Makala

MWANAMKE MWELEDI: Jina lake sawia na Uanahabari

July 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KEYB

NI vigumu kwa gumzo kuhusu historia ya fani ya habari kukamilika pasipo kulitaja jina lake.

Huku taaluma yake Catherine Kasavuli ikidumu zaidi ya miongo mitatu, uso wake ulikuwa miongoni mwa sura maarufu zilizopamba televisheni zetu nchini Kenya mwanzo wa miaka ya tisini, wakati matangazo kwa lugha ya Kiingereza yalizinduliwa.

Hasa jina lake lilitambulika kutokana na ustadi wake kitaaluma kwenye skrini, vilevile uteuzi na matumizi ya maneno, suala lililomfanya kuwa mmojawapo wa wanahabari walioheshimika katika historia ya utangazaji nchini Kenya.

Ni umahiri huu uliompa fursa ya kuhudumu kama mtangazaji wa vituo mbalimbali vya televisheni.

Na katika harakati hizo, alijishindia mashabiki kibao suala lililomfanya kubandikwa jina Catherine The Great, sawa na aliyekuwa malkia wa Uingereza.

Yeye ni mmoja wa watangazaji waliochochea kizazi cha wanahabari wa kike wa sasa, enzi ambazo taaluma ya utangazaji iliheshimika na kuenziwa.

Na kama wasemavyo kwamba chanda chema huvikwa pete, Kasavuli ametambuliwa katika majukwaa mbalimbali kutokana na mchango wake katika uanahabari, ikiwa ni pamoja na Order of The Grand Warrior, tuzo aliyopokea kutoka kwa Rais wa zamani, Mwai Kibaki.

Alilelewa eneo la Nairobi West jijini Nairobi, ambapo alikuwa mwanafunzi wa zamani wa shule ya upili ya wasichana ya Ngara Girls’.

Safari yake kama mwanahabari ilianza mwaka wa 1980 kama mtangazaji wa redio wa idhaa ya kitaifa wakati huo Voice of Kenya (VOK), kwa sasa ikijulikana kama shirika la habari la Kenya (Kenya Broadcasting Corporation (KBC).

Wakati huo alikuwa mchanga kiumri ambapo hakuwa bado amepata mafunzo ya taaluma hii. Alijiunga na chuo cha mafunzo ya Uanahabari cha Kenya Institute of Mass Communication miaka miwili baada ya kuanza kazi hii, kisha 1985 akajitosa rasmi katika fani ya televisheni.

Alionekana kwenye televisheni mara ya kwanza nchini Kenya, wakati ambapo kulikuwa na kituo kimoja cha televisheni cha habari, VOK, kilichokuwa kikiendeshwa na serikali.

Miaka kadha baadaye alijumuisha kikosi cha wahusika wakuu waliochangia pakubwa kuzinduliwa kwa kituo cha Kenya Television Network (KTN), mwezi Machi 1990.

Ni hapa ndipo alipohudumu kwa miaka mingi huku akijiundia jina na kujikusanyia mashabiki.

Alijiunga na kampuni ya habari ya Royal Media Services mwaka wa 2007 ambapo alikuwa mtangazaji wa kwanza kuendesha matangazo ya moja kwa moja kwenye kituo cha televisheni cha Citizen TV.

Alistaafu kutoka utangazaji mwaka wa 2013 huku akihudumu kama msimamizi wa masuala ya mahusiano mema wa kampuni ya Royal Media Services.

Mbali na hayo, yeye ni mwanzilishi wa Kasavuli Media Group Ltd, chuo cha utangazaji kinachosaidia wanafunzi kupiga msasa ujuzi wao wa kutangaza.

Aidha, chuo hicho hutoa mafunzo ya taratibu za itifaki, utaalamu, miiko na adabu kwa umma.