Mwanamke apata mtoto aliyepotea siku 90 zilizopita
MWANAMKE ambaye mtoto wake aliibwa miezi mitatu iliyopita katika Kaunti ya Nakuru hatimaye amejawa na furaha baada ya kumpata mtoto huyo.
Baby Maya Kerubo alipotea siku 90 zilizopita wakati ambapo alikuwa na watoto wanne wengine katika mtaa wa Rhonda, eneobunge la Nakuru Mashariki. Mshukiwa huyo aliwahadaa kwa soda na smoki kabla kutoweka naye.
Mtoto huyo alipatikana katika nyumba moja ya kukodisha kwenye mtaa wa Maili Kumi, eneobunge la Bahati na mshukiwa akanyakwa na polisi.
Kwa mujibu wa nyanyake Lilian Moraa, alipokea simu mnamo Januari 8 kutoka kwa mtu ambaye alimsaili kuhusu kutoweka mjukuu wake. Aliyempigia alimuuliza kuhusu lini mtoto alitoweka, kama amepatikana pamoja na maelezo mengine ya kibinafsi.
“Aliniuliza kuhusu maumbile yake, umri wake na masuala mengine. Baadaye nilikuja nikagundua kuwa alikuwa mwanamke mwenye nyumba ambako aliyeniibia mtoto alikuwa akiishi. Nyumba hizo zilikuw katika mtaa wa Maili Kumi, Kaunti ndogo ya Bahati,” Bi Moraa akasema.
Landilodi huyo alifichua kuwa mpangaji wake hakuwa na mtoto kwa kipindi ambacho ameishi kwenye nyumba yake japo alikuwa ameolewa. Alionekana na mtoto huyo mnamo Oktoba mwaka jana na akasema ni wake.
“Sikumwaamini kwa sababu sikujua alikuwa akilenga nini. Aliniuliza nimtumie picha ya mjukuu wangu nikafanya hivyo, kisha akanitumia picha ya mjukuu wangu. Baada ya kuthibitisha kuwa huyo alikuwa mjukuu wangu ndipo tuliamua nay kuwafahamisha polisi ili mshukiwa akamatwe,” akaongeza Bi Moraa.
Baadaye, mshukiwa huyo alinyakwa kisha akazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kaptembwa. Bi Moraa kisha alielekea katika Hospitali ya Nakuru ambapo mwanawe Maureen Gesare alijifungua mjukuu wake huyo na akapewa barua ya kuthibitisha kuwa huyo alikuwa mjukuu wake.
Kituoni wawili hao waliulizwa maelezo ya mtoto huyo na iwapo alikuwa na alama aliyozaliwa nayo ya kumtambua.
“Tulitoa stakabadhi hitajika, tukawapa maelezo kisha mtoto akapelekwa hospitali kubaini iwapo alikuwa sawa kiafya. Baada ya hapo, tulipewa mtoto na kutamatisha miezi mitatu ya huzuni na kusaka mtoto,” akasema Bi Moraa.
Mshukiwa huyo alikamatwa na akawaeleza polisi kuwa alikuwa amekaa kwenye ndoa kwa miaka mingi bila mtoto ndiposa akaamua kumuiba mtoto huyo.
Alisema alikuwa na shinikizo kutoka kwa mumewe ili apate mtoto na alimhadaa mume huyo ambaye hakuwa nyumbani kwa kipindi kirefu kuwa alikuwa na ujauzito na alijifungua mtoto.
Bi Gesare alisema kuwa ameandamwa na msongo wa mawazo kwa siku hizo 90. Maya alisherehekea siku ya kuzaliwa mnamo Januari 8 na japo hakuwa amepatikana, Bi Gesare na wanafamilia wengine waliandaa sherehe na hata kukata keti.
Wakati wa hafla hiyo familia yake iliandaa maombi spesheli ili apatikane na ni siku hiyo hiyo ndipo nyanyake alipokea simu kisha keshowe wakampata.
“Miezi hii mitatu haijakuwa rahisi kwa sababu hata baadhi ya majirani walikuwa wameanza kueneza habari feki kuwa nilimuuza mtoto wangu. Nimefurahi kuwa sasa nimempata,” akaongeza Bi Gesare.