Makala

Mwalimu Thomas Wasonga alivyomchangamsha Moi kwa utunzi wa nyimbo

October 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

KABLA ya kufutiliwa mbali na katiba ya sasa mnamo 2010, Sikukuu ya Moi ilikuwa ya kipekee kwa uongozi wa Rais Mstaafu Daniel Moi.

Maadhimisho yake yalitambuliwa na kila mmoja hasa kutokana na nyimbo za kipekee zilizotungwa kuusifia uongozi wake.

Nyimbo hizo ni pamoja na ‘Tawala Kenya’ uliotungwa na Mwalimu Thomas Wasonga, uliomsifia Mzee Moi kama kiongozi shupavu aliyerejesha umoja na utangamano wa kitaifa nchini.

Bw Wasonga alianza kujihusisha na muziki mnamo 1982 akiwa Mombasa kwa nduguye, wakati huo akiongoza kwaya ya Kanisa Katoliki ya St Mary’s.

Hata hivyo, msukumo kutoka kwa Bi Truphena Onyango ambaye alikuwa afisa wa utamaduni serikalini ndio ulimpa ulimfanya kuanza kutunga nyimbo za kizalendo.

“Kanisani, nilikuwa nikishiriki tu katika nyimbo za kumsifu Mungu. Hata hivyo, shinikizo za Bi Onyango zilinifanya kufikiria upya ushauri wake. Ni baada ya hapo ambapo nilitunga wimbo ‘Mkenya Daima’ ambao ndio ulikuwa wa kwanza kwa msururu wa nyimbo za kizalendo ambazo nimetunga,” asema Bw Wasonga. Kufikia sasa, Bw Wasonga ametunga zaidi ya nyimbo 40, ila zile zimenakiliwa na kutumika katika hafla za kitaifa ni 15.

Asema kwamba yu mbioni kuandaa video za nyimbo zote na kuziweka katika jukwaa ambalo Wakenya wote watazipata kwa urahisi.

Lakini, je, alifanikiwa vipi kutambuliwa na Mzee Moi na kujumuishwa kama mtumbuizaji rasmi wa hafla za kitaifa?

Baada ya ushauri wa Bi Otieno, Bw Wasonga aliongoza kwaya yake rasmi kumtumbuiza Mzee Moi katika hafla moja aliyohudhuria Mombasa.

“Wimbo ‘Mkenya Daima’ ulimfurahisha sana Mzee Moi kiasi kwamba aliamka na kuanza kucheza densi nasi,” akasema.

Baada ya Moi kustaafu aliajiriwa rasmi na serikali katika kitengo cha kusimamia utumbuizaji katika hafla za kitaifa za serikali.

Nyimbo zake zingine zinazosifika ni ‘Twajivunia Nchi ya Kenya’, ‘Kenya Nchi Yetu Nzuri,’ ‘Kutunza Mazingira,’ ‘Heko Jamhuri,’ ‘Tushangilie Kenya’ kati ya nyingine nyingi.

Bw Wasonga asema kuwa Rais Mstaafu Moi pia aliwapa shinikizo kutunga nyimbo zaidi, kwani alipenda kutumbuizwa sana.

“Rais Mstaafu Moi alikuwa anapenda muziki sana, hasa wa kizalendo. Mapenzi yake yalitokana na hali kuwa jumbe zake kuu kwa wananchi katika majukwa ya hadhara yalikuwa kuhusu umuhimu za kuzingatia uzalendo,” akasema.

Kulingana naye, mapenzi ya muziki ya Bw Moi yalimfanya kutangamana sana na wanakwaya mbalimbali, hali ambayo pia anataja kuchangia kujumuishwa kwa Somo la Muziki kwa mtaala wa 8-4-4 kabla ya kuondolewa.

Bw Wasonga pia anamsifia Rais Mstaafu Mwai Kibaki, akisema kuwa kinyume na dhana za wengi, pia alipenda sana muziki.

Hata hivyo, anamtaja Rais Uhuru Kenyatta kuwa kiongozi anayependa zaidi kuwazidi watangulizi wake.

Baada ya kuajiriwa rasmi na serikali, Bw Wasonga aliacha rasmi ualimu, akisema kuwa mapenzi yake ya muziki yalizidi taaluma yake.

Kwa sasa, Bw Wasonga ni Naibu Mkurugenzi Msimamizi wa sherehe za kitaifa katika Afisi ya Rais. Ingawa amestaafu katika ushiriki wa moja kwa moja wa hafla za utumbuizaji, lengo lake kuu huwa ni kusimamia taratibu za maandalizi ili kuhakikisha kuwa zinaendelea bila matatizo yoyote.

Wito wake ni kwa asasi husika ni kuwekeza zaidi katika masuala ya kitamaduni, ili kuwawezesha vijana kugundua vipaji vyao kwa kushangia utunzi wa nyimbo za kizalendo.