Makala

MWANAMKE MWELEDI: Aweka kumbukumbu kuchaguliwa mbunge

January 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KEYB

ALIENDA kinyume na matarajio na kuwa mwanamke wa kwanza kutoka eneo la Kaskazini Mashariki kuchaguliwa mbunge.

Sophia Abdi Noor ndilo jina lake, ambapo katika uchaguzi wa mwaka wa 2017 alishinda kiti cha eneo bunge la Ijara kupitia chama cha Party of Reforms and Development (PDR).

Alijitosa katika siasa mwaka wa 2008, kama mbunge mteule wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) katika Bunge la kumi. Kuchaguliwa kwake katika Bunge la Kitaifa kuliandikisha jina lake kwenye vitabu vya kumbukumbu, hasa ikizingatiwa kwamba anatoka katika eneo ambalo bado limeshikilia ukale, ambapo hakuna mwanamke alikuwa amewahi kuchaguliwa katika wadhifa wa kisiasa.

Lakini safari yake ya kisiasa ilianza mwaka wa 1997 ambapo alikuwa mwanamke wa kwanza kutoka eneo hilo kuwania kiti cha ubunge. Hata hivyo, uteuzi wake ulitupiliwa mbali kwa misingi ya kitamaduni na kidini kwamba mwanamke hawezi kuongoza jamii ya Kiislamu.

Kabla ya kujiunga na siasa, Bi Noor alikuwa ashajiundia taaluma. Alikuwa mwanzilishi wa Womankind Kenya, shirika linaloendesha kampeni dhidi ya ndoa za mapema na ukeketaji. Shirika hilo pia huwaokoa wasichana mayatima na wale wako katika hatari ya kutahiriwa kwa kuwasaidia kupata elimu.

Alihudumu kama mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya Yuga Girls’ kati ya mwaka wa 1989 na 1992. Alikuwa mwanachama wa Baraza la Kitaifa la huduma za watoto kati ya mwaka 2005 na 2008. Alipendekezwa na Wizara ya Elimu ili kujiunga na Hazina ya elimu ya watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) eneo la Garissa. Akiwa hapo, alikumbana ana kwa ana na tukio la ukeketaji katika mojawapo ya vijiji alivyokuwa akizuru. Msichana mhusika alifariki akipelekwa hospitalini.

Ni tukio lililofufua kumbukumbu za kutisha akiwa mtoto, jambo ambalo bado yeye hukiri wazi kwamba linaendelea kumsumbua hadi sasa, na ambalo lilimsababishia matatizo mengi wakati wa hedhi na kujifungua. Ni suala lililomsukuma kujitosa katika vita dhidi ya utamaduni huu, licha ya kuendelea kupokea pingamizi.

Aidha, Bi Noor alifanya kazi na mashirika mengine kama vile CARE International, MSF-Uhispania, United Nations High Commissioner for Refugees (UNHCR), Oxfam, Save the Children, World Vision na MIKONO International.

Mwaka wa 2008 alipoteuliwa kama mbunge, Bi Noor aliteuliwa pia kama Naibu Mwenyekiti wa muungano wa wanawake wabunge na kuhudumu kati ya 2008 na 2013.

Bi Noor ana stashahada katika masuala ya huduma kwa jamii.

Aidha ana shahada ya digrii katika masuala ya ustawi wa kijamii kutoka Chuo Kikuu cha Arusha, na shahada ya uzamili katika masuala ya ustawi wa usimamizi wa masuala ya utendaji kutoka Chuo Kikuu cha United States International University.