MWANAMKE MWELEDI: Aliwahi kuvaa taji la malkia wa masumbwi
Na KEYB
ALITAMBULISHA sio tu Kenya bali bara la Afrika katika ulimwengu wa masumbwi kwa upande wa akina dada.
Japo huenda miongoni mwa wengi hatambuliki, ustadi wake Conjestina Achieng katika ulimwengu wa ndondi ni wa kipekee, suala ambalo wakati mmoja lilimfanya kupewa jina “Hands of Stone”.
Yeye ni mwanamke wa kwanza wa Kiafrika kushikilia taji la masumbwi la kimataifa la International Boxing Federation (WIBF) middleweight.
Bi Achieng ametambulika kwa kuwaangusha wanandondi mahiri humu nchini na nje, miongoni mwao Zarika Njeri, Jane Kavulani wa Uganda, Monica Mwakasanga kutoka Tanzania na Guillermina Fernandez wa Argentina.
Ni ustadi huu uliomfanya wakati mmoja kuorodheshwa wa tano miongoni mwa wanamasumbwi stadi wa kike duniani.
Katika safari yake, anajivunia kushinda mataji mengine kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na World Boxing Council middleweight, taji aliloshinda mara mbili, vile vile mataji ya World Boxing Federation, Global Boxing Union na World Boxing International Federation middleweight.
Bi Achieng alizaliwa Oktoba 20, 1977, katika kijiji cha Umiru, Kaunti ya Siaya, wa tano katika familia ya watoto kumi.
Kiu yake ya kutaka kujihusisha na ndondi ilianza akiwa na miaka tisa pekee, wakati huo kama mwanafunzi wa shule ya msingi ya St. Jesus Primary School, Yala.
Alijitosa ulingoni kwa mara ya kwanza mwaka wa 2000 baada ya kuhitimu katika viwango kadha vya mchezo wa soka mtaani Makongeni, Nairobi huku kakake, Joseph Kusimba, ambaye wakati huo alikuwa mwanachama wa kikosi cha kitaifa cha wanamasumbwi akichochea uamuzi wake wa kujitosa katika mchezo huu.
Kakake ndiye alimsaidia kupiga msasa ujuzi wake wa ndondi na hata kumsaidia kubadilisha mawazo kutoka kuwa mwanasoka, hadi mwanamasumbwi.
Baadaye alifanya mazoezi kwa mwezi mmoja kabla ya kupata pigano lake la kwanza kama mwanamasumbwi asiye wa kulipwa. Huu ulikuwa mwanzo wa safari kwani ilimbidi kushiriki katika mechi kadha bila malipo kabla ya hatimaye Juni 8, 2002, kujitosa ulingoni, wakati huu kwa malipo.
Pigano hili lilifuatiwa na mechi zingine kadha za kulipwa nchini na ng’ambo, na katika harakati hizo kujiundia jina hapa Kenya na mbali. Lakini licha ya ufanisi wake, Bi Achieng amekuwa akikumbwa na matatizo ya kifedha, suala ambalo hatimaye liliathiri mazoezi yake, na matokeo yake ulingoni.
Mbali na masaibu hayo, mambo yalizidi kuwa mabaya baada ya kukumbwa na matatizo ya kiakili, suala lililomfanya wakati mmoja kupelekwa katika hospitali ya kiakili ya Mathari.
Upeo wa matatizo yake ulidhihirika Januari 2011, babake alipolazimika kujitokeza na kuomba msaada wa kumpeleka bingwa huyu hospitalini. Septemba 2012 hadithi kuhusu masaibu yaliyokuwa yakimkumba ilipeperushwa na mojawapo ya vituo vya televisheni nchini, ambapo ripoti ya kimatibabu ilithibitisha kwamba kwa kweli alikuwa na matatizo ya kiakili.
Lakini licha ya kukumbwa na matatizo ya kiafya na ya kifedha kwa muda mrefu, Bi Achieng anatumai kurejea ulingoni na kung’aa sawa na alivyofanya, katika enzi ambapo aliiweka Kenya kwenye ramani ya ndondi ya akina dada.