alifunga ndoa mwishoni mwa 1996 na kuanza kufanya biashara katika eneo la Mtongwe, Mombasa. Amejaliwa watoto wanne.

Ilikuwa hadi 2006 ambapo alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha St John’s Kilimambogo, Thika. Alifuzu mnamo 2008 na akafundisha katika Shule ya Msingi ya Mtongwe kwa muda mfupi kabla kuajiriwa na Shule ya Msingi ya Kenya Navy Mtongwe akiwa mwalimu wa kujitolea.

Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ilimpa kazi kwa kandarasi mnamo 2010 na kisha kuifanya ya kudumu mwaka mmoja baadaye papo hapo katika shule ya Kenya Navy Mtongwe.

Wakfu wa Aga Khan umekuwa mstari wa mbele kupiga jeki juhudi zake za kuchangia maendeleo ya jamii, na kuhakikisha kwamba anawapa wanafunzi malezi bora ya kielimu katika eneo zima la Mtongwe tangu Julai 2020.

“Nilianza kuvutiwa na ualimu tangu nikiwa mtoto mdogo. Walimu walikuwa watu wa kuheshimika zaidi katika jamii. Walikuwa wamepiga hatua kubwa kimaendeleo na walitegemewa sana kwa ushauri wa kila aina. Ualimu ilikuwa kazi ya hadhi na ilikuwa tija kujihusisha nayo.”

Kati ya watu waliomhimiza sana Bi Achieng kujitosa katika taaluma ya ualimu ni mjomba wake, Bw Juma, aliyemfundisha katika Shule ya Msingi ya Achego.

Mbali na kufundisha wanafunzi wa chekechea hadi gredi ya tatu katika Shule ya Msingi ya Kenya Navy Mtongwe, Bi Achieng pia ni mwanakwaya stadi katika Kanisa la ACK St John’s Mtongwe. Uimbaji, ukulima na ufugaji ni kazi anazopania kumakinikia zaidi baada ya kustaafu.

Bi Achieng amejaliwa watoto wanne: Handel Offiro Juma, 23, Mozart Eshiteti, 22, Jester Ayieko, 15, na Christine Helidah Were, 9.