Makala

Mwanajeshi Mwingereza ajitetea akisema alipigwa Kiswahili akajikuta ameoa mke wa pili bila kukusudia

February 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WANDERI KAMAU NA MASHIRIKA

HARUSI ya Kiislamu iliyofanyika miaka miwili iliyopita, imeanza kumsumbua mwanajeshi kutoka Uingereza anayehudumu mjini Nanyuki, ambaye sasa ameshtakiwa kwa kumuoa mwanamke mwingine akiwa bado kwenye ndoa.

Kinaya ni kuwa, mwanajeshi huyo analalamikia hali yake ya kutokifahamu Kiswahili kufanya makosa hayo.

Mnamo Oktoba 2021, Sajenti Noa Dravikula alimwoa Bi Kuki Wason, aliye Mkenya, kwenye harusi ya kufana ya Kiislamu, iitwayo ‘Nikah’.

Kulingana na sheria za Uingereza, mtu anayemwoa mtu aliyeolewa na mtu mwingine huwa kwenye hatari ya  kufungwa gerezani kwa hadi miaka saba au kupigwa faini kali.

Mnamo Februari 19, 2024, upande wa mashtaka nchini Uingereza uliiambia Mahakama ya Kijeshi ya Bulford kwamba Bw Dravikula alimwoa mke wake wa kwanza kwenye kanisa la Methodist mnamo 2011, nchini Fiji.

Wawili hao walianza mchakato wa kutalikiana mnamo Machi 2017, ijapokuwa suala hilo halikuwa limekamilishwa wakati alikuwa akimwoa Bi Watson. Bw Dravikula na mke wake wa kwanza wana mtoto mmoja.

Kiongozi wa mashtaka, Luteni Charlotte Adams, aliiambia mahakama kwamba anaamini uhusiano baina ya Bw Dravikula na mpenziwe ulianza baada yake kutumwa kuhudumu nchini Kenya.

“Alitumwa kuhudumu katika Kambi ya Mafunzo ya Wanajeshi wa Uingereza nchini Kenya, alikoanza uhusiano wa kimapenzi na Bi Kuki Wason. Mnamo Oktoba 29, 2021, hafla ya harusi iitwayo Nikah ilifanyika—ni harusi iliyokuwa halali, inayotambulika kisheria,” akasema.

Upande wa mashtaka pia ulisema harusi hiyo iliendeshwa na afisa mmoja nyumbani kwa mamake mwanamke huyo. Ulisema kwamba kulikuwa na mashahidi wawili.

Hata hivyo, hafla hiyo yote iliendeshwa kwa Kiswahili, lugha ambayo mshtakiwa anasema hakuielewa.

Hali ya mshikemshike ilianza wakati mwanajeshi huyo aliposema alikuwa akipanga kumpeleka mkewe mpya nchini Uingereza. Hata hivyo, wakubwa wake walizua maswali, walipobaini hakuwa amemtaliki mke wake wa kwanza.

Wakati mshtakiwa alijaza fomu za kumpeleka mkewe mpya nchini Uingereza, alisema yeye ni mwanamume aliyemtaliki mke wake wa kwanza, dai ambalo upande wa mashtaka ulikataa kabisa.

Kesi hiyo ya kushangaza inaendelea kusikizwa.