Mwanamke hali mahututi hospitalini, alipigwa na mume wakizozania Sh200
MWANAMKE mwenye umri wa miaka 38 anapokea matibabu katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha, kaunti ya Nakuru baada ya kujeruhiwa vibaya sana na mumewe.
Bi Rose Wanja anasimulia kuwa mume wake alirudi nyumbani jioni ya Jumatatu akiwa mlevi na kumtuhumu kwa kuiba Sh200 aliyoacha nyumbani.
Hapo ndipo mume alimpiga mfululizo kwa kipande cha chuma katika chumba kilichokuwa kimefungwa.
Licha ya majirani kujaribu kuingilia kati, Wanja aliokolewa tu wakati mpwa wake aliporipoti kisa hicho kwa polisi siku mbili baadaye ambapo mume wake alikamatwa.
Wanja, mama wa watoto watatu, alipata majeraha usoni na miguuni, na kuvunjika fupanyonga.
Sasa, Bi Wanja ana majuto juu ya ndoa yake ya miaka 22, ambayo imekumbwa na unyanyasaji wa kimwili mara kwa mara, hususan kufuatia kisa cha hivi majuzi ambacho kiliweka maisha yake katika hatari.
“Mume wangu alitumikia kifungo cha miaka mitatu jela katika gereza la Naivasha GK baada ya kumpiga na kumuua mtoto wetu wa miezi miwili kwa fimbo miaka tisa iliyopita katika kisa sawa,” alikumbuka Wanja.
Wanja anasisitiza kuwa mumewe, ambaye tangu wakati huo amekamatwa, anafaa kukabiliwa kisheria ili iwe funzo kwa wengine.
Kulingana na Benjamin Mwaura, Naibu Muuguzi Mkuu katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha, Bi Wanja alilazwa akiwa na majeraha makubwa usoni, miguuni, shingoni na kwenye fupanyonga.
Ingawa hali yake inaonekana kuimarika, Bw Mwaura alisema bado hawezi kutembea kutokana na kuvunjika kwa fupanyonga akibainisha kuwa hali hiyo inaweza kuchukua miezi kadhaa kupona.
Visa vingi
Bw Mwaura alifunguka kuwa hospitali hiyo inaendelea kushughulikia visa vingi vya unyanyasaji wa kijinsia, akiangazia kisa cha hivi majuzi ambapo mwanamke alichomwa kwa maji moto na mumewe.
John Kinuthia, Mratibu wa Kundi la Kuangazia Unyanyasaji wa Kijinsia Naivasha, alisema kuwa Bi Wanja amevumilia maumivu makali kutokana na unyanyasaji wa miaka mingi, na hivyo kusababisha tukio hili la kuhatarisha maisha yake.
Bw Kinuthia amesema kikundi chake kitampa Wanja makazi salama na usaidizi wa kisaikolojia ili kumsaidia kupona kutokana na kiwewe na majeraha.
Amefichua kuwa ana wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa visa vya unyanyasaji wa kijinsia, ambavyo mara nyingi vinahusishwa na masuala ya afya ya akili na matatizo ya kiuchumi ambayo familia zinakabiliwa nayo.
“Tumeshuhudia ongezeko la unyanyasaji dhidi ya wanawake Naivasha, haswa katika maeneo ya Kabati, Kinamba, Karati, na Mai Mahiu,” Kinuthia alisema.
Alipongeza jitihada za polisi na mahakama katika kushughulikia kwa haraka kesi za udhalilishaji na ukatili huku akiwataka wahanga kuripoti matukio hayo kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe haraka.
Kulingana na Utafiti wa Kenya Democratic Health Survey, 2022, zaidi ya asilimia 31 ya wanawake jijini Nakuru wenye umri wa kati ya miaka 15 na 49 ambao wameolewa au wana wapenzi wa karibu wamekabiliwa na unyanyasaji wa kimwili, kingono, na kihisia kutoka kwa wapenzi wao.
Ripoti hiyo ilifichua kuwa asilimia 24 ya wanawake katika Kaunti ya Nakuru wamekumbana na ukatili wa kimwili tangu wakiwa na umri wa miaka 15.
Kitaifa, takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya wanawake walio kwenye ndoa wamekumbana na ukatili wa kimwili huku mamia ya wanawake wakiuawa zaidi na wapenzi wao.
Serikali imejitolea kukomesha ukatili wa kijinsia (GBV) ifikapo mwaka 2026 na ingawa sheria kadhaa zimetungwa kushughulikia chanzo cha matukio hayo, visa vinaendelea kuripotiwa kila siku hasa kwa wanawake na wasichana wadogo ambao wamekuwa wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia.
Serikali kwa kushirikiana na mashirika ya kibinafsi pia imewezesha uanzishwaji wa madawati ya kijinsia katika vituo vya polisi kote nchini ambapo wahasiriwa wa ukatili huripoti matukio haya kabla hayajasababisha vifo.
Mintarafu hii, wahusika wanaendelea kutoa wito wa kuwepo kwa michango ya wadau mbalimbali ambao unahusisha watu wote katika jamii, mashirika ya kijamii na mashirika ya usalama.