MWANAMKE MWELEDI: Alenga kudumisha haki, usawa na amani katika jamii
Na KEYB
WAHU Kaara ni mwanaharakati wa masuala ya kijamii, mkufunzi katika masuala ya ubinafsishaji na kijinsia.
Yeye ni mmoja wa waasisi wa Mfumo wa Kitaifa wa Nafuu ya Madeni (KENDREN), shirika linalohusika na utafiti na uchanganuzi wa sera.
Shirika hili pia limechukua nafasi ya ushauri katika serikali kuhusu masuala ya fedha ya umma, msaada na madeni ya wa kigeni. Aidha linahusika katika masuala ya kuendesha shughuli za Kenya kama sehemu ya Jubilee 2000 Debt Cancellation Campaign, kampeni ya kushinikiza kutupiliwa mbali madeni.
Ari yake Bi Kaara katika masuala ya umuhimu wa kitaifa ilianza katika miaka ya sabini alipojifunza kuhusu masuala ya kikomunisti na maadili ya haki na usawa, alipokuwa akisomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Baada ya hapo alienda kufunza Historia na Kiswahili katika shule mbalimbali kabla ya baadaye kuwa mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya Nginda ambapo alifanya jitihada za kukuza umoja miongoni mwa wanafunzi ili kurekebisha utovu wa nidhamu katika jamii.
Kutokana na hatua kali ya serikali dhidi ya upinzani katika miaka ya themanini, mumewe alitoroka nchini huku baadhi ya marafiki na jamaa zake wakitiwa nguvuni. Alishushwa madaraka kama mwalimu mkuu na kupelekwa kufunza katika shule ya upili ya wasichana ya Ngara Girls jijini Nairobi.
Katika miaka ya tisini, pamoja na mwanaharakati mwenzake Njeri Kabeberi na marehemu Profesa Wangari Maathai, walikuwa miongoni mwa wanawake waliosusia chakula kama mbinu ya kushinikiza hatua ya kuachiliwa kwa wafungwa wa siasa. Wakati huu alifanya utafiti mwingi katika masuala ya kilimo, HIV/AIDS na uhusiano wa kijinsia.
Mwaka wa 1995 alihitimu kutoka taasisi ya Karolinska Institute nchini Uswidi ambapo alihitimu na shahada ya uzamifu katika Afya ya Umma. Miaka michache baadaye aliacha kazi ya ualimu na kuanza kujihusisha na uanaharakati wa kisiasa, ambapo mwaka wa 1999 alisaidia kuanzisha KENDREN.
Mwaka wa 2004, Bi Kaara alitawazwa kama mratibu wa UN Millennium Development Goals, suala lililotokana na huduma yake ya uanaharakati, ushirika na KENDREN. Alihudumu katika nafasi hii hadi mwaka wa 2006.
Alishiriki katika mabaraza mengi ya uundaji sera katika masuala ya madeni, ubaguzi wa rangi, amani, na masuala ya kijinsia hapa nchini na kimataifa ikiwa ni pamoja na kongamano la G8 nchini Italia mwaka wa 2001 na mpango wa Women Peacemakers nchini Amerika, mwaka wa 2011.
Mwaka wa 2005, alishirikiana na Rais wa Brazil wakati huo, Lula da Silva, kuzindua mwito wa kukabiliana na umaskini (GCAP), ambapo hadi wa leo ndilo jukwaa kubwa zaidi linalounganisha raia dhidi ya umaskini.
Hii leo, anahusika katika miradi kama vile African Social Forum, Action Aid na Coalition for Peace in Africa (COPA), bali na majukumu yake kama mkurugenzi mtendaji wa KENDREN. Aidha, amekuwa akiandika kuhusiana na masuala ya kutupiliwa mbali madeni na haki za wanawake. Pia yeye huzungumza na kutoa mihadhara ya umma kwa serikali na taasisi mbalimbali ulimwenguni kuhusiana na umma ya jamii.
Kazi yake imemfanya kutambuliwa katika viwango mbalimbali. Mwaka wa 2005 alikuwa mmoja wa wanawake 1,000 walioteuliwa kupokea tuzo ya amani ya Nobel, na alitajwa kama mwanachama wa Dame Nita Barrow katika taasisi ya Ontario Institute for Studies in Education nchini Canada, mwaka wa 2008.
Mwaka wa 2009 alipewa tuzo ya kibinadamu ya Project Concern Global Humanitarian. Mwaka wa 2011 alitambuliwa kama mwanamke mleta amani. Mwaka wa 2012 alitajwa kama mmoja wa wanawake 150 jasiri na jarida la Newsweek Magazine, pamoja na watu wengine wenye ushawishi kama vile Oprah Winfrey na Hillary Clinton.
Aliwahi wania nyadhifa katika serikali ya Kenya mara mbili bila mafanikio. Hata hivyo, mwanaharakati huyu ambaye alijifunza salamu kutoka kwa jamii zote 42 kama mbinu ya kukuza umoja nchini, ana imani kwamba Kenya itaendelea kufanikiwa katika siku zijazo na anajikaza kuhakikisha kwamba anaafikia ndoto hii.