Mwanamke alivyopatwa amefia kwenye tanki la maji ‘alilopanda kuliosha’
SOPHIA WANJIRU NA LABAAN SHABAAN
WAKAZI wa eneo la Kiruga katika Kaunti Ndogo ya Othaya, Nyeri walimtafuta mwenzao Sarah Wairuri kwa siku tano lakini hawakuangalia tanki lao la maji.
Tanki hilo la lita 2500 lilikuwa chanzo cha maji kwa majirani na baadhi ya makanisa mkabala na makazi ya marehemu.
Humo ndani ndimo mlimopatikana mwili wa Bi Wairuri mnamo Januari 18, 2024 baada ya kupotea Januari 13, 2024.
Taarifa hii ilithibitishwa na Naibu Afisa Msimamizi wa Vituo vya Polisi (OCPD) eneo la Othaya Safari Katana.
Ilikisiwa kuwa mwendazake, aliyeopolewa akiwa amefariki, alitumbukia kwenye tanki baada ya stuli kuonekana kando ya tanki hiyo aliyotumia kupanda ili ‘kuliosha.’
Bi Wairuri anatajwa kuwa mwanamke mkakamavu na mkarimu asiyetoza ada ya maji kwa watu waliokuja kuteka maji.
Hata hivyo, anasemekana alikuwa na msongo wa mawazo na alikuwa anatumia tembe za kuganga hali hiyo.
Binamu yake kwa jina Beth, anaambia Taifa Leo kuwa mnamo Januari 13, Sarah alienda kijijini Irindi kumtembelea pacha wake asubuhi kabla ya kurejea nyumbani na kisha kuwatembelea majirani na mwishowe kutoweka.
Alhamisi ya Januari 18, binti yake Beth mwenye umri wa miaka 15 alienda kumtafuta Sarah nyumbani mwake ambapo alikutana na harufu mbaya asijue ilitoka wapi.
Baadaye, kwa msaada wa majirani, waliamua kuchungulia kwenye tanki na kuona mavazi yakielea.
Awali waliotumia maji haya waligundua yalikuwa na povu lakini hawakudhania Bi Sarah alitumbukia humo.
Familia ilitoa taarifa hii kwa kituo cha Polisi cha Kiruga ambapo maafisa wa polisi na makachero walianza kushughulikia suala hilo.
Kitendawili cha kifo hiki hakijateguliwa huku aila yake ikiwa na mashaka sababu wanaamini mwendazake alikuwa na mwili mkubwa kushinda mlango wa tanki hiyo.
Upasuaji wa kuchunguza kiini cha kifo hicho utafanywa Jumatano, Januari 24, 2024.
Itakumbukwa kuwa, mwaka wa 2020, Bi Sarah alisaidiwa na wahisani baada ya kutamba mitandaoni alipoonekana mama masikini mwenye watoto wanane.
Wakfu wa My Brother’s Keeper na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga walimjengea nyumba baada ya kuona hali yake.