Makala

Mwanahisabati aliyegeuka mwandishi wa vitabu

January 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA WANDERI KAMAU

JE, unaweza kuiacha taaluma yako uliyoisomea na kujitosa kwenye taaluma jipya usiojua itakakokupeleka?

Kwa barobaro Samuel Kanja, hii ndiyo safari na mkondo wa kimaisha aliyoamua kuchukua

Licha ya kuwa mwanahisabati aliyesoma hadi katika kiwango cha kupata Shahada ya Uzamili, aliamua kujitosa kwenye tasnia ya uandishi wa vitabu na kutoa mashauri jamii kuhusu masuala tofauti ya kimaisha.

Kanja, 35, ni msomi wa kipekee. Alikuwa wembe darasani.

Katika Mtihani wake wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE), Bw Kanja alizoa alama ya ‘A’ (Pointi 83) mnamo 2006 katika Shule ya Upili ya Wavulana ya St Mary’s, iliyo katika Kaunti ya Nyeri.

Baada ya kuupita mtihani wake, aliitwa katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alikosomea Shahada ya Sayansi (Takwimu) na kufuzu mnamo 2012.

Aliamua kurejea darasani 2017 na kusomea Shahada ya Uzamili (Sayansi, Ujasiriamali na Ubunifu) katika chuo chicho hicho.


Mojawapo ya vitabu ambavyo Samuel Kanja ametunga. PICHA|WANDERI KAMAU

Aliajiriwa na mashirika kadhaa ya hadhi kama vile Ernst and Young kama mhasibu, lakini anasema kuwa wito wa kuwa mwandishi na mshauri wa jamii bado ulikuwa ndani yake. Mashirika mengine yaliyomwajiri ni KPMG, Citi Bank, British American Tobacco (BAT) kati ya mengine.

“Licha ya ufanisi wangu mkubwa kimasomo, nilikuwa bado na mwito wa kuandika vitabu vya kuwafaa wanafunzi kuhusu mbinu za kufaulu masomoni mwao na pia kuishauri jamii,” akasema Bw Kanja, kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo Dijitali’.

Kutokana na mwito huo, alianza kualikwa kutoa mihadhara na mashauri katika shule tofauti nchini.

Hata hivyo, alisema aliamua kurejea darasani tena, kusomea taaluma ya ushauri ili kujenga sifa yake kama mashauri wa kitaaluma, anayeweza kutegemewa na jamii bila kuulizwa maswali, au ujuzi wake kutiliwa shaka.

Kutokana na hilo, aliamua kusomea Diploma kuhusu Masuala ya Ushauri katika Taasisi ya Kibiashara na Huduma za Ushauri (KIBCS), jijini Nairobi, kati ya 2019 na 2022.

“Licha ya kuwa darasani, bado nilikuwa nikipata mialiko ya kutoa mashauri katika taasisi mbalimbali—za kielimu na zisizo za kielimu,” akasema.

Bw Kanja aliamua kuacha kazi ya kifahari ya uhasibu katika shirika la Ernst and Young na kuingilia utoaji ushauri kwa asilimia 100.

“Huu ulikuwa mwito wangu. Nilikuwa nimeshafanya maamuzi yangu,” akasema.

Licha ya shughuli nyingi za kimasomo na mialiko ya kutoa mashauri katika taasisi tofauti, aliamua kujitosa kwenye uandishi wa vitabu, ili kujiimarisha na kujiboresha kama mshauri anayetambulika.

Aliandika kitabu cha kwanza ‘Fashioned for Life’ (Aliyeundwa kwa Ajili ya Maisha). Anasema kuwa mapokezi ya kitabu hicho yalikuwa mazuri, hasa miongoni mwa wanafunzi, hali iliyompa motisha kuandika kitabu kingine.

Kitabu chenye mada Fashioned for Life ambacho Samuel Kanja ametunga. PICHA|WANDERI KAMAU

Alifuatiliza kwa kitabu Ultimate Recipe for a Wholesome Student’ (Mwongozo Mahsusi kwa Mwanafunzi Mkamilifu). Kwenye kitabu hicho, Bw Kanja anasema aliangazia mbinu ambazo mwanafunzi anaweza kuzingatia ili kufaulu masomoni na katika maisha yake.

Mapokezi ya vitabu vyake yaliendelea kuwa mazuri. Alipata motisha wa kuandika kitabu kingine ‘The Career Decoder’ (Ufunguo wa Kitaaluma), kinachotoa mwongozo kwa kila mmoja katika jamii kuhusu mbinu za kujikuza na kujiimarisha kitaaluma.

Pia, ameandika kitabu ‘My Values: My Identity (Thamani Yangu: Utambulisho Wangu)—kinachotoa ushauri kwa kila mwanajamii kuhusu njia ya kujifahamu kwa undani.

Kitabu chenye mada The Career Decoder ambacho Samuel Kanja ametunga. PICHA|WANDERI KAMAU

Mwezi huu, Januari 2024, Kanja alizindua kitabu cha tano ‘Money Matters’ (Masuala ya Fedha), kinachotoa mwongozo na ushauri kwa jamii kuhusu masuala muhimu yanayohusu udhibiti na matumizi ya fedha.

“Nilibaini kuwa watu wengi wanakumbwa na changamoto nyingi kwenye udhibiti na matumizi ya pesa zao. Kama mwanahisabati na mtaalamu wa fedha aliyesoma hadi katika kiwango cha Uzamili, sikuwa na ugumu wowote kuandika kitabu hicho, kwani ni mkusanyiko wa mashauri ambayo nimekuwa nikitoa katika majukwaa tofauti kuhusu matumizi ya fedha,” akasema Bw Kanja.

Kitabu chenye mada ‘Ultimate Recipe for a Wholesome Student’ ambacho Samuel Kanja ametunga. PICHA|WANDERI KAMAU

Kwa sasa, Bw Kanja anasema ametoa mashauri katika zaidi ya taasisi 300 na analenga kuendelea kufuata mkondo huo, akishikilia kuwa ndio mwito wake.

Kutokana na ufanisi wa safari yake, amefungua kampuni ya utoaji ushauri inayoitwa Ultimate Excellence Limited, inayotoa huduma tofauti za ushauri wa kimasomo na kijamii kwa tasisi zote.

“Natumia kampuni hii kama jukwaa la kumfikia kila mtu anayenihitaji ili kutoa mwongozo kwake kuhusu masuala tofauti ya kimaisha na kimasomo,” akasema mshauri huyo.

Ushauri wake kwa vijana ni kuchukua muda na kujijua kwa undani, kwani ni kupitia hilo wanaweza kutimiza ndoto zao maishani.