Makala

Mwana feki alivyorithi mamilioni ya mfanyabiashara

Na BENSON MATHEKA, JOSEPH WANGUI October 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Mnamo Januari 2013, Nathaniel Kibitok Sieley alikuwa akijihusisha na biashara yake ya kilimo cha chai katika eneo la Nandi. Bila kujua, mtu aliyedai kuwa mwanawe alianzisha kesi ya urithi kwa kutumia taarifa za uongo katika Mahakama Kuu ya Nakuru, akilenga kumiliki mali yake akidai kuwa Sieley alikuwa amefariki dunia.

Hata hivyo, Sieley alifariki dunia miezi miwili baadaye, akiwa na hazina ya thamani ya mamilioni ya pesa, iliyojumuisha Sh23.5 milioni katika akaunti yake katika Benki ya Kenya Commercial Bank, tawi la Nandi Hills. “Mwanawe” huyo aliendelea na kesi ya urithi kwa kuzingatia taarifa za uongo za kifo cha Sieley na hatimaye alipata hati ya usimamizi wa mali, iliyothibitishwa na mahakama  Julai 22 2017, na iliyoonekana kusainiwa na Jaji Maureen Odero.

Hati ya usimamizi wa mali ni hati ya kisheria inayotolewa na mahakama kumruhusu mtu kusimamia mali ya marehemu ambaye hakuwa na wasia.

Mtu huyo aliwasilisha hati hiyo benki, na benki ikamkabidhi fedha zote Februari 2019 na ikafunga akaunti hiyo. Wakati huu, familia ya Sieley haikujua lolote kuhusu jambo hilo, ingawa walifungua kesi ya urithi katika Mahakama Kuu ya Eldoret mwaka 2018 na kupata hati ya usimamizi Septemba 28 2018.

Familia hiyo iligundua udanganyifu huo na wizi walipowasilisha hati za mahakama benki ili kuanza kazi zao kama wasimamizi wa mali.

Hii ilisababisha mgogoro wa kisheria kuhusu jukumu la benki kuhifadhi mali ya marehemu, ambao ulimalizika wiki iliyopita pale Jaji John Wananda alipoamuru benki kurejesha akaunti na kurudisha Sh24 milioni zilizotolewa.

Jaji Wananda alisema benki ilikuwa na jukumu la kuangalia maslahi ya akaunti ya marehemu, akisema uhusiano kati ya benki na mteja ni makubaliano ya kisheria na benki inapaswa kutumia “angalifu na ustadi unaofaa” katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Benki haiwezi kuruhusiwa kuwa na uzembe unaoweza kuumiza mteja,” alisema jaji.

Jaji alibainisha kuwa benki ilionyesha uzembe mkubwa kutoa kiasi hicho kikubwa cha fedha bila hata kuomba  stakabadhi au maelezo ya mpokeaji wa pesa, hata kama kwa ajili ya kumbukumbu tu.

Ingawa shahidi wa benki alisema fedha zilitumwa kwenye akaunti inayomilikiwa na mtu huyo katika tawi la benki hilo Nairobi, mahakama haikupata ushahidi wowote unaothibitisha fedha kuhamishwa kutoka akaunti ya Nandi Hills.

Aidha, maelezo kuhusu akaunti ya mtu huyo Nairobi hayakuwahi kufichuliwa wala kuwepo kwa sababu za kushindwa kutoa maelezo hayo.

Pia taarifa za benki zilizotolewa na benki na meneja wake hazikuonyesha kuwepo kwa uhamishaji wowote wa fedha kwa mtu aliyedaiwa kuwa mwana wa marehemu.