MWANAMKE MWELEDI: Anathamini na kutambua umuhimu wa sayansi kwa ajili ya kufanya dunia pahala salama
Na PAULINE ONGAJI
ALIPOKUWA anakua, Prof Judy Wakhungu alitambua kwamba alipenda sayansi.
Mwaka wa 2013 aliteuliwa katika mojawapo ya nyadhifa za haiba ya juu nchini alipowajibishwa awe Waziri wa Mazingira, Maji na Maliasili.
Kabla ya hapo, alikuwa amethibitisha uwezo wake wa kusimamia majukumu makubwa.
Alikuwa mwanajiolojia wa kwanza wa kike katika Wizara ya kawi na ustawi wa maeneo ambapo majukumu yake yalihusisha kutafiti nishati inayozalishwa na kuhifadhiwa chini ya ardhi (geothermal energy) katika eneo la bonde la ufa. Alikuwa mwanajiolojia wa kwanza wa kike katika shirika la kitaifa la kusimamia mafuta (NOCK).
Nyanyake alimhimiza kufuata ndoto yake na kutia bidii endapo alitaka kuwa msimamizi wa mambo. Mbali na nyanyake, kichocheo chake Prof Wakhungu kinatokana na kwamba anatoka katika familia iliyojaa vigezo.
Kwa mfano, yeye ni mpwa wa aliyekuwa Makamu wa Rais Moody Awori na marehemu Profesa Nelson Awori, daktari wa upasuaji na mtaalamu wa kwanza wa figo nchini.
Aidha, mamake alikuwa msimamizi mkuu wa Benki ya Kenya Reinsurance and Consolidated.
Kutokana na vigezo hivi, tokea umri mdogo, Prof Wakhungu alijitahidi kwenda kinyume na dhana potovu katika harakati za kutaka kuwa na ushawishi duniani.
Ni akiwa katika shule ya upili ambapo alianza kuvutiwa na masuala ya petroli na nishati, na hivyo akaamua kusomea jiolojia.
Kutokana na bidii aliyokuwa nayo, aliunda mpango wa miaka kumi uliohusisha kusomea shahada ya uzamifu na kufunza katika chuo kikuu ambapo aliafikia yote.
Baada ya kukamilisha shule ya upili, alijiunga na Chuo Kikuu cha St Lawrence University jijini New York, Amerika, na kusomea shahada ya digrii katika sayansi na jiolojia.
Mwaka wa 1986 alipokuwa akifanya kazi katika shirika la NOCK, aliendeleza masmomo yake nchini Canada ambapo alihitimu na shahada ya uzamili katika sayansi na jiolojia.
Prof Wakhungu alirejea nchini na kuhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Alikuwa mwanamke wa kwanza kujiunga na Idara ya jiolojia chuoni humo.
Mwaka wa 1993, Bi Wakhungu alipokea shahada yake ya uzamifu katika masuala ya usimamizi wa rasilimali za nishati. Kutokana na jitihada na bidii yake, Bi Wakhungu amepokea tajriba kuu katika taaluma hii.
Kabla ya kuchukua wadhifa wake kama waziri, alikuwa mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya African Centre for Technology Studies (ACTS). Aidha, alihudumu kama profesa msaidizi wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania State University, na mkurugenzi wa chama cha wanawake katika fani ya sayansi (Women in the Sciences).