MWANAMKE MWELEDI: Amejiundia jina katika masuala ya diplomasia
Na KEYB
KWA miaka, jina lake limekuwa likihusishwa na masuala ya diplomasia huku akijivunia tajriba ya takriban miongo mitatu katika nyanja hii.
Balozi Amina Mohamed ni mmoja wa wanawake ambao wamejiundia jina katika masuala ya kidiplomasia humu nchini huku huduma yake ya hivi majuzi katika uga huu ikihusisha wadhifa wake kama Waziri wa Mashauri ya Kigeni kati ya Aprili 2013 na Januari 2018.
Licha ya kuhusika katika masuala ya mashauri ya kigeni kwa miaka, mwaka wa 2018 alibadili mkondo alipoteuliwa katika Wizara ya Elimu. Machi 2019, alibadili mkondo tena na kupelekwa katika Wizara ya Michezo, Utamaduni na Itikadi.
Balozi Mohamed alipanda na kufikia viwango mbali mbali alipotawazwa kama mshauri wa kisheria katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni mwaka wa 1986, baada ya kuhitimu na shahada ya sheria linganishi na shahada ya uzamifu katika masuala ya sheria ya kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Kiev.
Mwanadiplomasia huyu mwenye ufasaha katika lugha ya Kirusi alipanda na kuwa mshauri wa kisheria katika ujumbe wa Kenyan katika Umoja wa Mataifa jijini Geneva, UswiSi, vilevile katika ujumbe wa Kenya katika Baraza la Usalama jijini New York.
Kutokana na ufahamu wake katika fani hii, haikuwashangaza wengi alipotawazwa kama mwakilishi wa kudumu katika Umoja wa Mataifa na Hayati Rais Moi, nafasi aliyohudumu kwa miaka sita kuanzia mwaka wa 2000. Mwaka wa 2002 Balozi Mohamed aliandikisha vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa mwanamke na Mwafrika wa kwanza kusimamia Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.
Aidha, mwaka wa 2005 alikuwa mwanamke wa kwanza kusimamia Baraza kuu la Shirika la Kimataifa la Biashara.
Katika hatamu ya Rais Mwai Kibaki, alihudumu kama Katibu wa Kudumu, Wizara ya Haki, Mshikamano wa kitaifa na masuala ya Katiba kwa miaka mitatu tangu mwaka wa 2008. Katika kipindi cha huduma yake, Balozi Mohamed alihusika pakubwa katika shughuli zilizochochea uzinduzi rasmi wa Katiba Mpya mwaka wa 2010, kama mbinu ya kurejesha hali ya kawaida baada ya ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2008.
Kati ya mwaka wa 2010 na 2011 alihudumu kama Rais wa Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu uhalifu wa kimataifa, jijini Vienna.
Baadaye, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alimtawaza katika wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa Mpango wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Mazingira mwaka wa 2011, na kumfanya Mkenya mwenye mamlaka makuu katika shirika la Umoja wa Mataifa. Hii ilikuwa kabla ya uteuzi wa Mukhisa Kituyi katika afisi ya Katibu Mkuu wa Kongamano la Umoja wa Mataifa katika masuala ya Kibiashara na Ustawi (UNCTAD).
Uwakilishi wa Balozi Mohamed katika nafasi hizi uliiletea Kenya heshima, vile vile uteuzi wake katika mashirika ya kimataifa vilimfanya kupokea tuzo ya Chief of the Burning Spear (CBS).
Alithibitisha uwezo wake kwa mara nyingine alipoongoza ujumbe wa Muungano wa Afrika katika shughuli za kubadilisha masharti ya utaratibu wa Mahakama ya kimataifa ili kuwazuia marais wanaohudumu kutakikana kuhudhuria kesi zao katika mahakama ya kimataifa.
Mwaka wa 2013, kabla ya kuchukua hatamu kama Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Balozi Mohamed alikuwa amejaribu kujaza nafasi ya Mkurugenzi Mkuu katika Shirika la Kimataifa la kibiashara. Iwapo angefanikiwa, angekuwa sio tu mwanamke bali Mwafrika wa kwanza kufanya hivyo.
Mapema katika taaluma yake, Balozi Mohamed alishiriki katika uandishi wa kielelezo na majadiliano ya mapatano ya Afrika kuhusu haki za mtoto. Na hivi majuzi, mwaka wa 2017, kampeni zake za kuwa mwenyekiti wa kwanza wa kike kutoka Afrika kwenye Tume ya Muungano wa Afrika, AU, hazikuzaa matunda, alipoteza nafasi hiyo kwa Moussa Mahamat kutoka Chad.
Balozi Mohamed alibahatika kuwa na mama aliyejitahidi kuhakikisha kwamba binti yake anaelimika, badala ya kuolewa katika umri mdogo sawa na inavyoshuhudiwa katika jamii za kuhamahama na hasa yake ya Somali. Kwa sasa, Balozi Mohamed ameolewa na ni mama wa watoto wawili.
Uamuzi wake kupanga watoto wanne wengine, vilevile kukaa nchini Kenya na mamake babake alipougua mwisho wa miaka ya themanini, kunadhihirisha jinsi anavyothamini familia.
Hadithi ya Balozi Mohamed ni ya msichana mdogo ambaye wakati mmoja sare zake za shule zilibanwa na kukunjwa ili zimtoshe, lakini sasa anasimama kama mojawapo ya watu wanaoheshimika sio tu hapa Kenya, bali pia kimataifa.