Makala

Mwanamke aliyeombewa na mhubiri ‘tata’ ajipa tumaini

March 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

MWANAMKE aliyerekodiwa kwenye video ‘akipungwa pepo’ na mhubiri Danson Gichuhi almaarufu ‘Yohana’ wiki moja iliyopita, hatimaye amejitokeza hadharani.

Mwanamke huyo, aliyejitambulisha tu kama Bi Wanjiru, anasema kwamba matatizo mengi ambayo amekuwa akipitia kwenye ndoa yake ndiyo yalimfanya kutafuta usaidizi wa ‘nabii’ huyo.

Bi Wanjiru alisema aliamua kwenda kutafuta usaidizi baada ya mumewe kuanza kuishi na mwanamke mwingine, ambapo wakati mwingine alikuwa hata akiwachukua watoto wao na kuwapeleka kwa mwanamke huyo.

Kwenye mahojiano na Kameme FM mnamo Jumamosi, Bi Wanjiru alisema kuwa hakufahamu kwamba alikuwa akirekodiwa kwa simu alipokuwa akiombewa na nabii huyo.

Pia, alisema kwamba alikuwa amepoteza fahamu wakati ‘maombi’ hayo yalikuwa yakiendelea.

“Niliamua kutafuta usaidizi wa maombi kutoka kwa mhubiri baada ya kuelezewa kumhusu na rafiki yangu. Rafiki huyo alinishauri niende kwake, kwani alikuwa ameiombea familia yake kuhusu matatizo kadhaa ya kinyumbani waliyokuwa nayo na yakaisha. Hivyo, alinishauri niende kwake, nilipomwelezea changamoto za ndoa nilizokuwa nikipitia,” akasema Bi Wanjiru.

Mwanamke huyo alisema ni mtu wa familia na kwamba ni mchuuzi wa bidhaa rejareja jijini Nairobi.

Bi Wanjiru alisema wakati alipokubali ushauri wa rafikiye, walisafiri hadi jijini Nakuru kukutana na mhubiri huyo.

Anasema alimwitisha Sh3,000 kama ada ya maombi.

“Kusema ukweli, sikuwa na pesa hizo. Rafiki yangu alilipa ada hiyo na akaombewa. Tulirudi Nairobi, huku nikianza kutafuta pesa. Nilifanikiwa kupata Sh2,000. Tuliporudi kwake ili niweze kuombewa, alikubali pesa hizo. Tuliimba nyimbo tano za kumwabudu Mungu, ndipo baadaye akaanza kuniombea,” akasimulia.

Hata hivyo, alisema hakuelezwa taratibu au kanuni ambazo huwa zinafuatwa ili kuombewa.

“Nilipoteza fahamu nilipoanza kuombewa. Sikujua kile kilichokuwa kikiendelea. Hata hivyo, maombi yalipomalizika, niliona kamera kadhaa ambazo zilikuwa zikinirekodi,” akasema.

Waliporudi jijini Nairobi, Bi Wanjiru alisema alishangaa sana alipoitwa na rafiki yake na kuonyeshwa video yake akiombewa na mhubiri huyo, iliyokuwa ikienezwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Nilishangaa sana. Kama watu wale wengine, niliona video hiyo mtandaoni. Sikujua kuwa wakati wa maombi, nilikuwa nikirekodiwa na kwamba video hiyo hatimaye ingewekwa mtandaoni. Nilipompigia simu mhubiri huyo kuhusu suala hilo, alisema hata yeye hakufahamu kuhusu aliyechukua simu yake na kuanza kurekodi,” akasema.

Bi Wanjiru alisema kutokana na msongo wa mawazo uliomkumba, nusura ajitoe uhai hali anayosema pia ingeweka wanawe kwa hatari, japo aliokolewa na wasamaria wema.

Sasa wasamaria wema wameahidi kumsaidia kujijenga upya kimaisha akifurahia hilo kama “hatua muhimu kwangu.”