Makala

Mwanamke aliyetaka kujirusha majini afaulu biashara ya utalii 

April 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA PETER CHANGTOEK

NAOMI Ogutu alipoabiri ndege pamoja na wanawe mwaka 2012, alijipa matumaini kwamba, ifikapo mwaka wa kumi akiishi nchini Amerika, angekuwa mwajiri.

Ndoto yake ilitimia baada ya muda aliokuwa ameahidi kutimiza ndoto hiyo.

Kwa sasa, Naomi anaimiliki kampuni ya kutoa huduma za utalii, ambapo anadokeza kuwa ana wahudumu 1,099, na anaishi ndoto anayoitaja kama ‘Ndoto ya Amerika’.

Kabla ya ndoto yake kutimia, nusra akatize maisha yake kwa kujirusha katika Mto Mississippi kwa sababu ya changamoto za kifamilia.

“Nina watoto watatu. Kifungua mimba wangu ambaye ni msichana, Laura, mwenye umri wa miaka 23, anafanya kazi katika jimbo la New Jersey. Mwanangu wa kiume, Alvin, mwenye umri wa miaka 19, yuko katika mwaka wa kwanza katika chuo cha SUNY Polytechnic Institute, akisomea Uhandisi wa Umekanika. Nicole, mwenye umri wa miaka 17, anaingia chuoni. Ameitwa kujiunga na vyuo 20, lakini ameamua kuchagua kati ya viwili – RPI (Rensselaer Polytechnic Institute) na Embry Riddle Aeronautical University, kusomea masuala ya uhandisi wa ndege,” afichua Naomi.

Anasema kuwa, jambo lililomsukuma kuondoka nchini na kuenda Amerika, ni kutaka familia yake kuwa na maisha bora nay a kutamanika.

“Nilitamani sana sera za shughuli za biashara katika taifa la Amerika. Nilijua kwa uhakika kuwa bidii hulipa na kwamba mazingira ya biashara huko ni mazuri. Mimi ni mtu wa kuchangamka, na niliwahi kumiliki duka la vitabu lililovutia wateja wengi jijini Nairobi, ambapo nilikuwa nikisambaza vitabu katika vyuo na vyuo vikuu,” aeleza.

Anasema kuwa, biashara hiyo ilikuwa nzuri, lakini alikuwa akilazimika kufuatilia sana malipo, kwa sababu alikuwa akizungushwazungushwa na wale waliokuwa wakihusika na utoaji malipo, wakitaka kuhongwa ili kumlipa.

“Nilichoka sana kwa ufisadi na ukosefu wa maadili katika taasisi mbalimbali. Hata nilipowasilisha vitabu mapema, nilikuwa nikilazimika kutoa kitu kidogo. Kusema ukweli, nilichoka, ” asikitika.

Walipowasili nchini Amerika, mambo hayakuwa rahisi mwanzoni. Iliwachukua mwaka mmoja kuzipata stakabadhi muhimu, japo walipata stakabadhi za kufanya kazi kwa miezi sita.

Hawakupewa makao na yeyote, isipokuwa hoteli waliyokodi kwa muda wa wiki moja.

“Nadhani kutokaribishwa na kutoishi na mtu ndilo jambo lililonipa ujasiri na imani kutumia akili yangu kufikiria kusaka maisha hapa Amerika. Nina uhakika kuwa, ningekuwa nimekaribishwa na watu, wangenikatisha matumaini ya kuishi katika jiji la New York City. Lakini kwa juhudi zangu, ninaweza kusema kuwa ninaishi ‘Ndoto yangu ya Amerika,” asema.

Kwa sasa ana umri wa miaka 48.

Alipata kazi ya kwanza katika eneo la 5th Avenue na 53rd Street Manhattan, aliyoifanya kwa miezi mitatu tu. Baadaye, akafanya kazi nyingine kuanzia 2013-2015, kwa kampuni moja kubwa ya stima, katika eneo la New York City.

Alifanya kazi ya tatu katika idara ya hazina, Chuo Kikuu cha New York. Alianzia chini, na akapandishwa hadi kuwa meneja, na pia kuhudumu kwa idara ya ukaguzi. Hata hivyo, alihudumu katika chuo hicho kikuu kwa mwaka mmoja tu.

“Nilifanya kosa moja kubwa 2016, ambalo karibu linifanye kufutwa kazi, lakini nikaamua kujiuzulu, kabla hawajanifuta kazi. Kwa wakati huo, nilikuwa nikipitia msongo wa akili na dhuluma kutoka kwa aliyekuwa mume wangu,” asema, akiongeza kuwa, jambo hilo lilichangia kuathirika kwa kazi yake, ndiposa akaamua kuiacha.

Alikuwa ameathirika na kuhangaika kiasi kwamba, alikuwa ameamua kujiua. Alilichukua gari na kuliendesha katika barabara ya I-95 kuelekea Pittsburgh, ili kumwona rafiki yake mmoja.

“Nilikuwa nikitamani nigongwe na lori. Ilikuwa vibaya! Niliokolewa na dereva wa lori, nilipokuwa nimeketi kando ya Mto Mississippi katika nyanda za juu kabisa. Nilikuwa nikitaka kujitosa majini lakini alikua mtu alinishika mkono, na kunipeleka katika mkahawa wa Wendy’s, akaninunulia chakula cha mchana na kuniruhusu nilie na kumwambia kila kitu.

Aliniandikia nambari yake ya simu kwa karatasi lakini nikaitupa,” asema, akiongeza kuwa, alikuwa na haya ya kumwona baadaye.

Naomi akaanza kuwaza kuhusu siku walipowasili katika uwanja wa ndege wa JKF alasiri, na kulikuwa na baridi kali.

“Nilijua kuwa New York ni nyumbani. Jiji hili la kupendeza litanisaidia kutimiza ndoto yangu na siendi mahali popote. New York ilikuwa kwa damu yangu. Mawazo yangu yalikuwa kuhusu New York.”

Wimbo wa Alicia Keys – New York, ukawa unaimba ukijirudiarudia akilini mwake. Ni wimbo uliompa matumaini.

Wazo la biashara likamjia akiwa kando ya Mto Mississippi alikokuwa akitaka kujirusha. Alirudi New York akiwa amefanya uamuzi. “Nikiwa New York, nilikuwa nikisafiri kwa Uber. Siku moja, dereva wangu wa Uber anayeitwa Famara kutoka Senegal akanipeleka nyumbani. Tuliongea mambo mengi, na akaniamba kuwa, biashara ya Uber ni nzuri.”

Dereva huyo alimjuza kuwa, wao walikuwa wakiunda pesa kwa biashara hiyo, bila kusumbuka akilini. “Alinielezea kuhusu Cabbie Academy, na 2017, tayari nilikuwa nimekuwa dereva nikiendesha Uber katika New York City,” adokeza.

Baada ya kupata leseni na stakabadhi muhimu za usajili kutoka kwa tasisi husika, alianza kuendesha teksi ya Uber katika maeneo ya Manhattan, Brooklyn, Queens, The Bronx and Staten Island.

Mwaka 2018, alianzisha kampuni yake, na mwaka 2020 akaisajili kama S-Corporation Naomi Cars NYC, na ana afisi katika eneo la West 57th Street, Midtown Manhattan, NYC.

Ogutu alianza kuwatangazia wateja wake wa Uber kuhusu  huduma ya kutalii maeneo tofauti tofauti. “Nilipokutana na mteja, nilikuwa nikimpa kadi yangu ya kazi, ili ajue kuwa mimi nipo tayari kuwapeleka kutalii maeneo ya kuvutia katika New York City.

Kwa kweli Mungu hamwachi mja wake. Anaishi maisha anayotaja kama ‘Ndoto ya Amerika’ na amewaajiri watu zaidi ya 1,099.