• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
MWANAMKE MWELEDI: Alitikisa riadha akibeba Golden League Jackpot

MWANAMKE MWELEDI: Alitikisa riadha akibeba Golden League Jackpot

Na KEYB

YEYE ni mmoja wa wanawake wachanga zaidi kuwahi kuishindia Kenya nishani ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki. Sio hayo tu, Pamela Jelimo aliingia vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa mwanamke wa kwanza Mkenya kushinda taji la Golden League Jackpot, na hivyo kujishindia mamilioni ya pesa.

Isitoshe, Bi Jelimo anafurahia pia kuwahi kushikilia rekodi kadha wa kadha za mbio, hapa nchini na kimataifa.

Kabla ya kushiriki katika michezo ya Olimpiki, alikuwa amekimbia mbio kadhaa na kuvunja rekodi kadha wa kadha. Kwa mfano aliwahi kushikilia rekodi ya duniani ya mbio za mita 800 kwa upande wa vijana, vile vile ile ya Afrika kwa upande wa watu wazima.

Bi Jelimo alizaliwa Desemba 5, 1989 katika kijiji cha Kiptamok Kaunti ya Nandi, eneo la Rift Valley. Kipaji chake cha muziki kilianza kuonekana akiwa angali mdogo huku akichochewa na mamake, Esther Cheptoo Keter ambaye pia alikuwa mkimbiaji aliyebobea katika mbio za mita za 200 na 400.

Alianza kukimbia rasmi mwaka wa 2003, wakati huo akiwa na miaka 13 pekee. Wakati huu alianza kujiundia jina huku akishinda mataji kadha wa kadha akiwa shuleni katika mbio za mita 100, 200, 400, 800, na 400 kuruka viunzi miongoni mwa vitengo vingine.

Kutokana na matatizo ya kifedha, ili kuendelea na masomo, Bi Jelimo alilazimika kuuza maziwa kutoka kwa ng’ombe nyumbani kwao ili kulipa karo. Wakati huo huo, mwalimu wake mkuu alimfadhili kwa kumnunulia mavazi na viatu vya kukimbia ili kumwezesha kuhudhuria kituo cha mafunzo ya kukimbia. Kufikia mwaka wa 2004, Bi Jelimo alikuwa amefikia kiwango cha mkoa katika mashindano ya mbio za mita 400.

Juni mwaka wa 2007 alimaliza wa tano katika mbio za mita 400 katika mashindano ya kitaifa. Alizidi kuimarika katika mbio hizi na hata kushinda nishani ya dhahabu katika mbio za mita 400 kwenye mashindano ya African Junior Championships na kuvunja rekodi ya kitaifa katika mbio za mita 200.

Ni ufanisi uliomfurahisha mwanariadha huyu lakini mkufunzi wake mpya Zaid Kipkemboi Aziz alipendekeza abadilishe na kuanza kukimbia mbio za mita 800.

Wakati huu alianza kufanya kazi na kikosi cha polisi cha Kenya ambapo pia alikuwa akifanya mazoezi na mwanariadha Mkenya mwingine Janeth Jepkosgei. Bi Jelimo alikimbia mbio za mita 800 kwa mara ya kwanza Aprili 19, 2008 katika majaribio ya kitaifa kuiwakilisha Kenya katika mashindano ya Afrika.

Tokea hapo, ufanisi wake katika riadha ulionekana huku akijishindia nishani katika mbio mbali mbali. Hasa nyota yake iling’aa Agosti 18, 2008 aliposhinda nishani ya dhahabu katika mbio za mita 800 kwenye michezo ya Olimpiki jijini Beijing, Uchina.

Ni ushupavu huu uliomfanya kuorodheshwa miongoni mwa wanariadha wa kike waliogombea taji la mwanariadha wa kike wa mwaka wa Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF), kando ya Yelena Isinbayeva wa Urusi na Tirunesh Dibaba wa Ethiopia, taji ambalo Isinbayeva alishinda.

Mkenya Pamela Jelimo baada ya kukamilisha mbio za mita 800 awamu ya nusu-fainali mashindano ya Olimpiki Agosti 9, 2012, London. Picha/ AFP

Hata hivyo, Bi Jelimo hakuambulia patupu mwaka wa 2008 alijishindia tuzo ya IAAF Revelation of the Year Award na mwanaspoti wa kike wa mwaka hapa nchini.

Kati ya mwaka wa 2009 na 2011, matokeo ya mwanariadha huyu yalirudi chini kutokana na changamoto mbali mbali alizokumbana nazo uwanjani na hasa kutokana na majeraha.

Lakini hayo hayakuzima moto wake wa riadha kwani mwaka wa 2012 alirejea kwa kishindo na kumaliza wa pili katika mbio za ukumbini zilizoandaliwa Lievin, Ufaransa huku akitwaa nishani ya dhahabu katika mashindano ya ukumbini duniani ya mwaka wa 2012 yaliyoandaliwa jijini Istanbul, Uturuki.

Mwaka wa 2017, Jelimo alijishindia nishani ya shaba katika michezo ya Olimpiki ya 2012 jijini London ambapo awali alikuwa amemaliza wa nne, lakini baadaye akatuzwa ushindi wa mwanariadha Mariya Savinova-Farnosova wa Urusi ulipotupiliwa mbali baada ya kubainika kwamba alikuwa akitumia pufya.

Japo uwepo wake katika ulingo wa riadha kidogo umerudi chini, Haina shaka kwamba katika muda mfupi ambao Bi Jelimo alishiriki vilivyo katika ulingo wa riadha, alijiundia jina na kujitambulisha vilivyo.

You can share this post!

DAU LA MAISHA: Mwenge wa haki za wasichana na wanawake...

SHANGAZI AKUJIBU: Wakwe zangu wananichukia ajabu lakini...

adminleo