Makala

Mwanadada asimulia jinsi alibebwa kwa nguvu na wanaume 7 kuozwa kwa lazima

Na VITALIS KIMUTAI July 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MWANAMKE mmoja alisimulia kwa machozi alivyotekwa na wanaume saba na kuozwa kwa nguvu.

Mary (si jina lake halisi), 18, alikuwa amekamilisha masomo yake ya shule ya upili alipotekwa nyara na wanaume saba kutoka nyumbani kwa wazazi wake huko Lolgorian, Kaunti ya Narok, na kulazimishwa kuolewa na mwanaume asiyemfahamu katika desturi ya kiasili ya jamii ya Wamaasai ambayo bado haijatokomea.

Alitarajiwa kukubali hali hiyo, aanze maisha kama mwanamke wa ndoa, azae watoto na kuwalea bila kuuliza maswali.

Hata hivyo, aligoma kula kwa siku tatu na kudanganya kwamba alikuwa na hitaji la haraka la matibabu, mbinu iliyowadanganya watekaji wake na wakampeleka hospitalini.

Akiwa hospitalini, alipanga mpango wa kutoroka uliomfikisha mikononi mwa polisi, na hatimaye kupata uhuru wake lakini akiwa amejeruhiwa kimwili na kiakili.

“Nilinusurika ndoa ya kulazimishwa baada ya mateso ya saa 72 mikononi mwa wanaume saba, lakini kabla ya hayo, yule niliyepaswa kuolewa naye alitumia nguvu na kuninyang’anya usichana wangu niliokuwa nimeulinda kwa miaka 18,” Mary alisimulia kwa huzuni.

Akidondokwa na machozi, alisimulia Taifa Leo kisa hicho nyumbani kwao Kilgoris, Kaunti ya Narok, umbali mfupi kutoka mahali alikotoroka miaka minane iliyopita.

Mary anakumbuka vyema tukio hilo la kusikitisha lililotokea siku ya Jumatano. Wazazi wake walikuwa sokoni, ndugu yake akaenda kuchunga mifugo, na yeye akabaki akifanya kazi za nyumbani.

“Wanaume saba walifika nyumbani wakiwa vijana, wakasema wanatafuta ng’ombe aliyepotea. Niliwakaribisha kwa maji ya kunywa na kuwaeleza kwamba sikuona ng’ombe yeyote. Hawakumaanisha ng’ombe halisi, walikuwa wakizungumzia mimi,” alikumbuka Mary.

Aliporudi ndani kuweka vikombe, mwanaume mmoja aliagiza wenzake wamkamate na kumvuta kwa nguvu. Mary alipiga kelele, kupambana na kulia, lakini hakufua dafu.

Wanawake na watoto wa kijiji walijaribu kumsaidia lakini walifukuzwa na wale wanaume waliokuwa na fimbo.

“Nilichukuliwa hadi msituni na kisha mwanaume mmoja akatokea, nikaambiwa ndiye atakayenioa. Nilihisi nilikuwa nikiota ndoto mbaya.”

Mary alipambana zaidi alipoonyeshwa mwanaume huyo, lakini walimzingira na kumzuia. Mavazi yake yaliraruliwa, na mmoja akatumwa sokoni kununua nguo mpya ambazo alikataa kuvalia.

Baadaye alipelekwa nyumbani kwa yule kijana aliyekuwa na umri wa miaka mitano zaidi ya umri wake ambako alitarajiwa kuanza maisha ya ndoa.

Anasema alikataa kula kwa siku tatu mfululizo, akinywa maji pekee. Baadaye alidanganya kuwa alikuwa na miadi ya daktari mjini Kisii na alihitaji kufanyiwa uchunguzi wa haraka.

Alifanikiwa kumshawishi yule kijana, ambaye alimpeleka hospitalini. Alipowasili, alimdanganya kuwa daktari alihitaji kumuona peke yake, na ndipo alipomweleza daktari hali halisi na kuomba kutumia simu yake kupigia jamaa aliyekuwa afisa wa polisi.

“Tulipokuwa tukirudi Lolgorian, nilimdanganya kuwa niliona sweta niliyopenda karibu na kituo cha polisi. Tulipofika, nilifanya kana kwamba nafunga kamba ya viatu na nikawapa polisi ishara,” alisema Mary.

Alimpigia kelele mwanaume huyo na kuwaonyesha kwa kidole. Alitambua ulikuwa ni mtego na akakimbia na kutoroka.

Nililelewa katika familia yenye misingi imara ya Kikristo. Nilishangazwa kuona jamii ikiunga mkono uovu huu. Ni huzuni kuwa watu walioniona nikichukuliwa kwa nguvu hawakufanya lolote.”

Baada ya kuokolewa, Mary alipimwa hospitalini na akabainika hakuwa na matatizo ya kiafya. Kisha alijiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), kitivo cha Kisii, ambako alihitimu kwa diploma ya ununuzi mwaka wa 2021.

“Kwa sasa ninafanya kazi na shirika la Kakenya’s Dream nikiwa mtetezi wa haki za watoto na wanawake. Nawasaidia watoto wa shule kwa kuwapatia sodo za hedhi, chupi na sabuni ili waweze kubaki shuleni.”

Dkt Kakenya Ntaiya, mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Kakenya’s Dream, alisema ni jambo la kusikitisha kuwa jamii bado inashikilia mila za kizamani badala ya kuwawezesha wasichana kusoma.

“Jamii haijakubali kikamilifu kuwaelimisha wasichana na kuwawezesha. Kuna woga kuhusu mwanamke aliye huru kifikra. Wasichana wanalazimishwa kuolewa ili kudhibiti uwezo wao.”

“Bado tunawaokoa wasichana dhidi ya tohara na ndoa za kulazimishwa. Tunahitaji juhudi za pamoja kuhakikisha haki za watoto na wanawake zinalindwa,” alisema Dkt Kakenya.

“Wasichana hawa wanaohangaishwa wanahitaji matibabu, usaidizi wa kisaikolojia, na msaada wa kujikwamua kutokana na madhila ya ndoa za kulazimishwa, tohara na mimba za utotoni.”