Makala

Mwanaharakati: Sheria ya Marekebisho kuhusu Matumizi Mabaya ya Kampyuta inatunyima uhuru wa kujieleza

Na WINNIE ONYANDO October 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa vuguvugu la Kenya Moja Coalition, Francis Awino ambaye alikuwa rais wa Bunge la Mwananchi, amejiunga na orodha ya wale waliowasilisha kesi ya kupinga utekelezaji wa Sheria ya Marekebisho kuhusu Matumizi Mabaya ya Kampyuta.

Bw Awino anadai sheria hiyo inahujumu haki ya Wakenya ya kujieleza na kupata habari.

Katika ombi lililowasilishwa katika Mahakama ya Milimani, Bw Awino, ambaye pia ni mwanaharakati anapinga Kifungu cha 27 cha sheria hiyo akisema kinatoa mamlaka makubwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Masuala ya Kompyuta na Uhalifu wa Mitandaoni (NCCCC) kuzima tovuti na mitandao ya kijamii bila idhini ya mahakama.

Kupitia mawakili wake, Bw Awino ameiomba Mahakama kutoa amri za muda za kuizuia serikali na mashirika husika kutekeleza kifungu hicho hadi kesi hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa kikamilifu.

“Kifungu hiki kinaweka vikwazo visivyo na msingi kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari, kwa kutaja kuwa ni kosa kuchapisha taarifa zinazosababisha ‘maumivu ya kihisia’ bila hata kuthibitisha nia ya kufanya hivyo,” alisema Bw Awino.

Rais wa Bunge la Mwananchi Francis Awino akihutubia wanahabari Nairobi. PICHA|WINNIE ONYANDO

Kando na hayo, Bw Awino anasema sheria hiyo ina maelezo yasiyoeleweka vizuri na inaweza kutumiwa vibaya na maafisa wa usalama kuwakandamiza waandishi wa habari, wanablogu na wakosoaji wa serikali.

Mwanaharakati huyo pia anadai kuwa mchakato wa kupitisha marekebisho hayo haukufuata taratibu zinazohitajika, hasa katika suala la ushirikishwaji wa umma.

Hii inafuata kesi iliyowasilishwa na mwimbaji wa nyimbo za Injili na mwanasiasa Reuben Kagame na Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu Nchini (KHRC).

Kulingana na Bw Kagame, kuna hatari kuwa sheria hiyo itatumiwa vibaya na serikali kuhujumu uhuru wa kujieleza, demokrasia na utawala bora.

Oktoba 23, 2025, seneta wa Busia Okiya Omtatah pia kupitia taarifa aliyochapisha Alhamisi katika akaunti yake ya mtandao wa X, alieleza kuwa analenga kupinga sheria tatu miongoni mwa nane iliyotiwa saini Oktoba 15, 2025 na Rais William Ruto.

“Kwanza ni Sheria ya Marekebisho kuhusu Matumizi Mabaya ya Kampyuta inayohujumu uhuru wa Wakenya kujieleza na kupata habari. Inatisha kugeuza Kenya kuwa nchi hatari ambako mitandao ya kijamii inaweza kuzimwa kiholela. Nitawasilisha kesi kortini kupinga sehemu za sheria hii zinazokiuka katiba,” Bw Omtatah akasema.